Mafuriko Pakistan: 'Maji yamekuja na sasa kila kitu kimetoweka'

Mvua kubwa na zisizo na kikomo nchini Pakistan zimeharibu nyumba na mali, na kuathiri makumi ya mamilioni na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000.
Waandishi wawili wa BBC, walioko kaskazini na kusini mwa nchi wanaelezea uharibifu wanaouona.
Nowshera, Pakistan Kaskazini
Katika mitaa iliyokumbwa na mafuriko kwenye vitongoji vya mji wa kaskazini wa Nowshera, wakaazi wanaanza kujaribu na kurejea majumbani mwao kukagua uharibifu na kuona ni nini wanaweza kuokoa.
Wengine walitumia mabomba y mipira ili kusaidia kuelea kando ya maji ya rangi ya udongo yenye matope, ambayo nyakati fulani yalifika hadi kwenye vifua vyao, na wengine walipitia humo kwa bidii.

Imadullah, mpishi, akiwa na mwanawe mdogo juu ya mabega yake, alikuwa amefanikiwa kufika nyumbani kwake. Vitu vyao vyote vilirundikana, vikiwa vimefunikwa na matope na kwa kiasi kikubwa havifai kutumika tena
"Hatuna chochote kilichosalia," aliambia BBC, "Hatukuweza kuokoa chochote, maisha ya watoto wetu tu."
Zaidi chini ya barabara iliyojaa maji, wanawake wawili walishikana kwa msaada walipokuwa wakijaribu kusonga mbele hadi nyumbani kwao. Lakini maji yalikuwa ya mengi sana.
"Hatujui ikiwa bado imesimama au imeanguka," alisema mmoja, "sijui tutaijengaje tena. Tunaishi kambini shuleni. Mungu ni shahidi yangu, hatuna hata pesa."
Mamia ya maelfu ya nyumba zimeharibiwa kabisa au kuharibiwa kiasi na kuwaacha mamilioni bila makazi.
Maafisa wa Pakistani wanakadiria karibu uharibifu wa thamani ya $10bn umefanywa, na kuibua wasiwasi juu ya uhaba wa chakula na mazao kufutwa.

Wengi sasa wanaishi katika kambi za misaada. Sio mbali na Nowshera, mamia ya wengine wameweka mahema kando ya barabara, sehemu ambapo wanaweza kuona kwa macho nyumba zao, wakiwa na tumaini kuwa na uwezo wa kurudi mara tu maji yanapopungua zaidi.
"Inauma sana siwezi kuieleza kwa maneno," Rozina anasema, huku watoto wake saba wakizunguka kando yake.

Mvua kubwa za masika ni jambo la kila mwaka, lakini si kwa kiwango hiki. Sehemu za Pakistan zimeshuhudia kiasi kikubwa cha mvua zaidi kuliko katika mwaka wa kawaida.
Mvua ya majira ya kiangazi ndiyo kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa katika muongo mmoja na mawaziri wa serikali wanasema nchi hiyo inalipa gharama ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani, licha ya kuchangia sehemu ndogo tu ya hewa chafu duniani.
Akizungumza na BBC katika kikao kilichoandaliwa kwa ajili ya waandishi wa habari wa kigeni, Waziri Mkuu Shehbaz Sharif alipuuzia ukosoaji kwamba maafisa walikuwa wamechelewa kufanya lolote mafuriko hayo yalipoanza mwanzoni mwa msimu wa joto.
"Kwa hakika tunajifunza kutokana na tuliyopitia," alisema, "lakini jumuiya ya kimataifa inapaswa kusimama nasi leo, ni pengo kubwa kati ya mahitaji yetu na kile tunachopokea hadi wakati huu."

Saeeabad, Pakistan Kusini
Mvua imesimama katika sehemu za Pakistani lakini uharibifu haujaacha . Mafuriko makubwa kaskazini mwa nchi yanasafiri kuelekea maeneo ya kusini mwa nchi ambapo maeneo makubwa ya ardhi tayari hayawezi kukaliwa.
Mamia ya maelfu ya nyumba zimeharibiwa na mamilioni ya watu wamefanywa kuwa maskini.
Huko Saeedabad, katika mkoa wa Sindh nchini Pakistan, mamia ya watu wanaishi kando ya barabara ya changarawe ambapo barabara imejaa maji
Kwa mbali unaweza kuona nyumba zao, baadhi ya nyumba maji yamejaa hadi kufikia juu usawa wa dirisha.

Nilikutana na Banul kwenye hema na watoto 15 wengine wake, wengine wapwa na binamu zake. Anafurahi kuwa wote wako hai lakini sasa ana wasiwasi kwamba watalisha watoto nini.
"Tumekuwa tukiishi hapa kwa wiki, hakuna nyumba, hema moja tu kwa ajili yetu sote. Tunahitaji msaada. Tunaweza kuokoa maisha yetu tu ," anasema Banul.
"Nyumbani tulikuwa wakulima. Tulikuwa na pamba, tulikuwa na mahindi. Kila kitu kilikuwa tayari maji yamekuja na sasa kila kitu kimetoweka. Hatuna chochote na hatuna chakula."

Katika barabara hii chafu hadi mbele, watu wanaweza kukaa kwa siku kadhaa bila kula wakati mwingine. Lori la chakula linapokuja, chakula huisha haraka na sio kila mtu anapata.
Wafanyakazi wa ndani wamezidiwa na kusema hawana rasilimali za kutosha. Juhudi za kutoa misaada zimekuwa hazitabiriki, haswa katika jamii za mbali ambako barabara zisizo na lami zimemezwa na maji.
Mojawapo ya changamoto kubwa zaidi ambazo wafanyakazi wa misaada watakabiliana nazo wakati au kama misaada ya kimataifa itakapowasili, itakuwa jinsi ya kuifikisha kwa kila mtu anayeihitaji huku barabara hazipitiki na maelfu ya watu bado wamenasa kwenye maji.
Lakini kwa watu hao, misaada ndiyo tumaini lao la mwisho la kunusurika katika janga lililowakumba na kuharibu vitu vyao vingi.















