Kwanini kande, mbege na machalari ni bora kuliko Pizza na Burger?

- Author, Na Yusuph Mazimu
- Nafasi, BBC Dar es Salaam
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Utafiti mpya uliofanyika nchini Tanzania na kuchapishwa na jarida kubwa la Nature Medicine la nchini Uingereza mwishoni mwa wiki, umebaini kuwa lishe ya asili ya Kiafrika ina faida kubwa kiafya kuliko lishe ya Kimagharibi.
Utafiti huo ulioanza kufanyika mwaka 2021 umefanywa na watafiti wa Chuo Kikuu cha KCMC na Taasisi ya Utafiti ya KCRI na kubaini kwamba mabadiliko ya lishe ya wiki mbili yananatosha kuleta mabadiliko ama chanya ama hasi katika mfumo mzima wa kinga ya mwili.
Utafiti huo ulioshirikisha watu 77 wenye afya njema kutoka maeneo ya mijini na vijijini, ulilenga kuangalia athari za vyakula vya asili dhidi ya vyakula vya kisasa na vya mjini vinavyofanana na vya Magharibi kwa afya ya mwili. Ukizingatia mfumo wa kinga ya mwili na jinsi unavyoweza kukabiliana na magonjwa.
"Tulifanya utafiti huu kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali za kimataifa, lakini tukalenga Moshi, Kilimanjaro kwa sababu watu bado wanatumia vyakula vya jadi," anasema Godfrey Temba, mtafiti kutoka timu ya utafiti ya KCMC, ambaye pia Daktari wa kinga ya mwili.
Vyakula vilivyothibitishwa kuwa ngome ya afya
Vyakula vilivyofanyiwa utafiti ni vyakula vya asili, kienyeji, jadi na Afrika ambavyo hasa vilikuwa vyakula vya watu wa asili ya Kilimanjaro, ambao wengi ni Wachaga, dhidi ya vyakula vya kisasa, vya mjini na vinavyotumika zaidi na watu wa Magharibi.
Washiriki wa utafiti waligawanywa kwenye makundi matatu, kundi la kijijini, ambao walibadilisha mlo kutoka kula vyakula vya asili wakala vyakula vya kisasa kwa wiki mbili, kundi la pili ni la wale wa mjini waliobadili mlo na kula vyakula vya asili na kienyeji kwa wiki mbili pia, na kundi la tatu walipewa kinywaji cha asili ya mbege inayotengenezwa kwa kutumia ndizi mbivu, kimea cha ulezi, na maji.
Baadhi ya vyakula vya asili vilivyotumika ni kande (mahindi na maharage), Machalari (ndizi nyama), Kiburu (ndizi maharage) kinywaji cha asili cha mbege, mbogamboga, viazi vitamu, ugali wa dona au muhogo, uji wa ulezi, matunda ya msimu kama parachichi na chai ya rangi. Ingawa vyakula hivi pia vinatumika na baadhi ya watu wa asili nyingine mbali na Wachaga. Kande iliyotumia mahindi yasiyokobolewa, ikiwekwa chumvi kidogo bila mafuta ni chakula cha asili chenye afya.
Kwa upande wa vyakula vya kisasa, washiriki walipewa wali mweupe wa mafuta, mikate ya Sandwich, chapati, Juisi za pakiti, Soseji na Chipsi mayai, tambi, ugali wa sembe, pizza na chai ya maziwa, vyakula vilivyozoeleka mijini na kwenye migahawa ya haraka. Vyakula hivi vinalika sana Ulaya Magharibi, vinavyojumuisha pia vyakula kama Pizza na Burger.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Matokeo ya utafiti yameonesha kuwa wale waliobadili lishe kwenda ya Kimagharibi kinga zao zilianza kupungua uwezo wake, pia protini zao mwilini ziliongezeka zinazohusiana na uvimbe mchungu (inflammation) ambazo zikiongezeka kwa kasi na kwa muda mrefu zinasababisha kupata hatari ya kupata magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza kama ya moyo, kisukari, na saratani.
Kwa upande mwingine, waliorejea kwenye lishe ya Kiafrika au waliotumia mbege walionyesha kupungua kwa viashiria vya uvimbe mchungu, na hali yao ya kinga zao za zilionyesha kuimarika.
'Tulijifunza kwamba lishe zetu za asili zina uwezo mkubwa sana wa kuimarisha kinga zetu za mwili na kutuweka mbali na hatari ya kupata magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza na hizi lishe zetu za asili hasa katika eneo la Kilimanjao, ni lishe ambazo watu wanatumia nafaka zaidi kama mahindi, ambayo maeneo ya vijijini wengi wanatumia ambayo hajakobolewa, ndizi nyama (Machalari), ndizi na maharage (Kiburu)", alisema Temba.
Kwa mujibu wa utafiti, baadhi ya madhara au faida za mabadiliko ya lishe ziliendelea kuonekana mpaka wiki nne baada ya utafiti, jambo linaloonesha kuwa vyakula unavyokula vinaweza kuwa na athari nzuri ama mbaya ya muda mrefu kwenye afya yako.
Tafiti nyingine zinasemaje kuhusu lishe asilia?

