Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

“Kwa nini tupigane ikiwa tunaweza kuzungumza?” – Rais wa Iran

Kwa upande mwingine, afisa mmoja wa Marekani ameiambia Reuters kuwa kumekuwa na maendeleo mazuri katika mazungumzo kati ya Iran na Oman kuhusu Mlango Bahari wa Hormuz, huku Washington ikitarajia makubaliano kufikiwa hivi karibuni.

Moja kwa moja

Na Abdalla Seif Dzungu

  1. Uhispania yaweka udhibiti wa mpaka dhidi ya Italia huku mzozo kuhusu wimbi la wahamiaji huko Ceuta ukizidi kushika kasi

    Hispania imeweka udhibiti wa mpaka kwa safari zote za anga na baharini kutoka Italia huku mzozo kati ya nchi hizo mbili za Umoja wa Ulaya ukizidi kushika kasi.

    Hatua hizo - ambazo zilianza saa sita usiku (saa 22:00 GMT) na zitadumu kwa mwezi mmoja - zinakuja wiki moja baada ya Italia kuweka vikwazo kama hivyo kufuatia kuingia kwa wahamiaji wapatao 78,000 kutoka Morocco hadi eneo la Ceuta, ambalo ni himaya ya Hispania iliyo ndani ya ardhi ya Morocco.

    Maafisa wa Hispania walisema nyaraka za asilimia 5 hadi 10 ya abiria zilikuwa zikikaguliwa kabla ya kuruhusiwa kushuka kwenye ndege. Italia pia imesema ukaguzi wake wa mpakani hufanywa kwa kuchagua abiria bila mpangilio maalum.

    Mgogoro huo umewaleta katika mzozo kiongozi wa mrengo wa kushoto wa Hispania, Pedro Sanchez, na kiongozi wa mrengo wa kihafidhina wa Italia, Giorgia Meloni - ambaye kwa muda mrefu amekuwa akitaka sheria kali zaidi za uhamiaji ndani ya Umoja wa Ulaya.

    Italia haina mpaka wa nchi kavu na Hispania. Serikali yake ilisema wiki iliyopita kuwa uamuzi wa kusitisha kwa muda makubaliano ya Schengen ambayo huruhusu watu kuvuka mipaka bila ukaguzi ulilenga kuzuia wahamiaji walioingia Ceuta kusafiri hadi Italia.

    Madrid ilipinga msimamo huo, ikisema ulitokana na "hoja zisizo na mashiko" na zisizo na ukweli wowote, kwa kuwa wahamiaji walioingia Ceuta hawakuwa na njia yoyote ya kuingia katika eneo la Schengen.

  2. IRGC: Kufunguliwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz kunategemea Marekani kukubali masharti ya Iran

    Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi (IRGC) linasema kuwa Mlango-Bahari wa Hormuz utafunguliwa tu pale Marekani itakapokubali masharti yote ya Iran.

    Wakati ripoti zikionyesha kuwa Iran na Oman ziko karibu kufikia mwafaka kuhusu Mlango-Bahari wa Hormuz, na maafisa wa Marekani wakielezea kufunguliwa kwa njia hiyo ya maji kuwa jambo linalotarajiwa kutokea "hivi karibuni," msemaji wa IRGC, Hossein Mohebbi, alisisitiza kuwa kufunguliwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz hakuhusiani na mazungumzo na Muscat.

    Hossein Mohebbi aliwaambia waandishi wa habari: "Kwetu sisi, Mlango-Bahari wa Hormuz si njia ya maji ya kiuchumi pekee, bali ni chanzo cha nguvu na uwezo ambacho kipo mikononi mwa Jamhuri ya Kiislamu kijiografia, na adui analazimika kukubali masharti ya Iran ili mlango huo ufunguliwe."

    Pia alionya dhidi ya uingiliaji wowote katika mazungumzo hayo, akibainisha kuwa mazungumzo na Oman yanakaribia kukamilika.

