Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita vya Ukraine: Ni silaha gani nzito wanazotoa Uingereza kwenda Ukraine?
Na David Brown & Tural Ahmedzade
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amekuwa nchini Uingereza kwa mazungumzo na Waziri Mkuu Rishi Sunak.
Ziara hiyo ilikuja kabla ya mashambulizi makubwa ya Ukraine dhidi ya majeshi ya Urusi, yanayotarajiwa kuanza katika wiki zijazo.
Tangu kuanza kwa mzozo nchini Ukraine, Uingereza imekuwa msambazaji mkuu wa silaha na vifaa kwenda Kyiv, ingawa kwa kiwango kidogo zaidi kuliko Marekani.
Je ni silaha gani zinapelekwa Ukraine, na zitaleta tofauti gani?
Makombora ya masafa marefu
Uingereza ilithibitisha kuwa iliipatia Ukraine makombora ya masafa marefu mapema mwezi huu.
Kombora la Storm Shadow cruise lina masafa ya zaidi ya 250km (maili 155), kulingana na mtengenezaji.
Lakini makombora ya Himars yanayotolewa na Marekani yanayotumiwa na Ukraine yana kwenda umbali wa kilomita 80 pekee (maili 50).
Kwa sasa, kombora la Storm Shadow ndiyo lenye masafu marefu zaidi ya kombora lolote linalopatikana Ukraine, na kwa hivyo inaweza kulenga maeneo ambayo awali yalionekana salama kwa vikosi vya Urusi.
Urusi inadai kombora hilo tayari limetumika dhidi ya vikosi vyake.
Uingereza ni nchi ya kwanza kusambaza makombora ya cruise kwa Kyiv.
Vifaru
Uingereza pia iliongoza katika kusambaza vifaru vikubwa kati ya nchi za Nato kwa ajili ya Ukraine.
Mnamo Januari Uingereza ilitangaza kwamba vifaru 14 vya Challenger 2 vitatumwa Ukraine, pamoja na karibu bunduki 30 za kujiendesha zenyewe za AS90.
Challenger 2 vilitengenezwa katika miaka ya 1990, lakini ni vya kisasa zaidi vile vya Warsaw Pact vinavyotumiwa na Ukraine.
Kufuatia tangazo la Uingereza, wengine kadhaa walijitolea kutuma vifaru kwa Ukraine, ikiwa ni pamoja na Ujerumani kupitia vifaru vyake vya Leopard 2.
Wachambuzi wengi wa masuala ya kijeshi wanaamini kwamba vifaru, kwa kuangalia mifumo mingine ya silaha, itakuwa muhimu kwa jaribio lolote la Ukraine la kuondoa majeshi ya Urusi kutoka kwenye maeneo yenye ngome nyingi katika mashambulizi yanayotarajiwa kufanywa wiki chache zijazo.
Ndege zisizo na rubani
Siku ya Jumatatu, Downing Street ilisema kwamba itapeleka "mamia" ya ndege zisizo na rubani na makombora ya ulinzi wa anga huko Ukraine.
Taarifa hiyo haikufichua ni aina gani ya ndege zisizo na rubani zitatolewa, lakini ilisema zitakuwa na masafa ya zaidi ya maili 124 (200km).
Mnamo 2022, Wizara ya Ulinzi ilitangaza usambazaji wa mifumo ya ndege nzito zisizo na rubani ili kutoa msaada wa vifaa kwa vikosi vya Ukraie.
Wachambuzi wanasema kwamba ndege zisizo na rubani zinaweza kuwa na ufanisi mkubwa katika kushambulia vifaa vilivyo mbali kwa askari wa mstari wa mbele, hasa kwenye tishio la mizinga ya Kirusi na katika hali ambapo kuna hatari ya kuzingirwa.
