Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ukraine inakabiliwa na uhaba mkubwa wa mifumo ya ulinzi wa anga
Mashambulizi ya makombora na droni yaliyofanywa na Urusi usiku wa kuamkia Jumatano dhidi ya mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, na maeneo yanayouzunguka yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 17 na kujeruhi makumi wengine, kwa mujibu wa mamlaka za Ukraine.
Mashambulizi hayo ni sehemu ya wimbi la hivi karibuni la mashambulizi mabaya ya Urusi, wakati Ukraine ikiendelea kutoa wito kwa washirika wake kuongeza msaada wa mifumo ya kujihami dhidi ya makombora, hususan mifumo ya Patriot kutoka Marekani.
Milipuko ilisikika mjini Kyiv muda mfupi baada ya saa sita usiku (takribani saa 3:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki), baada ya Jeshi la Anga la Ukraine kutoa onyo kuhusu mashambulizi ya makombora ya masafa mafupi yaliyokuwa yakielekezwa katika mji huo.
Uhaba wa mifumo ya ulinzi wa anga
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, alitangaza Jumatano kuwa watu 17 waliuawa katika mashambulizi hayo.
Akizungumza baada ya shambulio hilo, Zelensky alisema kuwa kama kungekuwa na idadi ya kutosha ya makombora ya kuzuia makombora ya balistiki, maisha ya baadhi ya waliopoteza maisha yangeokolewa.
Rais huyo pia alionya kuwa Ukraine inakabiliwa na uhaba mkubwa wa mifumo ya ulinzi wa anga, ambayo ni muhimu katika kukabiliana na mashambulizi ya makombora, hasa wakati Urusi ikizidi kutumia makombora ya balistiki katika mashambulizi yake.
Zelensky aliwataka washirika wa Ukraine kuongeza msaada wa kijeshi, hususan kwa kuipatia nchi hiyo mifumo zaidi ya kisasa ya ulinzi wa anga ili kulinda raia na miundombinu muhimu dhidi ya mashambulizi yanayoendelea.
End of Unaweza kusoma
Mamlaka za eneo zilisema watu zaidi ya 40 walijeruhiwa katika mji mkuu wa Kyiv na maeneo yanayouzunguka kutokana na mashambulizi hayo.
Ingawa Ukraine imefanikiwa kutungua idadi kubwa ya droni zinazorushwa na Urusi, bado inategemea msaada wa washirika wake wa kimataifa kupata mifumo na makombora ya kujihami dhidi ya mashambulizi ya makombora ya Urusi.
Mkuu wa utawala wa kijeshi wa mji wa Kyiv, Timur Tkachenko, aliandika kupitia mtandao wa Telegram kwamba:
"Usiku wa leo, eneo la Kyiv limeshuhudia moja ya mashambulizi mabaya zaidi ya adui kuwahi kutokea hadi sasa."
Mashambulizi hayo yameongeza hofu kuhusu kuongezeka kwa mashambulizi ya anga ya Urusi na kuimarisha wito wa Ukraine kwa washirika wake kuongeza msaada wa mifumo ya ulinzi wa anga.
Mkuu wa utawala wa kijeshi wa Kyiv, Timur Tkachenko, aliongeza kusema:
"Urusi kwa mara nyingine imeleta kifo na uharibifu katika ardhi yetu na kuwaua raia wasio na hatia. Kutakuwa na haki kwa kila uhalifu wa aina hii."
Kwa upande wake, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema kuwa uhaba wa makombora ya kuzuia makombora ya balistiki "unaipa Urusi ujasiri wa kuendelea kufanya mashambulizi ya mauti."
Mwishoni mwa Julai, Zelensky alikutana na Rais wa Marekani Donald Trump katika Ikulu ya White House, ambako aliomba Marekani iruhusu Ukraine kuzalisha makombora ya Patriot ndani ya nchi kupitia leseni maalumu.
Ingawa Zelensky alisema baada ya mkutano huo kuwa Trump alikuwa amekubali kutoa leseni hiyo, rais wa Marekani alieleza tu kwamba walijadili "mambo mengi" na kwamba mazungumzo yao "yalikwenda vizuri sana."
Baadaye, Trump alisema Marekani inapaswa kuwa "makini sana" kabla ya kuipa Ukraine ruhusa ya kuzalisha makombora hayo.
Katika miezi ya hivi karibuni, Urusi imeongeza kwa kiwango kikubwa mashambulizi dhidi ya mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, kwa kutumia makombora ya balistiki ambayo ni vigumu kuyazuia. Mashambulizi hayo hufanyika kwa kasi na ndani ya muda mfupi, yakitikisa majengo na kusababisha milipuko mikubwa kusikika katika jiji lote.
Jeshi la Anga la Ukraine lilisema lilifanikiwa kudungua droni 98 kati ya 115 zilizorushwa na Urusi usiku wa Jumanne kuamkia Jumatano. Hata hivyo, takwimu za awali zilionesha kuwa halikufanikiwa kudungua hata kombora moja la Urusi katika shambulio hilo.
Katika tukio jingine kubwa la hivi karibuni, mashambulizi ya Urusi dhidi ya Kyiv na vitongoji vyake Jumamosi iliyopita yaliua watu 10 na kujeruhi zaidi ya 30.