Chanzo cha picha, Getty Images
Utafiti huu sio wa Moshi pekee. Ni sehemu ya utafiti mpana uliohusisha nchi kama Uingereza, Afrika Kusini, Brazil, na Marekani, ukishirikisha jumla ya washiriki 1,205. Katika nchi za Magharibi, walioshiriki walikuwa na ulaji mkubwa wa vyakula vilivyosindikwa kwa wastani wa zaidi ya 45% ya mlo wao wa kila siku.
Tanzania ilitoa kundi dogo la watu 77, lakini mchango wake ulikuwa wa kipekee, hasa kwa sababu ya tofauti kubwa katika aina ya lishe inayopatikana maeneo ya vijijini na mijini na pia bado kuna jamii zinazotegemea lishe ya asili. Matokeo yake yaliwawezesha watafiti wa kimataifa kuthibitisha kwamba lishebora si swala la teknolojia, bali ni urithi wa maisha ya kawaida unaohitaji kuthaminiwa tena.
Utofauti wa mazingira mijini dhidi ya vijijini ulionesha kuwa watu wanaoishi maeneo ya vijijini au wenye mtindo wa maisha wa jadi walikuwa na kinga bora zaidi tofauti na wale waliotegemea vyakula vya haraka na vya kusindika na kukobolewa. Pia utafiti ulionyesha vijijini wengi wanaanda vyakula vyao kwa kuvichemsha na kuweka kiwango kidogo cha chumvi na mafuta, kuliko kundi la mjini.
Lakini Utafiti mwingine wa kimataifa uliofanywa na vyuo mbalimbali vikiwemo vya Harvard na Oxford umeonyesha athari za lishe ya asili na matumizi ya vyakula visivyosindikwa vinamchango mkubwa wa kupunguza hatari ya magonjwa sugu kama vile kisukari, magonjwa ya moyo, na saratani.
"Ukitazama data, unaona wazi kuwa watu wa vijijini ambao lishe yao haijachakachuliwa sana walikuwa na mwitikio mzuri wa kinga. Lakini hata wale wa mjini, walipobadilishiwa chakula kwa siku 14 tu, walionyesha matokeo mazuri," asema Temba.
Licha ya watafiti kuonya kula kwa wastani hasa vyakula vya wanga kama viazi, magimbi na nafaka, Utafiti huu unathibitisha umuhimu wa lishe ya asili, na jinsi vyakula visivyopitia viwanda vinavyoweza kuboresha mfumo wa kinga na afya ya mwili kwa ujumla.
Chaguo ni lako, 'kitamu' au chenye 'afya'

Chanzo cha picha, Getty Images
Utafiti huu sio tu kuhusu utofauti wa vyakula vya asili ya kiafrika na vile vya Magharibi, bali unatoa ujumbe mpana kwamba lishe ni nguzo muhimu ya kinga ya mwili. Katika kipindi ambacho magonjwa yanazidi kuongezeka, na ulimwengu ukikabiliwa na changamoto mpya kila mwaka, lishe bora inaweza kuwa ngome ya kwanza ya ulinzi.
Kwa hiyo, badala ya kulazimika kuchagua kati ya "kitamu" na "cha afya," tunapaswa kutambua kwamba ladha halisi iko kwenye vyakula vya nyumbani na kwamba afya ya muda mrefu inaanzia kwenye mlo wetu wa kila siku.
'Ukiweka mbali suala la ladha lakini hata mtu anavyojisikia inakuwa ni tofauti sana na jinsi ambavyo umezoea kula Chipsi, kula burger ukilinganisha na kula magimbi mazuri ya kienyeji', alisema mmoja wa washiriki wa utafiti.
Hata hivyo changamoto inayotajwa na wengi ni upatikanaji wa lishe ya asili hasa kwa watu waishio mjini.
"Nilishindwa kuendelea na ulaji wa chakula cha asili kutokana na mtindo wa maisha tunaoishi...na kwamba hivi vyakula vya asili upatakanaji wake na upishi mzuri kwa maeneo ya mjini ni mgumu sana', anasema mshiriki.
Pamoja na changamoto kula vyakula vya asili na kuvilinda ni wito unaozungumzwa na watafiti. Huenda leo kande, viazi vitamu, magimbi, mbege na mboga za kienyeji zikawa hazijafungashwa kwenye maboksi na vifungashio vingine vya kuvutia kama ilivyo burger au pizza, lakini ndani yake kuna kinga isiyolipiwa, kinga ambayo sasa imethibitishwa kisayansi.
End of Maelezo zaidi:
Imehaririwa na Ambia Hirsi












