Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi ya kupata talaka: Sababu za kuombea talaka ni zipi?
"Shemeji zangu tu ndio wanaotazama TV ukumbini, hawaniruhusu kutazama kipindi ninachopenda." "Mume wangu haruhusu mbwa atoke nje, nywele zake zinapukutika ndani ya nyumba."
Je, unajua kwamba baadhi ya watu huomba talaka kwa sababu hizo? Baadhi ya wanasheria wanaofanya kazi katika mahakama za familia wamefichua mambo hayo.
Ndoa za leo zinabadilika kulingana na wakati. Ndivyo ilivyo talaka. Kulingana na Sheria ya Ndoa ya Kihindu-1955, mke au mume ana haki ya kubatilisha ndoa. Kifungu cha 13 cha Sheria hii pia kinataja sababu ambazo talaka inaweza kutolewa. Hebu tuone sababu hizo ni zipi.
Sababu za Talaka - India
Kutoka nje ya ndoa: Talaka inaweza kuombwa ikiwa mwana ndoa ana mahusiano mengine nje ya ndoa.
Ukatili: Talaka inaweza kuombwa kwa kuonyesha aina yoyote ya ukatili wa kiakili, kimwili au kingono.
Kutokuwepo kwa uhusiano: Talaka inaweza kutafutwa ikiwa hakuna uhusiano wowote wa mke na mume. Yaani wanaishi nyumba moja na hakuna kujaliana, hakuna mawasiliano ya kweli na kila mtu na hamsini zake.
Uwendawazimu: Talaka pia inaweza kupatikana kwa sababu ya kichaa cha mke au mume.
Kubadili Dini: Ikiwa mke au mume atabadili dini, talaka inaweza kupatikana kwa kutumia sababu hii.
Kuhamana: Ikiwa mmoja wa wanandoa atamuhama mwenzake, talaka inaweza kupatikana kwa sababu hii.
Kutoweka: Ikiwa mke au mume amepotea kwa miaka saba basi anahesabiwa amefariki. Kisha ombi la talaka linaweza kuwasilishwa kortini.
Ridhaa: Talaka pia inaweza kupatikana kwa ridhaa ya pande zote mbili. Pande zote mbili zinaweza kuachana kwa misingi ifuatayo. Mume na mke wanapotengana kwa zaidi ya mwaka mmoja. Inapotokea haiwezekani kwa mume na mke kuishi pamoja. Wakati wote wawili wanakubali kwamba hawawezi tena kuendelea katika uhusiano wa ndoa, wote wawili wanaweza kuwasilisha talaka pamoja.
Talaka huombwa wapi?
Ombi hili linapaswa kuwasilishwa katika Mahakama ya Familia ya eneo ambalo watu wanaishi. Maombi yanaweza pia kufanywa katika eneo ambalo ndoa ilifanyika. Au maombi haya yanaweza kufanywa katika mahakama ya eneo ambalo mke anaishi.
Kesi za talaka huanza wakati wahusika wanaotaka talaka wanapoomba au wakati wanandoa wanapotuma taarifa kwa kila mmoja. Ikiwa upande mwingine hauko tayari kwa talaka basi mchakato huo unaitwa 'Talaka Inayoshindaniwa.'
Hatua ya kwanza: Wanandoa wanaotafuta talaka wanapaswa kwanza kutuma maombi katika mahakama ya familia inayohusika. Pande zote mbili zinapaswa kusaini ombi hili.
Hatua ya Pili: Baada ya kuwasilisha ombi la talaka, pande zote mbili lazima zionekane katika mahakama ya familia. Wote wawili wanapaswa kuleta mawakili wao. Kisha mahakama itazingatia maombi ya pande zote mbili. Mahakama pia itajaribu kupatanisha pande hizo mbili. Ikishindikana kesi itaendelea.
Hatua ya tatu: Baada ya kuchunguza maombi ya pande zote mbili, hoja zao zitaandikwa mahakamani.
Hatua ya nne: Baada ya hatua ya tatu, mume na mke hupewa miezi sita. Katika kipindi hiki wanandoa hupewa nafasi ya kuishi pamoja. Baada ya hapo, maombi ya pili yanapaswa kufanywa.
Hatua ya Tano: Baada ya ombi la pili kuidhinishwa, usikilizaji wa mwisho unafanywa. Kwa mara nyingine tena taarifa zao zitarikodiwa mbele ya mahakama.
Hata hivyo, muda wa miezi sita umefutwa na Mahakama ya Juu katika baadhi ya kesi. Iwapo kuna makubaliano kati ya wawili hao kuhusu masuala ya masurufu na malezi ya watoto, kipindi cha miezi sita kitaghairishwa.
Kulingana na Sheria ya Ndoa ya Kihindu, talaka hairuhusiwi ndani ya mwaka wa kwanza baada ya ndoa. Wote wawili wanapewa nafasi ya kuishi baada ya ndoa. Hata hivyo, mambo mengine yanazingatiwa ikiwa matatizo ni makubwa zaidi au hali si nzuri.
Talaka ni rahisi?
Ingawa sheria zinataja baadhi ya sababu za talaka, watu wengi hufika mahakamani kutaka talaka kwa sababu tofauti sana.
Ketaki Jalatare, wakili anayefanya kazi katika mahakama ya familia huko Nagpur, Maharashtra, alisema, "kwa mabadiliko ya hali ya kijamii, sababu za talaka pia zinabadilika. Hapo zamani kulikuwa na kujaribu kubaki kwenye ndoa, sio hivyo sasa. Talaka ni nyingi.''
Malavika Rajkotia pia anafanya kazi kama wakili wa mahakama ya familia, anasema, "wasichana wanaishi kwa kujitegemea leo hii. Kwa hiyo wanafanya maamuzi yao wenyewe. Mtazamo wao kuhusu mfumo wa familia pia unabadilika. Ila wanaume wengi bado wanafuata mila za zamani."
Ketaki na Malavika walieleza kuwa idadi ya kesi za talaka zimeongezeka sana hasa wakati wa virusi vya Corona.
“Kukaa nyumbani kumewalazimu watu wengi kuondoka mijini na kwenda vijijini kwa wazazi wao. Miji mikubwa ilikuwa ni vigumu sana kwao kuishi, matokeo yake watu wengi waliomba maombi ya talaka," anaeleza Malvika.
Je, Talaka ni Rahisi? Talaka si rahisi. Kuna mambo mengi ya kisaikolojia na kijamii yanayohusiana nayo. Malvika anasema ikiwa wanandoa wana watoto, hali inakuwa ngumu zaidi.
Kwa hiyo talaka isionekane kuwa ni kipande cha karatasi tu. Inahusiana na mambo mengi kama vile masurufu na huduma ya watoto. Malvika anasema athari za talaka kwa watoto ni tatizo kubwa la kijamii.