    Awali, mwandishi wa habari wa Axios, Barak Ravid, alinukuu mwanadiplomasia kutoka nchi inayohusika na upatanishi akisema kuwa wajumbe wa Iran wanasubiri idhini kutoka Baraza la Juu la Usalama wa Taifa la nchi yao ili kuhitimisha makubaliano na Oman pamoja na Marekani.

  3. Habari za hivi punde, UAE: Iran yalenga meli ya mafuta ya Kampuni ya Kitaifa ya Mafuta ya Abu Dhabi katika Mlango-bahari wa Hormuz

    Falme za Kiarabu (UAE) zilitangaza Jumamosi kuwa meli ya mafuta kutoka nchi hiyo ililengwa na Iran wakati ikipita katika Mlango-bahari wa Hormuz.

    Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE ililaani "shambulio la uhasama la makombora lililofanywa na Iran dhidi ya meli ya mafuta ya Kampuni ya Kitaifa ya Mafuta ya Abu Dhabi wakati ikipita katika Mlango-bahari wa Hormuz."

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hakuna mtu aliyeuawa au kujeruhiwa katika shambulio hilo.

    Kampuni ya Kitaifa ya Mafuta ya Abu Dhabi ilitangaza Ijumaa kuwa tangu kuanza kwa vita, meli zake 15 zimeshambuliwa kwa makombora na ndege zisizo na rubani wakati zikipita katika Mlango-bahari wa Hormuz, huku matukio matatu kati ya hayo yakitokea katika wiki iliyopita.

  4. Mpira wa 'Hand of God' wa Maradona kupigwa mnada Marekani

    Mpira wa soka ambao Diego Maradona aliutumia kufunga bao lake maarufu la "Hand of God" wakati Argentina ilipoifunga Uingereza katika Kombe la Dunia la mwaka 1986 unatarajiwa kuuzwa kwa dola milioni 10 katika mnada nchini Marekani mwezi huu.

    Katika bao hilo la mechi ya robo-fainali iliyochezwa kwenye uwanja wa Estadio Azteca, Maradona aliupiga mpira huo kwa ngumi na ukampita kipa wa Uingereza, huku timu hiyo ya Amerika Kusini ikifanikiwa kushinda kwa mabao 2-1.

    Baada ya mchezo huo, nyota huyo wa Argentina alisema bao lake lilifungwa "kidogo kwa kichwa cha Maradona na kidogo kwa mkono wa Mungu." Baadaye, timu ya taifa lake ilifanikiwa kutwaa taji la Kombe la Dunia.

    Kampuni ya Heritage Auctions, yenye makao yake makuu Texas, inatarajia kuwa mpira huo utauzwa kwa bei ya tarakimu nane (kiasi cha mamilioni mengi ya dola) utakapopigwa mnada kuanzia tarehe 21 hadi 23 Agosti, huku bei ya kuanzia ikiwa ni dola milioni 2.5.

    "Ninaamini bila shaka huu ndio mpira wenye historia kubwa zaidi katika ulimwengu wa soka," Dan Imler, makamu wa rais wa kitengo cha michezo katika Heritage Auctions, aliambia shirika la habari la AFP.

    Alibainisha kuwa huu pia ndio mpira ambao Maradona aliutumia, katika mechi hiyo hiyo, kufunga bao linalojulikana kama "Bao la Karne," ambapo aliwapita kwa chenga walinzi kadhaa wa Uingereza kabla ya kumfunga kipa.

  5. Liverpool kumsajili Araujo wa Barcelona kwa mkopo

    Liverpool iko katika hatua za mwisho za kumsajili beki wa Uruguay, Ronald Araujo, kwa mkopo wa msimu mmoja kutoka Barcelona.

    Makubaliano hayo yanajumuisha kipengele cha kumnunua moja kwa moja Araujo, ambaye anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya siku ya Jumapili.

    Beki huyo wa kati mwenye umri wa miaka 27 ameisaidia Barca kutwaa taji la La Liga katika misimu mitatu kati ya minne iliyopita, na alimaliza msimu uliopita akiwa nahodha wa klabu hiyo.

