Baridi kwa barafu Makete Njombe kulikoni?

Iliyochapishwa

Na Lulu Sanga

BBC Swahili

Njombe

Chanzo cha picha, Benjamin Kachingwe

Kwa nchi za  Afrika Mashariki suala la kuona barafu mitaani si jambo la kawaida sana japo hutokea msimu kwa msimu katika baadhi ya maeneo machache ya nyanda za juu.

Kwa upande wa Tanzania kumekuwa na taarifa mbali mbali juu ya hali ya baridi iliyokithiri katika Wilaya ya Makete iliyopo mkoani Njombe kusini magaribi mwa Tanzania.

Picha zinazo onyesha ukungu mzito na mabarafu pia zimekuwa zikisambazwa mtandaoni kwa takribani wiki tatu sasa.

Baadhi ya mitandao imekua ikirusha taarifa za kiwango cha joto katika wilaya ya makete zinazo onyesha mpaka nyuzi  joto 0. 

Taarifa iliyotolewa wiki hii na Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA) inaonyesha mkoa wa Njombe kuwa na kiwango cha chini cha joto cha nyuzi joto nne huku taarifa hiyo ikitabiri huenda kiwango hiki kikashuka zaidi hasa maeneo ya milimani.

 Lakini je hali hii ya baridi na barafu katika wilaya ya makete ni jambo jipya?

BBC imefanya mazungumzo na baadhhi ya wazaliwa na wakazi wa makete wao wanasema baridi ni sehemu ya maisha yao na joto hawawezani nalo.

Daktari Angelo Sanga mzaliwa wa Makete anasema wengi wanashangaa sababu zamani habari hizi zilikua haziwafikii labda sababu hakukuwa na mitandao.

''Sisi wazawa wa makete hii ni hali ya kawaida sana kwetu, na ndio maana nyumbani kwetu kila nyumba ina jiko ndani huwa tunaota moto wa kuni kupambana na makali ya baridi'' anasisitiza Sanga.

Nae  Godfrey Mahenge anasema hakuna jipya hapo huku akiturudisha nyuma miaka ya sabini kwenda themanini ambapo wazazi walikua wanawawekea makaa ya moto kwenye vibati ambavyo walienda navyo shule kisha kuviweka miguuni ili kupinguza baridi wanapokua darasani.

 ''Tulitembea na moto kwenda shule, njia nzima tulijizungusia kupambana na baridi kali. Kwetu ukisahau nguo nje asubuhhi unaikuta imeganda kwa barafu'', anasimulia Mahenge.

Benjamin Kachib

Chanzo cha picha, Benjamin Kachib

Njia za asili wanazotumia kupambana na baridi Makete Njombe

Bi Oliva Mahenge anasema inamlazimu kuwavalisha watotowake suruali mbili na blauzi mbili za kaba shingo kishha zinafuata sare za shule na juu huwaongezea masweta mawili na glovu mikononi ambazo huzivua wakati wa kuandika tu darasani wakimaliza wanavaa tena.

Baadhi wanasema wanabeba mabakuli ya bati yenye mkaa wa moto na kutembea nayo hhasa nyakati za asubuhi na jioni ili kupunguza makali ya baridi.

Pia katika vituo ama kwenye vijiwe vya waendesha pikipiki wao huwa wanakoka moto na kuuzunguka wakati wakisubiri wateja

Benjamin Kachingwe

Chanzo cha picha, Benjamin Kachingwe

Mamlaka ya hali ya hewa inasemaje?

Kwa mujibu wa mamlaka ya hali ya hewa, Njombe ndio mkoa ambao umekuwa ukirekodi kiwango cha chini zaidi cha joto kwa miongo kadhaa sasa.

Hata hivyo Mamlaka hiyo haikufafanua zaidi juu ya wilaya Makete lakini imesisitiza kuwa inawezekana kabisa kuwa makete kiwango chake cha chini cha joto kikashuka Zaidi mpaka kufikia nyuzi joto mbili na hata sifuri.

''Katika wilaya ya makete hatuna kituo ila kipo Njombe hivyo katika taarifa yetu tumeweka wazi kuwa kiwango cha chini cha joto kimefikia nyuzi joto nne (4) njombe hivyo maeneo ya makete na maeneo mengine ya milimani joto linaweza shuka zaidi mpaka nyuzi joto sifuri'',anasema Bi Rose kutoka mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania.

TMA  imesisitiza hali ya baridi kali itaendelea mpaka mwanzoni mwa mwezi wa nane ambapo hali ya joto itaanza kurejea taratibu japo kwa njombe huwa joto haliongezeki sana. Na kwa watu wa Makete wanasema hata msimu wa joto kwao huwa bado kuna baridi.