Mapigano Sudan: Kikosi maalumu kiliwaokoa wanadiplomasia wa Marekani kutoka Sudan

Iliyochapishwa

Jeshi la Marekani limewaokoa wanadiplomasia wa Marekani na familia zao kutoka Khartoum , Rais Joe Biden amesema.

"Leo , kwa agizo langu , jeshi la Marekani limefanya operesheni ya kuwaondoa wafanyakazi wa serikali ya Marekani mjini Khartoum," alisema katika taarifa yake.

Mapema Kikosi cha kijeshi cha Sudan Rapid Support Forces (RSF) kilisema kuwa ndege sita za kijeshi zilitumiwa Jumapili katika operesheni ya mapema asubuhi, na kwamba kiliratibu uokoaji huo pamoja na Marekani.

Taarifa kadhaa bado hazijawa wazi.

Idadi ya wangapi hasa waliookolewa kwa ndege nje ya Sudan bado haijathibitishwa. Hatahivyo kabla ya operesheni ya Jumamosi, Kituo cha habari cha CBS News, ambacho ni mshirika wa BBC nchini Marekani, kiliripoti mpango wa kuwaokoa wafanyakazi wapatao 70 wa serikali.

Bw Biden, alithibitisha kuwa ubalozi wa Khartoum sasa umefungwa : "Tunaahirisha kwa muda shughuli katika ubalozi wa Marekani nchini Sudan."

Pia alizishukuru nchi za Djibouti, Ethiopia na Saudi Arabia, akisema ‘’wamekuwas muhimu katika mafanikio ya operesheni yetu ".

Rais huyo wa Marekani alisihfu ‘ujasiri na ujuzi ‘’ wa wafanyakazi wa wa ubalozi na "ujuzi wa hali yajuu wa wanajeshi wetu ambao walifanikiwa kuwatoa nje salama".

Hii ni mara ya pili kwa shughuli ya uokoaji wa raia wa kigeni tangu ziibuke ghasia katika mji mkuu wa Sudan Khartoum.

Jumamosi, zaidi ya raia 150, wanadiplomasia, na maafisa wa kimataifa waliokolewa kwa kutumia bahari kwenye bandari ya Saudi Arabia ya Jeddah. Wengi wao walikuwa ni rai awa nchi za Ghuba, pamoja na Misri, Pakistan na Canada

Biden atoa wito wa usitishaji mapigano

Idhaa ya taarifa za Kiarabu Al Hadath iliryipoti kuwa ndege sita za Marekani zilitua kwenye uwanja wa ubalozi , na watumiaji kadhaa wa Twitter walituma taarifa kuwa walisikia sauti za helikopta juu ya ubalozi wa Marekani, hatahivyo BBC haikuweza kuthibitisha hili.

Uwanja wa ndege wa Khartoum umekuwa ukilengwa mara kwa mara na makombora pamoja na risasi, na hivyo kuifanya shughuli ya uokoaji kwa njia ya ndege kuwa kutowezekana.

Afisa wa Marekani ambaye jina lake halikutajwa ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba Rais Biden alikuwa ameagiza uokoaji Jumamosi baada ya kupokea taarifa kutoka kwa timu yake ya usalama wa taifa, ambao waliona kuwa hakutakuwa mwisho wa vita.

Taarifa ya Bw Biden ilisema "Ninapokea ripoti za mara kwa mara kutoka kwa timu yangu kuhusu kazi inayoendelea kuwasaidia."

"Tunafanya kazi kwa karibu na washirika wetu katika juhudi hizi."

Alilaani "ukatili mbaya " nchini Sudan, akisema "ni wa ukosefu wa ufahamu na unapaswa kusitishwa".

"Pande zinazohasimiana zinapaswa kutekeleza usitishaji mapigano usio na masharti , ili kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia watu, na kuheshimu utashi wa watu wa Sudan."

Uingereza inasema kuwa inaangalia uwezekano wa kuwaondosha wafanyakazi wake nchini Sudan.

Nambari ya simu imewekwa kwa wale wanaohitaji usaidizi wa haraka, na rai awa Uingereza waliopo nchini Sudan wanatolewa wito kuiambia wizara ya mambo yan je ni wapi walipo.

