Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Gudaf Tsegay: Alishinda ubingwa wa dunia wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe Ethiopia
Guduf Tsegay amekuwa bingwa wa dunia mara mbili, akishinda taji la mita 10,000 kwenye Mashindano ya Riadha ya Dunia huko Budapest. Muethiopia huyo pia alishinda taji la mita 5000 kwenye Mashindano ya Dunia ya 2022. Taji la dunia la Gudaf Tsegay katika mbio za mita 5000 ni miongoni mwa mafanikio makubwa zaidi ya maisha yake, lakini aliposimama kwenye jukwaa kupokea medali yake ya dhahabu Julai 2022 alikuwa akipitia shida binafsi.
Msichana huyo mwenye umri wa miaka 25 hakuwa amezungumza na wazazi wake na ndugu zake kwa miezi kadhaa. Tsegay anatoka Tigray, eneo la kaskazini mwa Ethiopia ambalo lilikuwa kitovu cha vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya Novemba 2020 na Novemba 2022, huku wanajeshi wa serikali wakipambana na vikosi vya Tigrayan vinavyopigania uhuru.
Mzozo huo uligharimu maisha ya maelfu ya watu. Babaraza za kuelekea Tigray zilifungwa, vilevile serikali ilizima huduma za simu na intaneti.
"Kutoweza kuzungumza na baba na kaka ambao wamekuwa wakikushauri kujitahidi na kupata mafanikio zaidi kila siku ni vigumu sana. Ni vigumu hata kueleza," Tsegay aliambia BBC. "Sikuzungumza nao kwa miezi 18."
Licha ya kutengana na familia na wasiwasi, Tsegay aliendelea na mazoezi katika mji mkuu wa nchi hiyo Addis Ababa na mumewe, ambaye pia ni kocha wake, Hiluf Yihdego - nguzo yake katika kipindi kigumu. Kazi yao ilizaa matunda katika mashindano makubwa ya mwaka jana.
"Ni mume wangu nyumbani na kocha uwanjani. Alinisaidia sana nilipokuwa na huzuni, alikuwa karibu nami," anasema Tsegay.
"Nimefanikiwa kwa sababu nilifanya kazi kwa bidii licha ya changamoto zote. Nilisherehekea mafanikio yangu na mume wangu na marafiki."
"Kwa mwanariadha kujiona kuwa amefanikiwa ni kushinda Olimpiki na Mashindano ya Dunia - hiyo ilikuwa ndoto yangu na niliifanikisha."
Usiku wa Hofu
Usiku mmoja mnamo Desemba 2021, Tsegay na mumewe waliamshwa kutoka usingizini na vikosi vya serikali vilivyomchukua Yihdego. Zaidi ya mwaka mmoja baadaye, anakumbuka kwa machozi usiku huo.
"Nililia usiku mzima. Nilikuwa na wasiwasi wangerudi kunichukua kila mlango unapogongwa."
Yihdego aliachiliwa baada ya siku moja lakini anasema ilikuwa tukio la kuogofya kwani wanajeshi walidai kuwa 'junta', neno linalotumiwa na vikosi vya serikali kwa wapiganaji wa Tigrayan na mtu yeyote anayefanya kazi nao.
"Askari 20 walikuja nyumbani kwangu katikati ya usiku," aliambia BBC.
Anaongeza, "walinishutumu kwa kuunga mkono chama cha Tigray People's Liberation Front, kuwapeleka wanariadha wa Tigrayan nje ya nchi, na kuhifadhi dola nyumbani. Walipekua nyumba yangu; inaonekana ni rahisi kuizungumzia sasa lakini ilikuwa ngumu."
Mwezi Novemba mwaka jana makubaliano ya amani yalitiwa saini nchini Afrika Kusini kati ya serikali ya Ethiopia na wapiganaji wa Tigrayan. Mawasiliano yaliporejeshwa, Tsegay hatimaye aliweza kuifikia familia yake ili kusherehekea mafanikio yake.
"Baada ya makubaliano ya amani familia yangu ilipiga simu na kuelezea furaha yao," anasema. "Ingekuwa vizuri kama wazazi wangu wangeniona na kuwa pamoja nami. Waliniambia baadaye walitazama mbio na kulia."
Sasa, Tsegay analenga Olimpiki ya mwaka ujao huko Paris.
"Mimi ni bingwa wa ndani, mimi ni bingwa wa dunia, lakini linapokuja suala la Olimpiki, mimi ni mshindi wa medali [shaba katika mita 5,000 huko Tokyo], sio bingwa.
"Kwa hiyo nataka kuwa bingwa wa ulimpiki. Ninaamini ninaweza kufikia lengo langu."