Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Urusi inakaribia kuishiwa nguvu nchini Ukraine - Mkuu wa MI6
Urusi inapambana kudumisha kampeni yake ya kijeshi na Ukraine na inaweza kuwa na uwezo wa kujibu mashambulizi, mkuu wa idara ya kijasusi ya kigeni ya Uingereza amesema.
Mkuu wa MI6 Richard Moore alisema Urusi imeshuhudia"anguko la kihistoria" katika malengo yake ya awali ya kumwondoa rais wa Ukraine, kuichukua Kyiv na kuweka mgawanyiko katika nchi za Magharibi.
Ameyasema hayo wakati akizungumza katika Jukwaa la Usalama la Aspen, ambapo ni nadra sana kuonekana hadharani.
Aliita uvamizi huo "kitendo cha wazi zaidi cha uchokozi ... kwa Ulaya tangu Vita vya Pili vya Dunia."
Alisema mafanikio ya hivi karibuni ya Urusi yalikuwa "madogo" na kwamba Urusi "inakaribia kuishiwa nguvu".
"Tathmini yetu ni kwamba Warusi watazidi kupata ugumu wa kupata nguvukazi na nyenzo katika wiki chache zijazo," Bw Moore alisema katikaa mkutano huko Colorado. "Watalazimika kusimama kwa namna fulani na hiyo itawapa Waukraine fursa ya kurudisha mashambulio."
Mtazamo huo unaweza kuonekana kuwa wa matumaini na uwezo wa Ukraine wa kukabiliana na mashambulizi unaweza kutegemea usambazaji mkubwa wa silaha za Magharibi ambazo maafisa wake wanasema mara nyingi umekuwa wa polepole sana kufika.
Mkuu wa MI6 alisema aina fulani ya mafanikio katika uwanja wa vita yatakuwa "ukumbusho muhimu kwa Ulaya yote kwamba hii ni kampeni ya kushinda" haswa kabla ya msimu wa baridi ambao kuna uwezekano wa kuona shinikizo kwenye usambazaji wa gesi.
"Tuko kwenye wakati mgumu," alisema. Sababu zaidi ya kudumisha uungwaji mkono kusaidia Waukraine kushinda au "angalau kujadiliana kuhusu nafasi yenye nguvu kubwa", alisema, ni kwa sababu kiongozi wa China Xi Jinping "alikuwa akitazama kama mwewe (kwa umakini)".
"Hakuna ushahidi kwamba [Rais Vladimir] Putin anasumbuliwa na tatizo la kiafya," alijibu alipoulizwa, akirejea maoni ya Mkurugenzi wa CIA William Burns katika Jukwaa hilo jana.
Takriban maafisa 400 wa ujasusi wa Urusi wanaofanya kazi kwa siri wamefukuzwa kote Ulaya, alisema, na kupunguza nusu ya uwezo wa Urusi wa kufanya ujasusi katika bara hilo.
"Mlango wetu uko wazi kila wakati," alisema linapokuja suala la kuajiri maafisa wa Urusi waliojitenga ili kupeleleza kwa ajili ya Uingereza.
MI6 inaweka juhudi nyingi China
Kuhusu China, alisema MI6 "haijawahi kuwa na udanganyifu wowote kuhusu Ukomunisti wa China".
Alifichua kuwa MI6 sasa imejitolea zaidi kwa China kuliko kitu kingine chochote, juhudi katika suala hili zimepita hata ambazo zilijitolea kukabiliana na ugaidi.
Alisema ilikuwa "mapema mno kueleza" ni somo gani China itapata kutokana na hatua ya Putin nchini Ukraine, lakini kulikuwa na ishara nyingi maafisa wa Beijing walifanya kazi kupita kiasi ili kufahamu wanachofikiria. "Ni vigumu sana kusoma kwa sasa," alisema.
Alisema ilikuwa "muhimu" kukumbusha uongozi wa China jinsi uvamizi wa Taiwan unaweza kwenda vibaya. Alisema uongozi wa China ulidharau azimio na uwezo wa Marekani na hii inaweza kuwafanya wafanye makosa. "Sidhani ni jambo lisiloepukika," alisema alipoulizwa kuhusu mzozo huo mkubwa.
Kuhusu Iran, alisema makubaliano ya nyuklia "yapo mezani kabisa", lakini alikuwa na shaka kwamba Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei anataka kutia saini makubaliano hayo.
Pamoja na vikwazo vyote, alisema makubaliano ya awali bado yalikuwa njia bora zaidi ya kuzuia mpango wa nyuklia wa Iran.
Alipoulizwa kama kujiondoa kwa mataifa ya Magharibi kutoka Afghanistan mwaka jana kulifanya iwe vigumu kukabiliana na vitisho, alikiri "hili lilikuwa kinyume kwetu lilipotokea na sasa ni vigumu zaidi". Alisema itahitaji kutafuta "njia tofauti" za kukabiliana na tishio la kigaidi la Kiislamu, ikiwa ni pamoja na kufanya kazi na washirika ambao MI6 inaweza kutoshughulika nao kwa kawaida.
Alipoulizwa kutafakari juu ya hali ya siasa na vurugu nchini Marekani, mkuu wa MI6 alipuuza swali hilo, lakini alisisitiza "upendo wake mkubwa" kwa Marekani, ambako alisoma na kufanya kazi yake ya kwanza ya kulipwa akiwa kijana.
Alimsahihisha aliyekuwa akimhoji kwa kusema kuwa kazi hii imekuwa kama mhudumu wa ufukweni badala ya kuwa muokoaji. "Sikuwa na mwili wa hilo," alisema kwa kicheko kutoka kwa watazamaji.