    Araujo ana mkataba unaoendelea hadi mwaka 2031 lakini alicheza mechi 11 pekee kama mchezaji wa kuanza katika ligi msimu uliopita, huku Gerard Martin na Pau Cubarsi wakionekana kuwa chaguo la kwanza katika safu ya ulinzi ya kati.

    Tangu ajiunge na Barca akitokea klabu ya Boston River ya Uruguay mwaka 2018, Araujo ameichezea klabu hiyo kubwa ya Uhispania zaidi ya mara 200.

    Liverpool ilikuwa ikitafuta kuimarisha safu yake ya ulinzi baada ya Ibrahima Konate kuondoka klabu hiyo na kujiunga na Real Madrid kwa uhamisho huru.

  6. Wahouthi waishambulia tena Marib huku Umoja wa Mataifa ukionya kuwa Yemen inakaribia kukumbwa na mzozo mpana zaidi

    Kundi la Houthi nchini Yemen, ambalo linafungamana na Iran, lilifyatua makombora ya masafa marefu na ndege zisizo na rubani (droni) kuelekea kambi za wakimbizi wa ndani na maeneo ya makazi katika mji wa Marib siku ya Ijumaa, na kusababisha vifo vya watu wawili na majeraha wengine 14, kulingana na ripoti ya shirika la habari la serikali la SABA ikinukuu mamlaka za eneo hilo.

    Jeshi la Yemen lilisema mapema Jumamosi kuwa lilijibu mashambulizi ya vikosi vya Houthi katika maeneo kadhaa kwenye mistari ya mapigano.

    Jeshi hilo halikutoa maelezo ya kina kuhusu operesheni hizo wala kusema ni lini zilifanyika, lakini lilisema litajibu shambulio lolote la baadaye dhidi ya vikosi vyake kwa hatua za kijeshi zinazochukuliwa kuwa muhimu.

    Mapigano haya yanaashiria kuongezeka kwa kasi kwa uhasama kati ya kundi la Houthi na vikosi vya serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa, baada ya miaka kadhaa ambapo mapigano makubwa kati ya pande hizo mbili yalikuwa yamepungua sana, hali inayozua hofu ya kurejea kwa mzozo mpana zaidi.

    Wakati vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran vikipanuka na kuathiri sehemu kubwa ya eneo hilo, afisa mwandamizi wa Saudi Arabia alisema siku ya Alhamisi kuwa Riyadh inatarajia mashambulizi ya pamoja na ya haraka kutoka kwa kundi la Houthi la Yemen pamoja na wanamgambo wa Iraq walio chini ya usimamizi wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu cha Iran..

  7. Infantino akanusha madai kuwa UEFA ilimlipa pesa mwanamke anayedaiwa kuwa 'mpenzi' wake

    Mwanamke anayedaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Gianni Infantino alilipwa malipo ya kuondoka kazini kuhusiana na uhusiano huo na shirikisho la soka barani Ulaya (UEFA) wakati Infantino akiwa katibu mkuu wake, kulingana na uchunguzi wa gazeti la *Daily Telegraph*.

    Msemaji wa Infantino, ambaye sasa ni rais wa FIFA, alinukuliwa akiliambia gazeti hilo kuwa Infantino "anakataa vikali madai haya ambayo si ya kweli hata kidogo".

    UEFA, ambapo Infantino alihudumu kama katibu mkuu kuanzia mwaka 2009 hadi 2016, ilitoa taarifa ikithibitisha kuwa "malipo ya kuondoka kazini yalifanywa kwa mtu huyo husika".

    Madai hayo yanakuja wakati Infantino akipigania hatima yake kama rais wa FIFA kufuatia mipango yake iliyofutwa ya kuuza hisa za Kombe la Dunia kwa wawekezaji binafsi.

    BBC Sport imewasiliana na FIFA pamoja na Infantino ili kupata maoni yao.