"Ni moja ya vifaa vingi vinavyohitajika na wanajeshi," anasema Justin Bronk wa Taasisi ya Huduma za Kifalme (Rusi). "Kila wakati unaweza kutumia ndege isiyo na rubani kushambulia badala ya askari ambaye anakuwa kwenye hatari kubwa."
Mifumo ya roketi
Mchango wa mifumo ya roketi ya M270 yenye zana za usahihi za M31A1 kwa Ukraine ulithibitishwa mnamo 2022.
Mfumo wa M270 wa Uingereza ni sawa na mifumo ya American Himars.
Jack Watling Rusi aliiambia BBC: "Mifumo hii ndiyo hasa Ukraine inachohitaji. Inawaruhusu Waukraine kushinda mifumo mingi ya mizinga ya Kirusi na pia kushambulia kwa usahihi."
Silaha au mifumo ya kupambana na vifaru
Uingereza imetuma zaidi ya mifumo au silaha 5,000 za kisasa za kuzuia vifaru, au Nlaw, kwenda Ukraine.
Nlaws zimetengenezwa kuharibu mizinga katika umbali mfupi kwa kutumia shambulio moja.
Muhimu sana kwa vikosi vya jeshi vya Ukraine vinavyohitaji silaha haraka, makombora hayo ni rahisi kusafirisha na ni rahisi kutumia. Askari anaweza kufundishwa kuzitumia chini ya siku moja.
Wachambuzi wengi wanaamini kuwa yatakuwa na mchango mkubwa katika muelekeo wa mzozo katika siku zilizofuataza uvamizi wa Urusi.
Makombora ya masafa mafupi
Makombora ya Maritime Brimstone pia yalitumwa Ukraine mnamo 2022.
Brimstone yanaweza kutumika dhidi ya vifaru, mizinga na vyombo vingine vidogo, kwa mujibu wa Kapteni Chris Carlson, aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Wanamaji la Marekani.
Makombora hayo huwa yanarushwa kutoka kwenye ndege, lakini nchini Ukraine yanafanyiwa marekebisho ili yarushwe kutoka kwenye malori.
Kurushwa kutoka ardhini kunapunguza ufanisi wake mzuri, anasema Capt Carlson.
"Yote inategemea wapi unalenga," anasema. "Ikiwa utapiga injini au karibu na njia ya maji, unaweza kuwapa adui matatizo makubwa."
Magari ya kivita
Uingereza imetoa angalau magari 120 ya kivita kwa Ukraine, yakiwemo magari ya doria ya Mastiff.
Magari ya Mastiff yalikuwa maarufu sana miongoni mwa wanajeshi wa Uingereza nchini Afghanistan kwani yanatoa ulinzi wa hali ya juu dhidi ya mabomu ya ardhini na vilipuzi vingine vya kisasa.
Wachambuzi wanasema kwamba katika eneo ambalo limechimbwa sana kama Donbas, Mastiffs yanaweza kuwa muhimu sana.
Inafahamika kuwa pande zote mbili katika mzozo huo zimekuwa zikitumia sana mabomu ya ardhini.
Mifumo ya ulinzi wa anga
Uingereza inasema imetoa angalau mifumo sita ya ulinzi wa anga, ikiwa ni pamoja na makombora ya Starstreak.
"Kwa rubani, Starstreak ni kitu kibaya," asema Bw Bronk. "Hauna unachoweza kufanya (dhidi ya mfumo huu)."
Anasema vikosi vya Urusi vinaweza kuona oparesheni zingine kuwa hatari sana ikiwa vinafahamu kuwa silaha hatari kama Starstreak iko ardhini.
Uingereza pia imetoa magari ya Stormer kusaidia makombora ya Starstreak.
Silaha zingine zilizotolewa na Uingereza kwenda Ukraine ni pamoja na:
Makombora ya kuzuia vifaa
Mabomu
Vilipuzi vya plastiki
Silaha ndogondogo
Kofia ngumu
Vifaa vya vita vya elektroniki
Mifumo ya rada
GPS