IGP Wambura na kibarua 'kizito' cha kuutafuna mfupa mgumu Polisi Tanzania

Iliyochapishwa

Na Yusuph Mazimu, BBC Swahili

Rais Samia Suluhu amefanya mabadiliko katika Jeshi la Polisi nchini Tanzania, kwa kumteua mkuu mpya wa Jeshi la Polisi, Camillus Wambura ambaye pia amepandishwa cheo kutoka Kamishna wa Polisi, kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP).

Wambura anachukua nafasi ya aliyekuwa Mkuu wa Polisi, Simon Sirro ambaye ameteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.

Rais Samia pia amempandisha cheo Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ramadhan Kingai kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Wambura, aliyeteuliwa kuongoza jeshi zima.

Kadhalika amemteua Kamishina wa polisi (CP) Hamad Khamis Hamad kuwa Kamishna wa Polisi Zanzibar akichukua nafasi ya Kamishna wa Polisi Awadhi Juma Haji aliyeteuliwa kuwa mkurugenzi wa operesheni Makao Makuu.

Pamoja na mabadiliko haya kuzua mjadala mitandaoni kutokana na mitazamo ya watu, kwa vyovyote vile yalilazimika kufanyika kutokana na picha ya Jeshi hilo machoni pa watu. 

Mabadiliko haya yana maana gani?

Mabadiliko haya katika Jeshi la Polisi Tanzania, si ya mara ya kwanza, kumekuwa na mabadiliko mengi ndani ya jeshi hilo, lakini mabadiliko ya sasa ni kama yalikuwa yakingojewa kwa muda hivi kutokana na sifa ya jeshi hilo katika miaka ya hivi karibuni.

Ukiuliza leo watanzania kuhusu mtazamo wao na imani yao kwa jeshi hilo hasa linapokuja kwenye suala la maadili ya watendaji wake, wengi watakuonyesha mashaka.

Mashaka hayo hata Rais Samia ameyaonesha mara kadhaa anapolizungumzia jeshi hilo hadharani.

'Vitendo vinavyofanywa na askari polisi barabarani, huwezi kudhani kwamba wamehitimu mafunzo', anasema Rais Samia mara baada ya kumuapisha IGP mpya Dodoma.

Mitazamo ya wachambuzi na wafuatiliaji wa masuala mbalimbali ya haki na usalama, wanaona ilikuwa muhimu kufanyika sasa kutokana na madoadoa na makandokando mengi yanayolikabili jeshi hilo kwenye utendaji wake.

'Kwa muda mrefu, Jeshi la Polisi linasifika vibaya, ilikuwa muhimu kuanza kuliangalia, ili watu walitazame vizuri, jeshi linapaswa kuwa kimbilio na sio kilio cha watu', anasema.

Utendaji, sifa za askari, upatikanaji wao, miundo mbinu na mifumo katika jeshi hilo unaakisi makandokando mengi yanayotokea sasa. Rais Samia anajua bado ana kazi kubwa ya kufanya kulisafisha.

Kwanini mabadiliko haya yanakosolewa?

Muda mfupi baada ya kutangazwa mabadiliko haya ya uongozi wa juu katika Jeshi la Polisi, mijadala mikubwa imeibuka mitandaoni, wako wanaoyaunga mkono mabadiliko hayo na wapo wanaoyakosoa.

Wanaoyakosoa wanaonesha kuwa hayataleta mabadiliko makubwa kwenye utendaji wa Jeshi hilo na namna linavyochukuliwa kutokana na makandokando yake. Huku wakiwataja baadhi ya watendaji wa jeshi hilo kuhusishwa na malalamiko kadhaa yakiwemo ya kubambikia watu kesi.  

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha Sheria na Haki za binadamu Tanzania, LHRC, Anna Henga ameiambia BBC kwamba anayaunga mkono mabadiliko hayo kutokana na udhaifu ulioko kwenye Jeshi hili kwa watendaji waliopita akitaja madawati la jinsia na mauaji kama doa kubwa.

‘Mie mabadiliko kimsingi nimeyafurahia kwa upande wa haki au mtizamo wa haki za binadamu’, alisema Henga akiona kwamba pengine yataleta utendaji tofauti.

Makandokando na madoa sugu katika Jeshi la Polisi

Moja ya jukumu kubwa la Polisi kwa mujibu wa sheria za Tanzania, ni kulinda watu na mali zao na kuhakikisha haki inatendeka na kusimamiwa.

Lakini doa kubwa katika Jeshi hilo katika miaka ya hivi karibuni ni kwa baadhi ya maafisa wake kuonekana kwenda kinyume na misingi na maadili ya Jeshi hilo pamoja na sheria zinazoliongeza katika utendaji wake. 