    Gazeti la *Telegraph* liliripoti kuwa UEFA ilimlipa mwanamke huyo ambaye anadaiwa kuwa na uhusiano na Infantino (ambaye ameoa), kiasi kikubwa cha fedha wakati Infantino akiwa katika shirikisho hilo linalosimamia soka barani Ulaya.

    "Rais wa FIFA Gianni Infantino anakataa vikali madai haya, na si ya kweli hata kidogo. Dhana yoyote ya mwenendo usiofaa au ukiukwaji wa katiba au kanuni ni ya kuchafua sifa," msemaji wa FIFA aliliambia Telegraph.

    "Hakuna mfanyakazi yeyote katika UEFA au FIFA aliyewahi kuwasilisha malalamiko kuhusu tabia ya Bw. Infantino kwa sababu hakukuwa na tukio lolote ambalo alihusika nalo."

    UEFA ilithibitisha kuwa malipo yalifanywa kwa mwanamke huyo na kwamba yaligharamia masomo yake ya kukamilisha shahada ya uzamili ya biashara (MBA) katika chuo cha biashara cha eneo hilo.

    Ilisema kuwa malipo yote yalizingatia kanuni zilizokuwepo wakati huo, lakini kanuni hizo zimeimarishwa tangu wakati huo na "zinaendana na zile zinazopatikana katika mashirika ya kisasa na yenye hadhi ya juu".

  8. Besigye arejeshwa gerezani Luzira licha ya utata wa hali yake ya kiafya

    Kiongozi wa muda mrefu wa upinzani nchini Uganda, Dk Kizza Besigye, amerudishwa katika gereza la Luzira kutoka Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Mulago, hatua ambayo imezua malalamiko kutoka kwa familia yake na wafuasi wa kisiasa.

    Besigye, ambaye amewahi kugombea urais mara nne, alilazwa hospitalini baada ya kuanguka akiwa mahakamani tarehe 29 Julai wakati akiendelea na kesi yake ya uhaini. Kwa mujibu wa familia yake, bado alikuwa katika hali dhaifu na hakuweza kutembea wala kuzungumza vizuri aliporejeshwa gerezani.

    Kwa mujibu wa Monitor, Mke wake, Winnie Byanyima, amesema madaktari walikuwa na wasiwasi kuhusu hali yake na kwamba maafisa wa magereza walikuwa wameeleza awali kuwa gereza la Luzira halikuwa na uwezo wa kutoa huduma ya afya aliyohitaji. Amesema uamuzi wa kumrudisha gerezani ulifuatia ziara ya Waziri wa Afya, Chris Baryomunsi, hospitalini.

    Hata hivyo, Baryomunsi alisema baada ya kumtembelea Besigye kuwa mwanasiasa huyo alikuwa akiendelea kuimarika na akamtakia apone haraka. Kauli hiyo inapingana na madai ya familia yake na chama chake cha People’s Front for Freedom, ambacho kimetaka aachiliwe na apelekwe nje ya nchi kwa matibabu maalumu.

    Besigye anashikiliwa kwa tuhuma za uhaini na kushindwa kutoa taarifa kuhusu njama ya uhaini, pamoja na washtakiwa wengine wawili. Serikali inamtuhumu kupanga njama ya kuipindua serikali kwa nguvu kati ya mwaka 2023 na Novemba 2024. Kesi yake ilihamishiwa Mahakama Kuu baada ya Mahakama ya Juu kuamua kwamba raia hawapaswi kushtakiwa katika mahakama za kijeshi alikopelekwa awali.

  9. Guimaraes ‘aliililia Arsenal’, hatukutaka aondoke - Newcastle

    Mkurugenzi wa michezo wa Newcastle United, Ross Wilson, amesema klabu hiyo haikupanga kumuuza nahodha wake Bruno Guimaraes, lakini kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28 alitaka kujiunga na Arsenal.

    Mabingwa hao wa Ligi Kuu ya England wanatarajiwa kukamilisha usajili wa Guimaraes kwa ada ya pauni milioni 75, baada ya mazungumzo kati ya klabu hizo kukamilika, ikielezwa na vipimo vya afya ameshafanya.