Uokoaji wowote wa Uingereza unatarajiwa kuwa wa kiwango kidogo sana na utawalenga zaidi wafanyakazi wa kibalozi - sio sawa na uokoaji wa watu wengi uliofanyika nchini Afghanstan mwaka 2021.

Wakati huo huo serikali ya Canada imewaambia raia wake walioko nchini Sudan ‘’wajifiche katika maeneo salama’’

Ikielezea hali ya usalama kama "ya ghasia ya kiwango cha juu", iliwaambia raia wake kuchaji simu zao wakati wote, kufunga milango na madirisha wakati wote na "kuangalia uwezekano wa kuondoka nchini humo iwapo kutakuwa na njia salama za kufanya hivyo".

Mapigano makali yaliibuka mjini Khartoum tarehe 15 Aprili, huku vikosi vinavyomtiii mkuu wa majeshi ya Sudan Abdel Fatteh al-Burhan vikipigania mamlaka ya nchi na mahasimu wao wa kijeshi wa kundi la Rapid Support Forces (RSF).

Kumekuwa na ufyatuaji wa risasi na ulipuaji wa makombora unaoendelea katika mji mkuu Khartoum na maeneo mengine ya nchi.

Usitisha kadhaa wa mapigano ambao umekuwa ukionekana kukubaliwa na pande zote ulipuuzwa, mkiwemo usitishaji mapigano wa siku tatu kwa ajili ya maadhinisho ya sherehe za Eid al-Fitr.

Raia wa Uingereza wamekwama na kuchanganyikiwa

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak aliongoza kikao cha dharura Jumamosi ili kutathmini mzozo wa Sudan ana mazungumzo zaidi yanatarajiwa kufanyika Jumapili.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza James Cleverly amekatiza ziara yake ya hort Pacific na kurejea mjini London.

Baadhi ya raia wa Uingereza waliokwama nchini Sudan wameelezea kuwa na wasi wasi na kusikitika kutokana na ukosefu wa ndege za kuwaokoa.

Imam Muingereza Iman Abu Garga, anayeitembelea Khartoum, alisema kuwa alikuwa amejisajiri yeye na watoto wake wawili, kama alivyoagizwa , " na tangu wakati huo hakuna kilichofanyika".

"Hatujui ni muda gani au kipindi gani. Hatujui hali itakuaje. Je tutaondolewa kwa ndege kutoka uwanja wa ndege wa Khartoum ? Je tutalazimika kwenda kwa barabara? Inakanganya tu kwamba hakuna mawasiliano na mtu yoyote," alilalamika.

Raia mwingine wa Uingereza aliyeko Khartoum aliiambia BBC kwamba alihisi "kutelekezwa kabisa " na serikali ya Uingereza, akisema kuwa hajapewa ‘’taarifa za kutosha kabisa’’ kuhusu mipango wa uokoaji.

Jumamosi, taarifa ya jeshi la Sudan ilisema kuwa Gen Burhan alikubali kuwezesha na kulinda uokoaji wa rai awa kigeni ‘’katika saa zijazo.’’

Ilisema kuwa waingereza, Wamarekani, Wafaransa na Wachina na Wanadiploamasia wataondolewa kwa ndegeza kijeshi kutoka Khartoum.

Serikali ya Uingereza ilisema kuwa "inafanya kila liwezekanalo kuwasaidia rai awa Uingereza na wafanyakazi wa kidiplomasia mjini Khartoum’’.

Waziri wa ulinzi wa Uhispania alisema kuwa ndege sita zilitumwa Djibouti kama sehemu ya juhudi za nchi hiyo za kuwaokoa raia Wahispania na wengine.

Shirika la Afya Duniani linasema kuwa zaidi ya watu 400 wameuawa. Idadi ya vifo inaweza kuwa ya juu zaidi kwwasababu watu wengi wanapata ugumu wa kufika hospitali.

Maelfu ya watu, wengi wao wakiwa ni raia wamejeruhiwa, huku vituo vya matibabu vikikabiliwa na shinikizo la kushughulikia idadi kubwa ya wagonjwa wanoingia.

Kando na Khartoum, jimbo la Magharibi mwa nchi la Darful, ambako kundi la RSF liliibuka kwa mara ya kwanzac, limeathiriwa vibaya na mapigano.

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa watu hadi 20,000 – wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto – wamekimbilia Chad kutafuta usalama, wakitokea Darfur.