Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ukraine na Urusi: Silaha za Urusi zilizotekwa na Ukraine zawekwa katika maonesho
Maonesho hayo ya kivita, ambayo ni pamoja na vifaru vilivyoharibika aina ya T-90, mfumo wa ulinzi wa anga wa Buk na Msta howitzer, yalizinduliwa kwenye Letna Plain, eneo kubwa la wazi lililo umbali mfupi kutoka Prague.
"Maonyesho haya yanathibitisha jinsi uungwaji mkono kutoka kwa nchi washirika ulivyo muhimu kwetu," Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ukraine Denys Monastyrsky aliambia BBC kupitia barua pepe baada ya kuzindua maonyesho hayo.
"Propaganda za Kirusi zinapenda kuwatisha watu kwamba mizinga yao inaweza kufika Prague, Berlin au Paris. Waukraine wanaonyesha – jinsi silaha hizo zilivyochakaa tu," alisema.
Maonyesho hayo - yaliyoandaliwa na wizara yake - pia yanajumuisha makombora ambayo yamekuwa yakipiga miji ya Ukraine tangu vita vya Urusi dhidi ya nchi hiyo kuanza mnamo Februari.
"Kwa maonyesho haya tunatumai kuonyesha kwa mara nyingine tena vitisho vya vita ambavyo uchokozi wa Urusi umeleta Ukraine," msemaji wa ubalozi wa Ukraine Tetiana Okopna aliambia Televisheni ya Czech.
"Lakini pia tunataka kuonyesha jinsi silaha za Czech zinavyotumiwa," aliendelea, akiongeza kuwa maonyesho kama hayo yalikuwa yakizinduliwa huko Warsaw, na mengine yakipangwa kufanyika Ujerumani na Uholanzi.
Aliyesimama kando ya Bw Monastyrsky alikuwa mwenzake wa Czech Vit Rakusan, pamoja na meya wa Prague Zdenek Hrib na Kamishna wa Ulaya Ylva Johansson.
"Mamilioni ya raia wa Ukraine wamelazimika kukimbia uvamizi wa Urusi," Bi Johansson aliuambia umati wa watazamaji waliokusanyika kwa maonyesho hayo.
"Ninasujudu mbele ya mshikamano wa ajabu wa Wacheki walioonyesha wakimbizi wa Ukraine. Mlichofanya sio tu hapa Prague lakini kote nchini ni mfano kwa Ulaya," aliongeza.
Balozi anayeondoka nchini Ukraine Yevhen Perebhinis amekuwa na jukumu muhimu katika kutafuta uungwaji mkono kwa nchi yake miongoni mwa wanasiasa wa Czech na umma.
Mapema katika mzozo huo ubalozi wa Ukraine uliungana na wizara ya ulinzi ya Czech kuanzisha kampeni ya kuhamasisha uma ili kuinunulia Ukraine silaha za Czech. Imeongeza zaidi ya €50m (£42m).
Serikali ya Czech, wakati huo huo, imekuwa mojawapo ya wafuasi wa kwanza na wakubwa wa Ukraine .
Jamhuri ya Czech ilikuwa nchi ya kwanza kutuma mizinga kwa Ukraine: Mizinga mikubwa aina ya T-72 kutoka kwa hifadhi yake ya akiba ya Jeshi la Czech. Tangu wakati huo imetuma silaha nzito zaidi, zikiwemo helikopta aina ya Mi-24.
Hata hivyo, uhamisho huo - mchanganyiko wa michango na ununuzi wa silaha - umegubikwa na utata wa kimkakati. Hata baada ya waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin kuishukuru hadharani Prague kwa kutuma ndege zake aina ya Mi-24 huko Kyiv, wizara ya ulinzi ya Czech ilidumisha kile kilichokuwa kimya kidiplomasia.
Picha za helikopta zenye nembo ya Kiukreni zimeonekana kwenye tovuti za kijasusi za wazi kwenye Twitter, inaonekana baada ya kutumwa kwenye uwanja wa vita.
Lakini wakati uungwaji mkono kwa Ukraine miongoni mwa Wacheki ukiendelea kuwa juu, wengine wana wasiwasi kuhusu athari za kupanda kwa bei ya nishati na vyakula kulikosababishwa na mzozo huo. Kuna hofu kwamba watu hapa katika Jamhuri ya Czech na kote Ulaya watapoteza hamu ya vita polepole.
Bwana Monastyrsky sio miongoni mwao.
"Hatuogopi kwamba Ulaya itapoteza hamu yetu," waziri huyo aliambia BBC.
"Tunahofia kwamba watu wengi zaidi watakufa kutokana na mauaji ya wanajeshi wa Urusi, mashambulizi ya makombora, milipuko ya migodi, nyumba zilizoanguka, au ukosefu wa chakula.
"Ikiwa dunia inatamani maendeleo endelevu na amani, lazima iondoe sababu ya matatizo - uvamizi wa Urusi. Ni lazima iwe uhamisho wa kisiasa, vikwazo vya kiuchumi, na silaha kwa jeshi la Ukraine."