    Ingawa Wilson amesema ilikuwa "jambo la kukatisha tamaa" kumuona Guimaraes akiondoka, amesisitiza kuwa mchezaji huyo hakutaka tena kuendelea kuichezea Newcastle.

    "Kwa heshima kubwa kwa Bruno kutokana na namna alivyotueleza, na pia kwa hisia nyingi, alituambia wazi kwamba alitaka kuondoka na kuendelea na maisha yake," Wilson alisema.

    Aliongeza kuwa kutaka kwa mchezaji kuondoka hakumaanishi moja kwa moja kwamba klabu itamuuza, lakini hali hiyo ilizingatiwa wakati Newcastle ilipokuwa ikifikiria kiwango cha ada ambacho ingekubali.

    Wilson amesema kumuuza Guimaraes haikuwa sehemu ya mkakati wa Newcastle katika dirisha hili la usajili.

    Guimaraes aliagana na wachezaji wenzake kwa hisia pamoja na wafanyakazi wa Newcastle kabla ya kuondoka kwenye kambi ya maandalizi ya msimu nchini Hispania.

    Ataondoka Newcastle akiwa mchezaji muhimu wa nne kuondoka ndani ya kipindi cha chini ya mwaka mmoja. Sandro Tonali (Tottenham Hotspur) na Anthony Gordon ( Barcelona) wameondoka katika dirisha hili, huku Alexander Isak akijiunga na Liverpool msimu uliopita.

    Kuondoka kwa Guimaraes ni pigo kubwa kwa Newcastle kutokana na nafasi yake kama mmoja wa wachezaji muhimu zaidi wa klabu hiyo.

  10. Rais wa Iran: Kwa nini tupigane ikiwa tunaweza kupata haki zetu kwa mazungumzo?

    Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, ametetea kuendelea kwa mazungumzo na Marekani, akisema Iran inaweza kupata haki zake kupitia diplomasia badala ya kuendelea na vita.

    Akizungumza katika hafla ya kuadhimisha miaka miwili tangu aingie madarakani, Pezeshkian aliuliza: “Kwa nini tupigane ikiwa tunaweza kupata haki zetu kupitia mazungumzo?”

    Hata hivyo, amesema Iran haitarudi nyuma katika misimamo yake, akidai kuwa kuendelea kwa vita ndilo chaguo ambalo Israel inataka ili kuilazimisha Iran kujisalimisha.

    Pezeshkian amesema mazungumzo yaliyopita yalisaidia kumaliza vita nchini Lebanon, kuondoa vizuizi na kupunguza baadhi ya vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Iran.

    Amesema pia Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, amekubali kujiunga na ujumbe wa Iran unaoshiriki katika mazungumzo hayo. Ujumbe huo pia unajumuisha wawakilishi kutoka mahakama, bunge, jeshi na taasisi nyingine za nchi hiyo.

    Kwa mujibu wa Pezeshkian, muundo huo unalenga kuonyesha kwamba “sote tuko upande mmoja” katika mazungumzo hayo.

    Kauli hiyo imekuja wakati mazungumzo kuhusu mustakabali wa Mlango Bahari wa Hormuz yakiendelea kati ya Iran na Oman.

    Afisa mmoja wa Marekani ameiambia Reuters kuwa kumekuwa na maendeleo katika mazungumzo hayo na kwamba Washington inatarajia makubaliano kufikiwa hivi karibuni. Kwa mujibu wa afisa huyo, Marekani inaweza kuondoa kizuizi katika bandari za Iran baada ya makubaliano hayo kutangazwa.

    Pezeshkian pia amekosoa watu anaodai wanazungumza kuhusu masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii bila kuwa na taarifa kamili, akisema kufanya hivyo kunaweza “kuipotosha jamii.”

    Rais huyo amesema Iran pia imefanikiwa kukabiliana na juhudi za wapinzani wake za kuidhoofisha au kuivuruga nchi kupitia shinikizo la kijeshi.