Wakati huohuo, droni za Ukraine zilifanikiwa kuzamisha meli kubwa ya mizigo ya Urusi katika Bahari Nyeusi, ikiwa ni moja ya mashambulizi makubwa ya Ukraine dhidi ya miundombinu ya kijeshi ya Urusi katika siku za karibuni.
Mataifa ya Ulaya yalaani mashambulizi
Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen, Jumatano alilaani kile alichokiita "ukatili wa kutisha" uliofanywa na Urusi katika eneo la Kyiv, na kutangaza msaada wa ziada wa euro bilioni 1.4 kwa juhudi za vita za Ukraine.
Fedha hizo zinatokana na riba iliyopatikana kutoka kwenye akiba ya fedha za Urusi zilizoshikiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) baada ya uvamizi wa Ukraine.
Katika taarifa yake, von der Leyen alisema:
"Urusi lazima iwajibike kwa uharibifu unaousababisha. Tunatumia mapato yanayotokana na mali za Urusi zilizozuiwa kuhakikisha kuwa inafanya hivyo."
Aliongeza kuwa:
"Tunatoa euro bilioni 1.4 zaidi kutoka katika mapato hayo kwa Ukraine. Fedha hizi zitasaidia Ukraine kuendelea kujitetea dhidi ya vita haramu vya Urusi."
Kwa upande wake, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, alilaani mashambulizi ya hivi karibuni ya Urusi dhidi ya mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, akisema kuwa Umoja wa Ulaya na washirika wake wataongeza shinikizo dhidi ya Moscow kupitia vikwazo vipya na wataendelea kuipa Ukraine msaada wa kijeshi.
Macron aliandika kupitia mtandao wa X:
"Umoja wa Ulaya na washirika wake wataendelea kuongeza shinikizo dhidi ya Urusi, ikiwemo kupitia vikwazo vipya, huku tukiongeza msaada wa kijeshi kwa Ukraine ili iweze kujilinda na kulinda raia wake."
Mashambulizi ya Urusi yalilenga maeneo gani?
Mamlaka za Ukraine zilisema mashambulizi ya Urusi yaliyofanyika usiku wa Jumanne kuamkia Jumatano yalilenga zaidi maghala ya kampuni za kiraia pamoja na miundombinu muhimu katika mji wa Kyiv na maeneo yanayouzunguka.
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, alisema mashambulizi hayo yalilenga hasa:
"Maghala yanayomilikiwa na kampuni za kiraia. Miundombinu na kituo cha reli pia vililengwa."
Aliongeza kuwa:
"Maeneo hayo hayakuwa na uhusiano wowote na vita. Kulikuwa na kiwanda cha kutengeneza bia, maghala ya vifaa vya ujenzi na vituo vya kiraia vya kuhifadhi na kusambaza bidhaa."
Kwa upande wake, Urusi ilisema mashambulizi hayo yalilenga vituo vya usafiri, usafirishaji wa mizigo na usambazaji katika mji na eneo la Kyiv, ambavyo ilidai vilikuwa vinatumika kuhifadhi na kusafirisha silaha pamoja na vifaa vya kijeshi, ikiwemo ndege zisizo na rubani.
Wakati huohuo, Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilitangaza Jumatano kuwa majeshi yake yalishambulia meli tatu zilizokuwa zikitumika kusafirisha mizigo ya kijeshi ya Ukraine katika Bahari Nyeusi, kwa mujibu wa shirika la habari la Urusi, Interfax.
Mashambulizi ya kujibu ya Ukraine
Nchini Urusi, Meya wa Moscow alisema Jumatano kuwa mifumo ya ulinzi wa anga ya nchi hiyo ilifanikiwa kutungua na kuharibu angalau droni 10 zilizokuwa zikielekea mji mkuu huo.
Gavana wa mkoa wa Tula, ulioko kusini mwa Moscow, pia alisema vikosi vya ulinzi wa anga vilitungua droni 107 za Ukraine zilizorushwa usiku kucha.
Aliongeza kuwa mashambulizi hayo yalisababisha uharibifu wa angalau majengo mawili ya makazi. Aidha, droni moja ilianguka ndani ya kituo cha usafirishaji na uhifadhi wa bidhaa cha kampuni ya Wildberries, na kusababisha moto.
Kampuni hiyo ilithibitisha kuwa iliamuru wafanyakazi kuondolewa katika eneo hilo kama hatua ya tahadhari.
Siku ya Jumanne asubuhi, watu watano waliuawa na wengine 10 kujeruhiwa katika mkoa wa Moscow kufuatia mashambulizi yaliyolenga maghala ya kampuni hiyo.
Wildberries, kampuni kubwa ya biashara mtandaoni nchini Urusi, imeripotiwa kulengwa na takriban mashambulizi 12 tangu katikati ya mwezi Julai. Mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya takribani watu wanane na kuvuruga sehemu kubwa ya uwezo wa kampuni hiyo wa kuhifadhi bidhaa.
Kwa upande wake, Ukraine inaishutumu Wildberries kwa kuhifadhi vipuri vya ndege zisizo na rubani na kusaidia shughuli za kijeshi za Urusi, madai ambayo yamekuwa yakitumiwa na Kyiv kueleza sababu za kuilenga kampuni hiyo.