Ferdinand Omanyala aishindia Kenya dhahabu ya kwanza michezo ya madola Birmingham

Ferdinand Omanyala

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ferdinand Omanyala
Iliyochapishwa

Mwanariadha wa Kenya katika mbio za mita 100 ferdinand Omanyala kwa mara nyengine ameushangaza ulimwengu baada ya kuibuka mshindi katika mashindano ya nchi za jumuiya ya madola mjini Birmingham Uingereza

Omanyala aliyeandakisha muda wa sekundę 10.02 aliipatia Kenya medali yake ya kwanza ya dhahabu katika mashindano hayo baada ya kumshinda bingwa mtetezi wa mashindano hayo Akani Simbine kutoka Afrika kusini aliyechukua nafasi ya pili.

Yupun Abeykoon kutoka Sri Lanka alimaliza wa tatu na hivyobasi kujipatia medali ya shaba kwa kumaliza katika muda wa sekunde 10.14.

Ushindi huo wa Omanyala unamweka katika vitabu vya kumbukumbu kama mwanariadha wa kwanza Mkenya katika miaka 60 kumaliza wa kwanza katika mbio za mita 100 za Wanaume katika mashindano hayo.

Mwanariadha wa kwanza kuishindia Kenya medali ya dhahabu katika mbio hizo alikuwa Seraphino Antao mwaka wa 1962.

Omanyala ambaye ndiye bingwa wa Afrika katika mbio hizo amelipiza kisasi cha mashindano ya dunia ya ulimwengu ambapo alishindwa kufanya vyema baada ya kuwasili saa tatu kabla ya kushiriki .

Hali hiyo ilitokana na kuchelewa kwa visa yake ya kuelekea nchini Marekani ambapo mashindano hayo yalikuwa yakiandaliwa.

Maelezo ya sauti, Ferdinand Omanyala aishindia Kenya dhahabu ya kwanza michezo ya madola Birmingham

"Tumekuwa tukitarajia hili na shukrani kwa timu yangu na Wakenya ambao wameniunga mkono katika safari hii," alieleza Omanyala.

"Najisikia vizuri, najua itachukua muda ili kuamini . Ninajisikia vizuri mbele ya umati huu ulionikubali, alinukuliwa na mtandao wa Daily Nation akisema”

Omanyala alisema ushindi huo ni motisha kubwa kuelekea msimu ujao ambapo kutakuwa na Mashindano ya Riadha ya Dunia huko Budapest, Hungary na Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024.

Omanyala anatumai kuwa ushindi huo utaendelea kuwatia moyo na kuwatia moyo Wakenya wengi na kufungua njia kwa wanariadha wengi wa siku zijazo.

"Ilihitaji mtu kuvunja kizuizi kwa sababu kutakuwa na wanariadha wengine wengi wanaokuja. Itakuwa na athari kubwa sasa kwa kuwa nina medali mbili za dhahabu za ubingwa na rekodi ya Afrika,” alibainisha Omanyala, ambaye ana kiwango bora zaidi cha sekunde 9.77.

Omanyala alisema kuwa alitumia changamoto alizokumbana nazo kuelekea Mashindano ya Riadha ya Dunia yaliyomalizika hivi punde huko Oregon kama hatua ya kufikia matokeo mazuri.