Mgonjwa wa saratani kutoka Marekani aliyepata 'lafudhi' ya Ireland ghafla

Iliyochapishwa

Mgonjwa huyo, ambaye aligunduliwa kuwa na saratani ya tezi dume, alipata "lafudhi isiyoweza kudhibitiwa ya Kiayalandi", licha ya kuwa hajawahi kutembelea Ireland au kuwa na jamaa yoyote wa Ireland.

Kulingana na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Duke na Kituo cha Utafiti wa Urolojia cha Carolina nchini Marekani, ugonjwa wa mwanamume huyo "uliendana na dalili za lafudhi za kigeni (SAE)."

Madaktari wanaowasilisha kesi hiyo iliyochapishwa katika jarida la matibabu la British Medical Journal (BMJ) wanaeleza kuwa ugonjwa huo ambao ni nadra, ulidumu kwa takriban miezi 20 hadi kifo chake.

"Kwa ufahamu wetu, hili ni tukio la kwanza la SAE lililoelezewa kwa mgonjwa aliye na saratani ya kibofu na ya tatu inaelezewa kwa mgonjwa aliye na ugonjwa mbaya (metastasis)," waandishi walibainisha.

Utafiti wa 2008 uliofanywa katika Chuo Kikuu cha Antwerp nchini Ubelgiji unaelezea SAE kama "shida ya usemi ambayo husababisha matamshi ambayo yanatambulika wazi kuwa ya kigeni."

Watafiti walibaini kuwa ugonjwa huo "umethibitishwa vizuri" kwa watu wazima walio na vidonda vya ubongo ambavyo vinaathiri mtandao wa ubongo ambao unadhibiti lugha.

Lakini pia walieleza kuwa kuna ripoti za wagonjwa ambao SAE ilitokana na ugonjwa wa akili.

Tafiti nyengine, hata hivyo, zinaonyesha kwamba SAE inatokana na kiharusi au kuendelea kutokana na maumivu ya kichwa au matatizo ya ukuaji.

Kulingana na utafiti, ugonjwa huo unaonekana kutokea kwa sababu ya uharibifu wa maeneo maalum ya lugha ya ubongo.

Uharibifu huu husababisha "upotoshaji wa michakato ya kutamka na uratibu" na kusababisha sikio ambalo halijazoezwa kuhisi kuwa wale walio na SAE wanazungumza lugha nyingine au kwa lafudhi ya kigeni.

Watafiti ambao wamesoma tatizo la SAE, hata hivyo wanasema kwamba licha ya hadithi maarufu kuhusu wagonjwa walio na uharibifu wa ubongo au mishipa, kuzungumza lugha ya kigeni au lafudhi baada ya kuumia, "hakujawa na kesi zilizothibitishwa kuwa wagonjwa wanaopata lafudhi hiyo ya kigeni huimarika na kuanza kuzungumza vizuri baada ya kuumia kuathiika katika ubongo.

‘Lafudhi isiodhibitika’

Kwa upande wa mgonjwa huyo wa Marekani, jina na uraia wake havikutajwa, lakini mtu huyo aliripotiwa kuishi Uingereza alipokuwa na umri wa miaka 20 na alikuwa na marafiki na familia ya mbali kutoka Ireland.

Hatahivyo, waandishi wanasisitiza katika BMJ, hakuwahi kuzungumza na lafudhi hii ya kigeni hapo awali.

"Lafudhi yake haikuweza kudhibitiwa, ilikuwepo katika mazingira yote, na polepole ikaendelea," watafiti wanasema.

Hii inaonekana kuwa moja ya kesi nadra sana ambayo hujitokeza .

"Hakuwa na kasoro za uchunguzi wa neva, hakuna historia ya tatizo la kiakili, au kasoro za MRI za ubongo wakati wa kuanza kwa dalili," watafiti wanaelezea.

Na wanashuku kuwa sababu ya SAE katika mtu huyu ilikuwa shida inayoitwa paraneoplastic neurological syndrome.

Ugonjwa huo unaweza kutokea kwa wagonjwa wengine wa saratani ambao mfumo wao wa kinga hushambulia sehemu za ubongo, uti wa mgongo, neva, au misuli.

Mgonjwa huyo alitibiwa kwa chemotherapy lakini ugonjwa wake, saratani ya neuroendocrine ya tezi dume, uliendelea.

Hii ilisababisha metastasis ya ubongo na kupooza kwa kasi ambayo ilisababisha kifo chake.

Watafiti wanasema kesi ya mgonjwa huyu inasisitiza hitaji la utafiti zaidi juu ya dalili za lafudhi za kigeni.

"Tatizo hili lisilo la kawaida linaonyesha umuhimu wa maandiko ya ziada juu ya SAE na ugonjwa wa neva wa paraneoplastic unaohusishwa na saratani ya kibofu ili kuboresha uelewa wa viungo kati ya ugonjwa huu nadra," ripoti inahitimisha.

Matukio mengine

BBC imeandika matukio mengine ya watu wenye matatizo ya SAE.

Mnamo 2006, Mwingereza Linda Walker alipatwa na kiharusi na akapata lafudhi yake ya Kiingereza ya Kaskazini imebadilishwa na "ile ya lafudhi ya kijamaika".

Kesi nyingine ilikuwa ya Julie Matthias, 49, Mwingereza ambaye aliachwa akizungumza kwa lafudhi tofauti za kigeni, zikiwemo za Afrika Kusini, Ufaransa na Italia.

Julie alipata SAE baada ya kupata maumivu makali ya kichwa mwaka wa 2011 na alipata dalili nyingine kama kiharusi, ikiwa ni pamoja na kupooza kwa upande wa kulia.

Mojawapo ya kesi za kwanza kuripotiwa ilikuwa mwaka wa 1941 wakati msichana mdogo wa Norway alianzisha lafudhi ya Kijerumani baada ya kupigwa na vipande vya bomu wakati wa mashambulizi ya anga ya Vita vya dunia vya pili.

Mwanamke huyo aliepukwa na wenyeji waliodhani kuwa ni jasusi wa Nazi.