Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mafuriko mabaya yakumba katikati ya Somalia
- Author, Rhoda Odhiambo
- Nafasi, BBC News, Beledweyne, Somalia
- Iliyochapishwa
Kuna bahari ya mahema ya plastiki yenye rangi nyeupe, chungwa na samawati hadi katika upeo ambao macho yanaweza kuona kwenye Kambi ya Waliohamishwa ya Shabelle, huko Beledweyne.
Nyumbani kwa takriban watu 43,000, makazi haya ya muda yameegemezwa kwa vijiti na familia zilizokata tamaa ambazo zimekimbia makazi yao katika eneo la Beledweyne katika Somalia ya Kati kutokana na mafuriko makubwa.
Mmoja wa wanaoishi hapa ni Ahmed Omar mwenye umri wa miaka 25.
“Nilipokuja kwenye kambi hii sikubeba mengi. Kila mtu alikuwa akikimbia kuokoa maisha yake, niliweza kubeba kitanda kimoja tu, godoro na vyombo vichache,” anasema.
Omar hakumbuki ni siku ngapi amekaa kambini, lakini ana wasiwasi kwamba wakati yuko salama, baba yake hayupo.
"Baba yangu anakaa katika eneo ambalo barabara zimekatika kutokana na mafuriko. Amekwama," Omar anasema.
Omar ananong'ona kuwa ana njaa sana lakini anajali zaidi mke wake na watoto wake wawili watakula nini. Ndani ya hema lao, mke wake ananyonyesha mtoto wao ambaye ana umri wa miezi mitano hivi.
Tangu Oktoba, viwango vya juu vya mvua visivyo vya kawaida vimenyesha kote Afrika Mashariki, vikiwa vibaya zaidi kutokana na athari ya pamoja ya matukio mawili ya hali ya hewa - El Niño na Dipole ya Bahari ya Hindi.
Mafuriko haya yamekuwa mabaya sana kwa Somalia kwa sababu yanafuatia misimu mitano mfululizo ya ukame. Makumi ya maelfu ya watu - ikiwa ni pamoja na watoto - wanakisiwa kufa kutokana na njaa nchini humo huku mazao yakifeli tena na tena. Mamilioni ya watu waliacha nyumba zao kutafuta chakula na maji. Sasa kutokana na mvua kubwa kunyesha, maeneo makubwa ya nchi yamekwama na mafuriko zaidi yanatabiriwa.
Kilomita chache kutoka kwa Kambi ya Shabelle ni Kituo cha Afya cha Eljalle, mojawapo ya vituo vikubwa zaidi vya matibabu katika eneo hilo. Wahudumu wa afya hapa wamezidiwa na idadi kubwa ya wagonjwa wanaohitaji huduma.
Muuguzi mkuu katika Kituo cha Afya cha Eljalle, Abdulkadir Dahir Afrah, anasema zaidi ya nusu ya watu wanaoishi Beledweyne wanaomba matibabu katika kituo hicho.
“Tangu mafuriko yaanze idadi imekuwa ikiongezeka kila siku, awali tulikuwa tukipokea wagonjwa walioathirika na ukame lakini sasa hivi tunashuhudia wagonjwa wengi hasa watoto wanaougua magonjwa yatokanayo na maji,” alisema. anasema.
Wahudumu wa afya katika kituo hicho wanasema wanafuatilia magonjwa ya typhoid, kipindupindu, homa ya dengue, malaria na ugonjwa wa tumbo.
Hivi majuzi Mariam Musa alisafiri hadi katika kambi ya Shabelle kutafuta matibabu ya mtoto wake.
“Amegundulika kuwa anaharisha na pia anatapika,” anasema.
"Madaktari wamenipa baadhi ya dawa za kumsaidia apone, lakini shida yangu sina chakula cha kutosha nyumbani cha kumpa, nimepoteza kila kitu kutokana na mafuriko, pia anapona utapiamlo [tangu awali kwa ajili ya ukame]."
Kulingana na wataalamu wa hali ya hewa , mji wa Beledweyne unakabiliwa na mafuriko kwa sababu ya eneo lake kwenye ardhi ya chini kati ya milima. Mafuriko ya ghafla katika nyanda za juu za Ethiopia yanaingiza kiasi kikubwa cha maji kwenye mto Shabelle, ambao unapita katikati ya mji, na kusababisha mto huo kuvunja kingo zake.
Mji huo ulikuwa wa jamii iliyochangamka, ya kibiashara, lakini sasa wilaya nzima zimejaa maduka na nyumba chini ya mkondo wa maji.
Ripoti ya UN Habitat inabainisha sehemu nne za mji ambapo mto huo huenda ukapasua kingo zake tena. Ilisema serikali inahitaji kujenga vizuizi vya kujihami na kuimarisha tuta ili kuzuia kufurika maji.
Hata hivyo, mwanamume anayesimamia kazi ya kuratibu misaada ana maoni tofauti. Mohammed Maalim, mshauri mkuu katika Mamlaka ya Kudhibiti Majanga ya Somalia, anafikiri chaguo pekee ni kuwahamisha watu wa eneo hilo.
"Jambo bora zaidi ni kuhama kabisa kwa mji na kujenga mji mpya. Hii ndiyo njia pekee kwa sasa kwa sababu hii imekuwa ya mara kwa mara. Inawezekana tu kupitia utashi wa kisiasa," anasema.
Tatizo jingine ni eneo la mji huo katika shimo kati ya milima ambayo ina maana kwamba barabara zimekatika na kupata misaada kwa jamii zilizoathirika ni changamoto.
"Inatuweka katika hali ngumu sana. Kwa upande mmoja, bila shaka, sisi ni mamlaka inayotarajiwa kujua [jinsi ya] kujibu hili. Na tunajaribu kadri tuwezavyo - nadhani kila mtu serikalini anajaribu hilo. ,” anasema Maalim.
Maalim anasema maafa ya mwaka huu ni sawa na mafuriko ambayo yalizamisha Beledweyne mwaka 1997, na kuua karibu watu 450 na wengine zaidi ya 150,000 kuyahama makazi yao.
Kwa sasa, mamlaka nchini Somalia zinatoa wito kwa jamii ya kimataifa kuwasaidia walioathirika.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah na kuhaririwa na Ambia Hirsi