Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Sungusungu wanaopambana na uhalifu kwa kutumia filimbi na mijeledi
- Author, Ayanda Charlie & Tamasin Ford
- Nafasi, BBC
- Iliyochapishwa
Wasiwasi kuhusu uhalifu wa kutumia nguvu utakuwepo katika vichwa vya Waafrika Kusini wanapopiga kura baadaye mwezi huu, licha ya wanasiasa kutoa ahadi za kila aina kuhusu kuukabili.
Kwa sasa viwango vya mauaji viko juu katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, BBC Africa Eye imeambatana na sungusungu walio mstari wa mbele katika kupambana na uhalifu.
Kelele za filimbi zinasikika huku watu waliovalia fulana za rangi ya njano na chungwa wakianza kukimbia.
“Ee Mungu,” mtu anapiga yowe huku polisi akiwa ameanguka chini. Amepigwa risasi.
Ni Ijumaa usiku huko Diepsloot, kitongoji kilicho nje kidogo ya Johannesburg - jiji ambalo ni kitovu cha biashara Afrika Kusini.
"Hili ni jambo la kawaida," anasema Abel Rapelego. Mwanaume mwenye umri wa miaka 41 anaeongoza timu ya watu wali jitolea ambao wanashika doria mitaani kila usiku baada ya giza kuingia.
Ving'ora kutoka gari la polisi vinatawanya umati wa watu waliokuwa wamekusanyika.
Afisa huyo wa polisi, Tom Mashele mwenye umri wa miaka 38, alipelekwa hospitali lakini alifariki dunia wiki chache baadaye. Hakuna mtu aliyekamatwa kwa mauaji yake, yaliyotokea wakati akiwa nje ya kazi.
Takwimu za Afrika Kusini
Afrika Kusini ina moja ya viwango vya juu zaidi vya mauaji duniani, kulingana na takwimu kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Madawa ya Kulevya na Uhalifu. Kulikuwa na mauaji zaidi ya 27,000 mwaka jana; ambayo ni sawa na watu 45 kwa kila watu 100,000.
Kutokana na hali hiyo, Rapelego anasema njia pekee ya kuweka familia zao salama ni watu kujitolea kushika doria katika jamii, hata ikimaanisha kuhatarisha maisha yao kwani “Diepsloot iko mikononi mwa wahalifu.”
Timu za sungusungu hufanya kazi kwa kushirikiana na polisi wa manispaa.
Ni mpango wa ulinzi usio rasmi, kwani baadhi ya mambo wanayofanya hayajaidhinishwa kisheria. Hakuna anayelipwa na hawabebi bunduki. Lakini wana sjambok, mjeledi wa jadi wa ngozi.
"Tunasimamisha na kupekua na ikiwa wewe ni mhalifu na hutatii amri zetu, sjambok itatumika dhidi yako," anasema Rapelego.
Watu hao hawana mamlaka ya kisheria ya kufanya shughuli za kusimamisha watu na kuwapekuwa, hata hivyo timu hiyo inapita mtaa kwa mtaa kuhoji mtu yeyote ambaye anatembea usiku.
Wakati wakipita karibu na duka, mmiliki anasema ameibiwa muda mfupi uliopita. Timu hiyo inafanikiwa kumkamata mtu anayeonekana akikimbia na kumpekuwa kutafuta simu na pesa zilizoibiwa.
Wanamchapa kwa sjambok, ambayo yenyewe inaonekana kama uhalifu. Hakuna ushahidi kwamba amefanya kosa lolote, hivyo wakamuacha aende zake.
Akihojiwa kuhusu haki gani waliyonayo kufanya wanayo yafanya, Rapelego anatetea matumizi ya nguvu akisema: “Kumbuka, Diepsloot ni nyumbani kwetu na tusiporekebisha Diepsloot yetu, hakuna mtu atakayeirekebisha Diepsloot hii.”
Sungusungu pia wako hatarini
Takwimu za uhalifu nchini Afrika Kusini zinaonyesha waathiriwa wakubwa wa mauaji ni vijana weusi, na sungusungu pia wanajiweka hatarini.
Miaka miwili iliyopita, Alpha Rikhotso mwenye umri wa miaka 21 alipigwa risasi na kuuawa akiwa nje wakati wa doria.
"Alikuwa akijaribu kuyalinda maisha yake, maisha yangu na ya kila mtu. Alikuwa anapambana na uhalifu," anasema babake, David Rikhotso.
