Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Siku 100 tangu Hamas kushambulia Israel, na kusababisha vita Gaza
Na Wyre Davies
Mwandishi wa BBC Mashariki ya Kati
Siku mia moja zilizopita, jambo lisilofikirika hapo awali lilitokea katika Israeli. Taifa , lililozaliwa kutokana na shida na vita miaka 75 tu iliyopita, liliamka kwa kile ambacho wengine wamekielezea kuwa tishio kwa uwepo wake.
Jumamosi usiku, huko Tel Aviv, matukio ya Oktoba 7 yaliadhimishwa na maelfu ya watu. Walio juu zaidi fikrani mwa kila mtu walikuwa mateka wapatao 130 waliotekwa nyara na Hamas na ambao bado wanazuiliwa huko Gaza, ingawa baadhi yao huenda bado hawako hai.
Baada ya mapambazuko siku 100 zilizopita, maelfu ya wapiganaji wa Hamas waliokuwa na silaha nzito walivamia na kuvuka uzio wa mpaka wa Gaza katika maeneo kadhaa tofauti.
Walishambulia kibbutzim, vituo vya kijeshi na miji ya mpakani, iliyozoea mashambulizi ya roketi kutoka Gaza lakini wakizidiwa na ukubwa wa uvamizi wa Hamas.
Takriban watu 1,200 waliuawa kwenye mpaka huku ulinzi wa Israel ukishikwa na mshangao.
Picha za mamia ya wapenzi wa muziki wachanga waliokimbia kuokoa maisha yao kwenye tamasha la Nova zilitikisa Israeli hadi mwisho. Zaidi ya watu 360 waliuawa katika eneo la tamasha na makumi ya wengine kutekwa nyara hadi Gaza.
Miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo kubwa ya ukumbusho mjini Tel Aviv ni familia za waliotoweka, wakiwa wamebeba mabango na kuvaa fulana zenye sura za wapendwa wao.
Nilizungumza na Yossi Schneider - binamu wa Shiri Bibas, ambaye alitekwa nyara pamoja na watoto wake wawili wadogo na mume wake.
"Kuna watu 130, hasa raia wanaoshikiliwa bila dawa na Shirika la Msalaba Mwekundu haliruhusiwi hata kuwatembelea," anasema Yossi, ambaye alikasirishwa na kwamba familia kubwa imepata taarifa kidogo juu ya ustawi wao wa kimwili au kiakili.
"Kuna vizazi vitatu vya familia yangu ambavyo vimetoweka. Vizazi vitatu vya familia yangu! Na dunia inanyamaza na kutuomba tutulie. Siwezi kuvumilia tena," anaongeza, akiwa amechoka lakini amechanganyikiwa waziwazi.
Watu wengi hapa wangesema kwamba tarehe 7 Oktoba ilikuwa tishio kubwa kuwahi kuikabili Israeli na kwamba Waisraeli hawajawahi kuhisi hatari sana. Wakati kurejea salama kwa mateka ni kipaumbele chao kabisa, wengi pia wanakubaliana na malengo ya vita ya serikali yao huko Gaza na sauti chache zinatoa wito wa kuvumiliana na kuishi pamoja.
Wakati jeshi la Israel lililotetereka la ulinzi hatimaye lilijibu kile kilichokuwa kikitokea kusini kama Jumamosi tarehe 7 Oktoba inakaribia mwisho, jeshi la Israel lilianza kampeni ya mashambulizi ya mabomu ambayo haijawahi kushuhudiwa huko Gaza - lengo lake lililoelezwa: uharibifu kamili wa Hamas na mfumo wake wa msaada.
Sehemu kubwa ya eneo hilo, kuanzia mji wa Gaza kaskazini hadi Khan Younis kusini, imeharibiwa tangu wakati huo.
Israel inasema Hamas imedhoofishwa sana na, kwa mujibu wa jeshi la Israel, imekuwa kundi lisililoweza tena kufanya shughuli za kutishia Israel kaskazini mwa Gaza.
Lakini idadi ya raia waliouawa katika shambulio la bomu la Israel imekuwa kubwa. Zaidi ya 23,000 wameuawa, kulingana na Wizara ya Afya inayosimamiwa na Hamas, wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Maelfu zaidi wanaaminika kufariki chini ya vifusi.
Maafisa wa Palestina wanasema kuwa asilimia 85 ya wakazi wa Gaza wameyakimbia makazi yao. Wakati misaada zaidi sasa ikiingia Gaza mkuu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa ameelezea hali hiyo kuwa "isiyovumilika".
Faten Abu Shahada anahitaji kusafishwa kwa figo mara kwa mara ambayo ni sababu moja kwa nini yeye na familia yake wamelazimika kuhamia kusini. Nyumbani kwa Faten na watoto sasa ni hema la plastiki huko Khan Younis - sauti ya ndege isiyo na rubani ya Israeli ikiruka juu ya mwenzao wa kudumu.
"Gaza imeharibiwa. Hakuna Gaza iliyobaki - hakuna hospitali, hakuna elimu," anasema Faten. "Watoto wetu wamepoteza mwaka wao wa shule, Gaza haipo tena."
Israel inakabiliwa na shinikizo kubwa la kimataifa kufikiria kusitisha mapigano huko Gaza, hivyo ndivyo ukubwa wa mateso ya raia.
Hata mshirika wake wa karibu Marekani, ambayo mara kwa mara inatetea haki ya Israel ya kujilinda na kuzuia marudio ya Oktoba 7, imemwambia mara kwa mara Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kwamba idadi ya vifo vya raia ni "kubwa mno".
Rais Biden amezungumzia "mashambulizi ya kiholela" ya Israel, ambayo alisema yanamaanisha kuwa nchi hiyo inapoteza uungwaji mkono kote duniani.
Gideon Levy ni mwandishi wa gazeti la Israel la Haaretz na mkosoaji wa mara kwa mara wa Bw Netanyahu. Nilimuuliza ikiwa vita hivi - ambavyo tayari ni vya muda mrefu zaidi kwa Israeli tangu 1948 - vitafikia tamati hivi karibuni.
"Vita katika sura yake ya sasa vitadumu kwa muda mrefu kama Waamerika watairuhusu Israel (ifanye)," anasema Levy.
Anaongeza: "Sidhani kuwa kutakuwa na wiki nyingi zaidi. Lakini hiyo haimaanishi kwamba vita vimekwisha kwa sababu hakuna aliyefikiria kuhusu siku inayofuata.
"Ikiwa Israel haitaondoka Gaza, kutakuwa na upinzani. Na kama kutakuwa na upinzani kutakuwa na kulipiza kisasi."
Huku wanajeshi wa Israel wakiendelea kushambulia maeneo ya Hamas katikati na kusini mwa Gaza, kukomesha vita kunaonekana kuwa mbali na nia ya Bw Netanyahu.
Israel inasema mapigano hayataisha hadi Hamas washindwe kabisa. Mustakabali wa hivi karibuni katika eneo lote, na haswa kwa maelfu ya raia wanaoishi katika hali mbaya huko Gaza, unaonekana kuwa mbaya sana.
Imetafsirirwa na Yusuf Jumah