Tetesi za soka Ulaya Jumapili: Isak anaweza kuigharimu Liverpool £120m

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 3

Liverpool huenda ikalazimika kulipa pauni milioni 120 au zaidi ili kumsajili mshambuliaji wa Uswidi Alexander Isak, 25, kutoka Newcastle United - na kukabiliana na ushindani kutoka kwa Chelsea na Arsenal . (Give Me Sport)

Tottenham , Liverpool , Manchester City na Chelsea wamejiunga na orodha ya vilabu vikubwa barani Ulaya vinavyomuwinda mshambuliaji wa Monaco mwenye umri wa miaka 21 Lamine Camara. (TBR Football)

Arsenal na Chelsea pia wamehusishwa na uwezekano wa kutaka kumnunua mshambuliaji wa RB Leipzig na Slovenia Benjamin Sesko, huku mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 akitazamiwa kusalia katika klabu hiyo inayoshika nafasi ya nne katika ligi ya Ujerumani Bundesliga iwapo watashindwa kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa msimu ujao. (Mirror)

Chelsea na Liverpool , wakati huohuo, wanaweza kupigana vita kumpata beki wa kati wa RB Leipzig wa Ufaransa, Castello Lukeba, ingawa Real Madrid pia ni miongoni mwa orodha ndefu ya timu zinazomtaka mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22. (Mirror)

Mkuu wa Bayern Munich Karl-Heinz Rummenigge anasema viongozi wa Bundesliga wanataka kushindania kumsajili mshambuliaji wa Bayer Leverkusen wa Ujerumani Florian Wirtz, 21, ambaye anahusishwa na kuhamia Manchester City majira ya kiangazi.. (AZ via Mail)

Arsenal wanaweza kuachwa na uchungu wa kumuuza mshambuliaji Mika Biereth, 22, kwa Sturm Graz kwa £4m msimu wa kiangazi- mchezaji huyo wa kimataifa wa vijana wadogo wa Denmark alifunga mabao 11 katika michezo 16 kwa timu hiyo ya Austria Bundesliga kabla ya kufungia Monaco mabao 10 katika mechi saba za ligi baada ya kuhamia kwa £10.7m Januari. (Mirror)

Barcelona wanamfuatilia kwa karibu winga wa Manchester United Alejandro Garnacho, 20, kwa nia ya kukamilisha uhamisho wa mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina msimu wa joto. (Fichajes - in Spanish)

Liverpool inamfuatilia kwa karibu Carlos Baleba wa Brighton kabla ya uwezekano wa kumnunua kiungo huyo wa kati mwenye umri wa miaka 21 kutoka Cameroon. (Football Insider)

Real Betis wanatafuta mkataba wa muda mrefu zaidi kwa winga wa Brazil Antony ambaye anacheza kwa mkopo lakini kuna uwezekano wa kushindwa kumudu mishahara au ada ya mchezaji huyo wa Manchester United , ambayo inatarajiwa kuwa £41m. (Fichajes - in Spanish)

Aston Villa wanatumai kukamilisha mipango miwili ya kumnunua "mshambuliaji kamili" Charalampos Kostoulas, mwenye umri wa miaka 17, na mchezaji mwenzake wa Ugiriki na Olympiakos Christos Mouzakitis, mwenye umri wa miaka 18. (TBR Football via Give Me Sport)

Mchezaji mpya anayetarajiwa kusajiliwa na Chelsea - ambaye jina lake kamili ni Denner Alves Evangelista Pereira lakini anajulikana kama Denner - ni binamu wa beki wa Arsenal wa Brazil Gabriel Magalhaes. (Metro)

Chelsea wanajiandaa kukamilisha mkataba wa thamani ya £12.4m pamoja na nyongeza za mlinzi wa Corinthians, raia wa Brazil, Denner Evangelista mwenye umri wa miaka 17, ambaye atajiunga na klabu hiyo ya magharibi mwa London mwaka wa 2026. (Fabrizio Romano)

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi