Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Matokeo ya uchaguzi wa urais kuhojiwa Mahakamani kunavyoweza kubadili siasa za Tanzania
Na Yusuph Mazimu
BBC Swahili
Uchaguzi nchini Kenya ni kama umekwisha sasa baada ya Mahakama ya upeo, ambayo ndiyo ya juu kabisa nchini humo, chini ya majaji saba kuthibitisha matokeo ya urais wa Agosti 9, 2022 yaliyompa ushindi naibu wa rais, William Ruto wa asilimia 50.49%.
Si mara ya kwanza kesi za kupinga matokeo ya urais Kenya kuwasilishwa Mahakamani. Mwaka 2017, Mahakama hiyo ya juu chini ya Jaji mkuu wa wakati huo David Maraga, ilitoa uamuzi wa kurejewa kwa uchaguzi baada ya kusikiliza kesi iliyowasilishwa na aliyekuwa mgombea wa muungano wa upinzani wa NASA, Raila Odinga.
Pamoja na mengi yanayotoa somo kwenye uchaguzi huo, suala la matokeo hayo kuhojiwa Mahakamani limeibua mijadala mingi nchini Tanzania.
Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, Mohammed Chande Othman, aliongoza jopo la majaji wengine wa Afrika kutoka katika Jukwaa la Majaji na Wanasheria Afrika kutazama mwenendo wa kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Kenya. Na yeye akihojiwa na moja ya magazeti ya nchini humo, ameungana na wale wanaotaka katiba ya Tanzania iruhusu matokeo ya urais kuhojiwa Mahakamani.
Katiba ya Kenya inaruhusu mtu yoyote kupinga matokeo ya urais Mahakamani, lakini katiba ya Tanzania ya Mwaka 1977 haitoi fursa hiyo. Hakuna Mahakama yoyote itakayoundwa kuchunguza uhalali wa kuchaguliwa kwa rais mara baada ya kutangwazwa na tume ya taifa ya uchaguzi (NEC).
Wanaotaka matokeo ya Urais Tanzania kuhojiwa Mahakamani wanahoja gani?
Ziko hoja nyingi zinazowasilishwa na wanaopigia chapuo matokeo ya urais Tanzania kuhojiwa mahakamani. Hoja nyingi kwenye vyombo vya habari na mitandaoni zinajiegemeza kwenye eneo la haki, utawala bora na ukuzaji wa demokrasia.
Jaji mkuu staafu wa Tanzania Chande katika hoja zake alinukuliwa akisema haoni sababu ya Tanzania kuhofia matokeo ya kura za urais kuhojiwa Mahakamani. Akisema ni suala la kukuza demokrasia, uwazi na utawala wa sheria. Na ni suala lenye mantiki kubwa.
Mmoja wa wachambuzi wa Tanzania, Raphael Kugesha, anasema hasara ya kutoruhusu matokeo kuhojiwa ni kuongeza mashaka ya uminyaji wa haki kama matokeo hayakuwa halali.
'ukiipata tume ya uchaguzi ambayo haina uadilifu, inaweza kuamua matokeo ya urais kwa niaba ya wananchi, na hilo ni nyundo ya mwisho kwa demokrasia'.
Si mara moja, wagombea urais wa upinzani na vyama vya upinzani nchini humo kulalamikia matokeo ya urais, lakini hakuna zaidi wanachoweza kufanya.
Tundu Lissu, mgombea wa urais katika uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2020 kupitia chama kikuu cha upinzani nchini humo, CHADEMA, alilalamikia matokeo na uchaguzi kwa ujumla, kwa hoja zinazoshabihiana.
'hatukubaliani na chochote kunachofanyika na matokeo yoyote, na tumesema mara nyingi sana katika kampeni hizi kwamba, hatutakubali chochote ambacho sio uchaguzi huru, wa haki na unaokubalika, kwa hiyo watanzania ambao haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka imeibiwa wanapaswa kuchukua hatua kutetea na kudai haki zao za kidemokrasia', alisema Tundu Lissu, mara baada ya matokeo ya urais kuanza kutangazwa.
Profesa Ibrahimu Lipumba, mwenyekiti wa chama cha upinzani cha CUF, alitangaza msimamo wa chama chake kutoshiriki uchaguzi wowote baada ya 2020, kwa sababu ya kasoro na udanganyifu wa matokeo.
