Erik ten Hag: Manchester United 'inahitaji wachezaji bora'

Chanzo cha picha, Getty Images
Meneja wa Manchester United Erik ten Hag amesema klabu hiyo "inahitaji wachezaji wenye ubora" baada ya kukubali kiwango cha kikosi hicho kuwa hakiridhishi.
United walichapwa mabao 4-0 na Brentford wakiruhusu manne katika dakika 35 za kwanza , na mpaka sasa hawana alama yoyote baada ya mechi mbili za Premier League.
Mholanzi Ten Hag, ambaye alichukua mikoba ya Old Trafford mwezi Mei, aliiambia Sky Sports kwamba hali hiyo "ina mchakato mgumu".
"Lazima tupate wachezaji wenye viwango vya juu kuliko vile tulivyofanya leo," alisema.
"Sisi, kama timu, tupo kwenye mchakato mgumu. Unatarajia mwanzo tofauti. Sio tulivyotarajia.
"Tunahitaji wachezaji wapya. Tunahitaji wachezaji wenye ubora. Tunafanyia kazi hilo na tutafanya kila kitu kuwashawishi waje."
United wamekuwa wakiwawinda kwa muda mrefu wachezaji wapya tangu dirisha la usajili lilipofunguliwa, kufuatia kiwango kibovu msimu uliopita sambamba na kushindwa nyumbani na Brighton Jumapili iliyopita.
Kiungo wa kati wa Barcelona Frenkie de Jong amekuwa akilengwa sana na Ten Hag lakini mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 ameripotiwa akisema kwamba angependelea kujiunga na Chelsea ikiwa ataondoka Nou Camp.
Uhamisho wa kumnunua mshambuliaji wa zamani wa Stoke na West Ham Marko Arnautovic ulileta mtizamo hasi kwa mashabiki tofauti na ilivyokua kwa kiungo wa Juventus Adrien Rabiot ,uhamisho ambao unaonekana kukaribia kukamilika.
"Timu inapaswa kuwajibika. Ninawaonea huruma sana mashabiki walifanya juhudi zote kutuunga mkono lakini tuliwaangusha," alisema Ten Hag.
"Lazima muwajibike uwanjani kama timu na mtu mmoja mmoja, hilo hatukufanya, nilichowaomba ni kucheza kwa imani na kuwajibika kwa utendaji, lazima tulifanyie kazi.
"Meneja anawajibika pia. Ana jukumu kuu na nitachukua hilo na kulifanyia kazi."
'Nimeigharimu timu yangu pointi tatu' - De Gea
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wakati Ten Hag akihisi kwamba timu yake kwa ujumla ilipaswa kulaumiwa kwa kuonyesha kiwango kibovu kupindukia dhidi ya kikosi cha Thomas Frank, mlinda mlango wa United David de Gea alijinyooshea kidole cha lawama.
Akijipendekeza mwenyewe kufanya mahojiano baada ya mchezo huo, aliiambia Sky Sports: "Ninapokea lawama zote dhidi yangu leo. Nafikiri niligharimu pointi tatu kwa timu yangu. Ilikuwa ni matokeo mabaya kutoka kwangu."
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uhispania aliruhusu goli la Josh Dasilva kutoka kwenye shuti la mbali kumpita kirahisi.
"Baada ya kosa la kwanza na kisha la pili, ilikuwa ngumu sana kwa wachezaji wenzangu," De Gea aliongeza. "Kwa sasa, ni ngumu kila tunaporuhusu bao. Ninapaswa kuokoa mkwaju wa kwanza - [kama ningepata] matokeo yangekuwa tofauti."
United sasa wamepoteza mechi nne mfululizo za ligi, hii ikijumuisha pia michezo ya mwisho wa msimu uliopita - na mechi saba mfululizo za ugenini katika ligi kuu ya EPL.