Miongoni mwa madoadoa haya ni:

1: Mauaji na mateso ya watu kwenye mikono ya Jeshi la Polisi

Kwa msingi wowote wa kuanzishwa kwake, Jeshi la Polisi linapaswa kuwa mahali salama kwa watu wanaoona kudhulumiwa haki zao. Lakini kwa Jeshi la Polisi Tanzania kuna mashaka kwenye hilo, hasa kutokana na uwepo wa baadhi ya maafisa wasio waadilifu.

Hivi karibuni Polisi saba mkoani Mtwara, Kusini mwa Tanzania walifikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamisi mkazi wa wilaya ya Nachingwea mkoa jirani wa Lindi.

Suala hili, Rais Samia analifahamu na alilisema katika moja ya ziara yake huko kanda ya Ziwa Victoria baada ya waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Hamad Yusuph Masauni kuligusia.

'Umezungumzia mauaji ya Mwanza, lakini kuna mauaji yametokea Mtwara na kwa taarifa zilizoko, ni jeshi lako ndilo lililofanya mauaji', alisema na kutangaza kuundwa kwa kamati ya kuchunguza mauaji hayo ambayo majibu yake, bado kitendawili, labda kwa kuwa suala lenyewe liko Mahakamani.

Pengine hapa palikuwa mwanzo wa mabadiliko ya sasa kwani Samia alitoa tamko: ”Nataka jeshi lako lijitafakari, waone kama kinachotokea ni msingi wa jeshi la Polisi au ni vinginevyo”.

Mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge na dereva teksi wa Manzese, Dar es Salaam, yaliyotokea Januari 14, 2006 hayawezi kusahaulika, yakimuhusisha Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (RCO) wakati huo, Abdallah Zombe.

Julai, 2016, Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa, ilimhukumu askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU), Pasificus Simon kifungo cha miaka 15 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten, Daud Mwangosi yaliyotokea Septemba 2, 2012 katika kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi alipokuwa akitekeleza majukumu yake ya kazi kwenye ufunguzi wa tawi la chama cha upinzani cha Chadema.

Haya ni machache tu. Malalamiko ni mengi ya watu kupoteza maisha ama kunyanyasika kwenye mikono ya Polisi, ingawa mara kadhaa polisi imekana kuhusika moja kwa moja na madhila hayo.

2: Kubambikiza Kesi na Uonevu

Kama kuna mahali kunatajwa sana kulichafua Jeshi la Polisi ni eneo hili la kubambikiza watu kesi. Kuna malalamiko mengi. Ukiacha kesi za kisiasa ambazo zimekuwa zikichukua nafasi kubwa, ziko kesi zingine nyingi ambazo zinatajwa kuwa sehemu ya ubambikaji huu.

Ucheleweshaji wa upelelezi, kukosekana au kupungua kwa uadilifu, nidhamu na maadili kwa baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi imekuwa kilio cha muda mrefu kwa wengi.

'Kesi nyingi zinakwama Mahakamani kwa sababu za kucheleweshwa kwa upelelezi au kwamba hazina ushahidi, na hizi ni zile tunazoita kesi za kubambikizwa.

Kwa mujibu wa Rais Samia hadi Agosti 22, 2021, idadi ya mahabusu katika jela za Tanzania ilikuwa karibu sawasawa na idadi ya wafungwa. Wafungwa walikuwa 16,542 na mahabusu walikuwa 15,194.

Mei 18, 2021 Rais Samia wakati akifungua Chuo cha ushonaji cha polisi Kurasini, Dar es Salaam, alilitaka jeshi hilo kufuta kesi zote za kubambikiza, ili kuondoa msongamano wa mahabusu gerezani.

 "Kwa sababu wengi wapo wanasubiri kuhukumiwa, kesi haiendi, ushahidi hakuna, mpelelezi anashindwa kupeleka kesi kwa sababu hakuna ushahidi, hivyo niombe sana, nilizungumza na Takukuru na wameweza kufuta kesi 147 ambazo waliwabambikia watu mbalimbali.

"Kwa hiyo nanyi Jeshi la Polisi jikagueni, kama kuna za aina hiyo nazo zifutwe ili kupunguza wingi wa mahabusu katika magereza zetu," alinukuliwa Rais Samia.

3: Rushwa

Hili ni Eneo lingine ambalo linanyooshewa kidole ndani ya polisi. Tafiti kadhaa ikiwemo iliyopewa jina la "Hawashikiki" uliofanywa na Shirika lisilo la kiserikali la Twaweza nchini Tanzania limetaja Idara za polisi kuwa miongoni mwa Idara za serikali zinazoongoza kwa rushwa.