Mwanawe alikuwa wa kwanza kufika kwenye eneo la tukio wakati sungusungu walipopuliza filimbi kuhusu uhalifu unaoendelea. Alifanikiwa kumkamata mhalifu, lakini alipigwa risasi mkononi.
Hakupona jeraha hilo. Kama vile polisi, hakuna mtu aliyewahi kukamatwa kwa mauaji hayo.
“Kila siku watu wanaibiwa. Watu wanakufa kila siku. Ninaomba mchana na usiku sungusungu wawe salama. Hakuna sheria mahali hapa,” Rikhotso aliambia BBC Africa Eye.
Wazungu wa Afrika Kusini
Benki ya Dunia inakadiria uhalifu huitia hasara Afrika Kusini karibu dola za Kimarekani bilioni 40 - kila mwaka ambayo ni sawa na 10% ya Pato la Taifa kila.
Kilomita sitini (maili 37) kaskazini-magharibi mwa Diepsloot, kikundi kingine cha sungusungu kinaanza doria huko Brits, mji katika jimbo la Kaskazini Magharibi.
Sungusungu hawa ni wakulima kutoka kikundi kiitwacho Afriforum. Wanasema wanawakilisha maslahi ya watu weupe na wana zaidi ya wanachama 300,000 kote nchini.
Wakiwa na magari, baiskeli na ndege zisizo na rubani wanafanya msako usiku kucha katika mashamba na majengo yaliyotelekezwa. Wanasema wanatafuta bidhaa zilizoibwa na kufichwa ili zichukuliwe baadaye, au mtu yeyote anaezurura na anaeonekana kuwa na walakini.
Wengi wao, kama vile Dewald van Wyngaardt, wana silaha.
"Huwezi kwenda kwenye mapigano ya bunduki na kisu. Sitasita kuilinda familia yangu,” anasema.
Wakulima huchukua zamu kufanya doria usiku kucha, wakati mwingine mara nne au tano kwa wiki. Johan de Klerk, kutoka Afriforum na kiongozi wa walinzi wa mashambani, amekuwa akifanya kazi hii kwa miaka mitano sasa.
"Tunalazimika kuwafungia kondoo wetu kila usiku ili kuhakikisha kuwa tuna kitu cha kutushughulisha kesho yake. Ni vigumu kuendelea hivi, kwa sababu unafanya kazi siku nzima na usiku unafanya doria.”
Mashambulizi dhidi ya wakulima wazungu yamepata mwamko wa kimataifa.
Mwaka 2018, Rais Donald Trump alituma ujumbe wa Twitter akidai serikali ya Afrika Kusini inanyakua ardhi kutoka kwa wakulima wa kizungu. Ingawa jambo hilo sio la kweli. Pia alisema kuna "mauaji makubwa ya wakulima."
Julai mwaka jana, mkuu wa Tesla mzaliwa wa Pretoria, Elon Musk, aliandika kwenye ukurasa wa twitter kuhusu chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters, akisema: "Wanachochea waziwazi mauaji ya kimbari ya watu weupe nchini Afrika Kusini."
Hakuna ushahidi kwamba wakulima wako katika hatari kubwa zaidi kuliko watu wengine wote.
Takwimu zinaonyesha Wazungu wa Afrika Kusini ni takribani 7% tu ya watu na wanaathiriwa na mauaji kwa 2% tu, hata hivyo hofu miongoni mwa jamii ya wakulima ni ya kweli.
Juhudi za Serikali
Polisi wanakubali kwamba "uhalifu uko katika viwango visivyokubalika katika baadhi ya maeneo ya nchi," lakini katika taarifa kwa BBC msemaji wa wizara ya polisi alisema "njia mbalimbali zimeanzishwa ili kupambana na uhalifu".
Ni pamoja na kuajiri maafisa wa polisi 30,000 katika kipindi cha miaka mitatu. Bajeti za polisi pia zimeongezeka karibu mara mbili katika miaka 20.
Lakini kuhusu baadhi ya matendo ya vikundi vya sungusungu, msemaji huyo alikuwa wazi kuwa "vitendo nje ya sheria kamwe haviwezi kusamehewa au kuvumiliwa na mwanajamii yeyote ambaye anaamua kuchukua sheria mkononi, sheria yenyewe itaendelea kukabiliana nae."
Hata hivyo, kauli hiyo huenda isiwazuie - kwa sababu viwango vya uhalifu vinasalia kuwa vya juu, na baadhi ya watu nchini Afrika Kusini wako tayari kufanya chochote wanachohisi kinahitajika kulinda jamii zao.