Mgogoro wa Sudan: 'Tunakula kiduchu ili chakula kiweze kudumu'
Na Fernando Duarte, BBC

Chanzo cha picha, Getty Images
Mapigano yanayoendelea katika mji mkuu wa Sudan sasa yanaathiri pakubwa usambazaji wa chakula, pamoja na kutatiza upatikanaji wa maji na umeme, kulingana na wakaazi wa Khartoum waliozungumza na BBC.
"Tuna chakula cha kutosha kwa siku mbili tu," Nisreen Al-Saim alisema.
Al-Saim aliongeza kuwa yeye na familia yake sasa wanapunguza kiwango cha chakula wanachotumia kwa matumaini kwamba kitadumu kwa muda mrefu.
Kukatwa kwa maji na umeme kumeathiri nyumba nyingi za Sudan tangu mapigano yalipoanza kati ya wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) na jeshi la Sudan tarehe 15 Aprili.
Pande hizo mbili zimekuwa zikigawana madaraka na mkuu wa jeshi, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, kama kiongozi na mkuu wa RSF, Mohamed Hamdan Dagalo kama naibu wake, lakini wameanza kupigana.
Kufikia Aprili 19, zaidi ya watu 200 walikuwa wamekufa na angalau 1,800 walikuwa wamejeruhiwa, kulingana na mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Volker Perthes.
Kufungwa kwa maduka
Huko Bahri, kaskazini mwa Khartoum, watu walioshuhudia tukio hilo waliambia BBC kwamba kituo kikuu cha kusukuma na kusambaza maji kimeathirika.
Hind, mkazi wa eneo hilo, alisema kukatika kwa maji mara kwa mara kulimlazimu yeye na familia yake kutegemea tu akiba yao ya abri - kinywaji cha nafaka ambacho kawaida hutumika wakati wa Ramadhani - ili kukata kiu yao.

Chanzo cha picha, Getty Images
Hind aliongeza kuwa maduka yote katika mtaa wake yalikuwa yamefungwa isipokuwa baadhi ya maduka ya mikate, na hata hayo pia ya unga kidogo wa ngano.
Siku chache kabla ya mapigano kuanza, jeshi lilikuwa limewaonya raia kuweka akiba ya chakula kufuatia kutumwa kwa wafanyakazi wa RSF katika maeneo tofauti ya mji mkuu.
Lakini Heba, mkazi mwingine wa Khartoum, aliiambia BBC kwamba "ni familia chache tu" zilizochukua ushauri huo kwa umakini, kwani hakuna mtu aliyefikiria kuwa hali hiyo ingeongezeka kwa kiwango cha sasa.
"Hatukutaka kwenda nje kwenye joto kwani tayari tulikuwa tumehifadhi chakula cha Ramadhani," Heba aliongeza.
Msaada wa UN umesitishwa
Hata hivyo, kitongoji cha Heba kinapata umeme kwa saa mbili tu kwa siku, ambayo ina maana kwamba chakula ambacho baadhi ya familia zimehifadhi kinaweza kuharibika.
Haijulikani ni kwa muda gani ugavi utalazimika kusimama, ikizingatiwa kuwa haijulikani mapigano yatakoma lini.
Usitishaji mapigano wa saa 24 ulioratibiwa na Marekani ulitangazwa awali tarehe 18 Aprili, lakini ulisambaratika huku mapigano yakiendelea kati ya pande zinazopigana.
Walioshuhudia waliripoti kuwa katika vitongoji vya Khartoum ambako mapigano angalau yametulia kiasi cha maduka ya mboga kufunguliwa tena, kuna foleni na bidhaa kama vile maji ya chupa ni chache.
Katika maeneo mengine, wakaazi bado wanaogopa hata kuacha milango yao wa mbele.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mambo yanayozidi kuwa magumu, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilitangaza kusitisha utoaji wa misaada kwa Sudan tarehe 16 Aprili kufuatia kifo cha wafanyakazi wake watatu katika eneo la Darfur.
Mapema mwaka huu, Umoja wa Mataifa ulisema kwamba thuluthi mbili ya Wasudan (takriban watu milioni 15.8) walikuwa tayari wanahitaji misaada ya kibinadamu mwaka 2023, hali iliyozidi kuwa mbaya zaidi baada ya misaada ya kimataifa kutoka kwa nchi wahisani kukoma kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya 2021 ambayo yalimuondoa madarakani Waziri Mkuu wa kiraia Abdalla Hamdok. .
Abla Karrar, msemaji wa muungano wa kisiasa unaojulikana kama Forces for Freedom and Change, alielezea masikitiko yake kwa uamuzi wa Umoja wa Mataifa wa kusitisha misaada kutokana na kile alichokiita "hali mbaya".
"Sudan tayari inakabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi, na kwa hivyo akiba ya chakula majumbani, haijalishi ni kubwa kiasi gani, haitatosha," alisema katika taarifa yake.
Karrar pia alisisitiza haja ya kusitisha mapigano kabla ya nchi kuingia katika "mgogoro mkubwa wa kibinadamu".