Kutajwa kwa jeshi hilo hakuji bahati mbaya. Idara za jeshi hilo ziliwahi kutajwa kuongoza katika nchi za Afrika Mashariki kwa rushwa kupitia ripoti ya utafiti ya shirika lenye maslahi ya kimaendeleo barani Afrika ForDIA kwa kushirikiana na Jukwaa wazi nchini Tanzania, Trafo.

Ripoti ya utafiti huo ilisema idara za jeshi hilo zilipokea asilimia 25% ya rushwa zote zilizoripotiwa Tanzania. 

Nini matarajio ya wengi kwa mabadiliko haya?  

Mabadiliko yoyote katika jeshi la Polisi hayatakuwa na maana kama hayagusi haki za watu na mali zao zinazolindwa kwa mujibu wa sheria. Kulindwa kwa haki zao na usalama wao, kunawapa nafasi ya kufanya shughuli zao za maendeleo bila hofu na woga.

Wengi hawayaoni mabadiliko haya kama muarobaini wa kumaliza madoadoa na makandokando yanayolizunguka Jeshi la Polisi, ila ni mahala pazuri pa kuanzia kuelekea kuwa na Jeshi la Polisi thabiti na lenye ufanisi.

'Mabadiliko yalishafanyika mengi tangu enzi za marais wastaafu Jakaya Kikwete, Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi, lakini malalamiko ni yaleyale, anasema Raphael Kugesha, mtaalam wa masuala ya jamii na maendeleo.

Hata ukifuatilia mitandao ya kijami, mashaka ni yale yale kwa sababu watendaji ni wale wale na mifumo iliyopo ni ileile, hivyo matokeo ya ufanisi hayawezi kuonekana kwa ukubwa na yale yanayotarajiwa.

Hili linaleta maswali je mawili makubwa je Rais Samia analisafisha kwa maji au Sabuni Jeshi la Polisi? Je Rais anunue shati jipya au aendelee kusafisha madoa sugu kwenye Jeshi hilo?

Pengine maswali haya Rais ameyajibu kwa kuunda kwake kamati ya watu 12 chini ya Jaji mstaafu Mohamed Chande Othman. Kuundwa kwa Kamati hiyo ili kumshauri kuhusu namna ya kuboresha utendaji wa Jeshi hilo na majeshi mengine ni kilelelezo tosha cha kubaini kazi kubwa iliyopo kwenye kuliboresha jeshi hilo.

Wakati umefika wa kuwa na Jeshi linalotoa huduma? (Police Service)

Kugesha anapendekea uundwa kwa Jeshi jipya litakalofuata mfumo na muundo mpya wa utoaji huduma zaidi kwa njia ya kawaida kuliko matumizi mengi ya nguvu kama lilivyojengwa sasa.

“Hili litasaidia kupunguza kesi za mauaji, unyanyasaji, itaongeza kuaminika, na kujenga urafiki na mahusiano baina yake na wananachi, polisi hawatakuwa maadui wa watu, watakuwa marafiki wa watu na watasaidiwa kwenye utendaji wao na raia', alisema.

Pengine kamati mpya ya Jaji Chande aliyoiunda sasa Rais Samia ili kumshauri njia bora ya kuleta mabadiliko ya utendaji wenye matokeo bora kwenye vyombo vya haki jinai, wakianza na Jeshi la Polisi inaweza kuwaza sawa na Kugesha.

Ingawa msingi zaidi ni kulinda raia na mali zao, mabadiliko yoyote yanayofanyika sasa na yatakayokuja mbeleni yanapaswa kujenga ufanisi utakaolinda haki za watu na haki za nchi.

Rais ameanza kwa kufanya mabadiliko kwenye uongozi wa juu wa Jeshi hili, kwa mifumo iliyopo, watendaji, sheria na kanuni, kuna kazi kubwa ya kufanya ili lifikie malengo na matamanio anayoyataka, ambayo ni kuwa na Jeshi lenye ufanisi linalozingatia sheria, kanuni na kulinda na kujali haki za watu na mali zao.

Wakati huu ikisubiriwa ushauri wa Kamati ya watu 12 aliyoiunda Rais, IGP mpya, Wambura ana kazi kubwa ya kumsaidia Rais Samia kuondoa madoadoa na makandokando yaliyopo sasa, kabla ya kununuliwa kwa shati jipya kwa maana ya kuboreshwa kwake, ili kurejesha heshima ya jeshi hilo machoni kwa watanzania.