'kuanzia sasa CUF kwa kushirikiana na wadau wengine kitajikita katika kuhamasisha watanzania kwa njia mbalimbali kupigania katiba mpya yenye misingi ya kidemokrasia na utawala bora', alisema Lipumba.
Hata hivyo tume ya uchaguzi nchini humo (NEC), ilikanusha madai yoyote ya udanganyifu kuhusu uchaguzi, ikisema ulikuwa huru, wa haki na ulifuata taratibu zote za kisheria.
Je ni wakati muafaka sasa kuifanyia kazi hoja hii?
Mchakato wa kupata katiba mpya Tanzania ulisimama miaka karibu 8 iliyopita baada ya kuanzishwa mwaka 2011 kwa kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Na. 83/2011 na baadaye ikatungwa Sheria nyingine ya Kura ya Maoni Na. 11/2013.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Waziri mkuu wa zamani, Jaji Joseph Sinde Warioba, ikaratibu mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa rasimu ya kwanza ya katiba ambayo kupitia uhariri wa Mabaraza ya Katiba ikapatikana Rasimu ya Pili ya Katiba.
Ikawasilishwa kwenye Bunge la Katiba na kupatikana kwa Katiba inayopendekezwa iliyopaswa kwenda kupigiwa kura. Hapo safari ya mchakato huo ilipokwamia mpaka leo.
Moja ya hoja ama maoni yaliyokuwepo kwenye rasimu ya katiba na katiba inayopendekezwa ni kuhusu matokeo ya rais kuhojiwa Mahakamani.
'kama maoni ya wananchi yangepitishwa wakati ule kwenye ule mchakato, na kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa ingefanyika naamini leo kungekuwa na mjadala tofauti, ingawa sasa hatujachelewa pia,' alisema Kugesha, mchambuzi.
Kwa hoja ya Kugesha, pengine ni wakati muafaka kwa sababu Rais Samia Suluhu ameunda Kikosi kazi cha kukusanya na kuchakata maoni ya wadau wa demokrasia na moja ya hoja iliyotawala maoni hayo ni pamoja na mabadiliko ya katiba kuruhusu tume huru ya uchaguzi, na hilo la matokeo ya urais kuhojiwa mahakamani.
'kwangu ni wakati muafaka, mabadiliko yoyote yatakayokubalika kabla ya uchaguzi mkuu ujao (2025), yakigusa tume huru, matokeo ya urais, na madaraka ya rais', hayataka kiu yote ya watanzania, lakini yatapunguza kelele', anasem Kugesha.
'Matokeo kupingwa Mahakamani si jambo geni' Afrika
'matokeo ya urais kupingwa mahakamani sio hoja ngeni wala haipaswi kuhofiwa na watanzania, ' anasema Jaji mstaafu wa Tanzania, Chande.
Nchi nyingi Afrika, kupitia katiba zao zimeruhusu matokeo ya urais kuhojiwa Mahakani. Ukiacha Kenya, kwa uchache kuna nchi kama Uganda, Malawi, Afrika Kusini na Zimbabwe ambazo matokeo ya uraisi yanaweza kupingwa Mahakamani.
Wengi walitarajia baada ya uamuzi wa mahakama ya Kenya kungezuka ghasia, lakini Kenya imekuwa tulivu na pande zote zimeheshimu uamuzi huo na kusonga mbele, licha ya wengine kutokubaliana nao.
Pengine hili ndilo limezidi kuibua wito kutoka kada mbalimbali nchini Tanzania kutaka na yenyewe kuruhusu kupitia mabadiliko ya Katiba, matokeo ya urais kupingwa Mahakamani.
Na wengi wanaamini siasa na demokrasia ya Tanzania zitabadilika kutokana na viwango vya uhuru, uwazi wenye kuthibitika na unaowajibika utakaoakisiwa na katiba na sheria. Lakini pia uhuru wa Mahakama kwenye kuendesha kesi kubwa za namna hii.
'watu watahofia kufanya udanganyifu kwenye matokeo kwa kuwa mwisho wa siku, itahitajika athibitishe mahakamani', alisema Kugesha, lakini hoja hapa je Mahakama itakuwa huru kuthibitisha kesi zitakazowasilishwa?