Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mafuriko Pakistan: 'Nilitoa miili kutoka katika maji'
Misaada ya kimataifa imeanza kuwasili Pakistan, lakini mamilioni ya watu ambao wamehamishwa na mafuriko mabaya zaidi katika kumbukumbu za hivi karibuni wanahangaika kupata msaada wowote.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Hina Rabbani Khar, aliita hali hiyo kuwa "mgogoro wa janga."
"Maskini zaidi kati ya watu maskini ambao wana kiwango sifuri cha kaboni wako wanapokea mwisho wa mzozo huu wa hali ya hewa," Khar alisema.
Theluthi moja ya Pakistan iko chini ya maji. Zaidi ya watu elfu moja wamefariki, na mamlaka inasema gharama ya uharibifu uliosababishwa na mafuriko huenda ikafika zaidi ya dola bilioni 10.
BBC imekuwa ikizungumza na wale ambao wamepoteza kila kitu, na wanaojaribu kupata msaada ambao wameathirika zaidi.
'Nilitoa miili kutoka kwa maji'
"Watu wengi wamefarioki katika eneo langu. Mimi, pamoja na watu wengine waliojitolea tulitoa miili zaidi ya 15 kutoka katika maji ya mafuriko", anasema Muhammad Awais Tariq,Kijana wa miaka 20 anayesomea udaktari na anaishi katika mji wa Taunsa Sharif, kilomita 490 kusini-magharibi mwa Islamabad.
Sehemu kubwa ya eneo hilo limemezwa na maji na hiyo ni pamoja na makaburi ya jiji.
"Hakukuwa na ardhi kavu kwenye makaburi. yalikuwa chini ya maji. Kwa hiyo tuliamua kuwazika walifariki nyumbani kwao."
Miili ya baadhi ya waliozama bado haijapatikana. katika moja ya misheni yake ya uokoaji, Tariq alijifunza jinsi ukosefu wa tahadhari kuhusu maji ya mafuriko yanayokuja kunaweza kuwa na matokeo ya kusikitisha.
"Nilimwona mtoto wa miaka mitano akiwa amefunikwa na matope katika kijiji kimoja karibu na mji wetu. Nilifahamu kutoka kwa wenyeji saa chache zilizopita kwamba mafuriko yameharibu mahali hapo, na mvulana huyo alikuwa amenaswa ndani ya maji pamoja na baba yake."
"Baba kwa namna fulani alifanikiwa kumpeleka mtoto kwenye usalama lakini katika harakati hizo alizama," Tariq aliambia BBC.
Wanakijiji waliweza kuuopoa mwili wa baba yake na Tariq aliambiwa mvulana huyo sasa yuko salama na mama yake
"Kuanzia tarehe 10 hadi 22 Agosti, mafuriko yaliingia katika eneo letu. Lakini mvua imesimama kwa sasa, na kiwango cha maji kinapungua", Tariq anafafanua.
Pia anasema watu kutoka vijijini sasa wanamiminika mijini na katika majiji kutafuta hifadhi jambo ambalo linaongeza shinikizo katika maeneo mengine ambayo hayakuathiriwa na mafuriko.
Tariq anasema kwamba nyumba yake ina maji hadi magotini hata sasa, na kwamba watu wengine wengi wanaishi katika nyumba zilizofurika. Lakini baada ya siku saba za kukatika kwa umeme, hatimaye wanashukuru huduma ya umeme sasa imerejea katika kitongoji chake.
'Kufurika kwa ziwa kulisomba nyumba nyingi'
"Angalau vijiji sita vimeathiriwa vibaya na mafuriko. Watu wengi wamepoteza makazi yao. Zaidi ya nyumba mia moja zimesombwa na maji," anasema Peerzada mwenye umri wa miaka 34.
Yeye ni dalali wa nyumba anayeishi katika mji mkuu wa wilaya ya Upper Chitral, Buni, katika mkoa wa milima wa Kyber Pakhtunkhwa.
"Maji ya mafuriko hayakuja Buni, lakini yameharibu vijiji vinavyozunguka," anasema.
"Tulikuwa na mvua kubwa na pia kupasuka kwa ziwa la barafu, ambalo ilisababisha mafuriko makubwa."
Kwa ufahamu wake hakuna aliyefariki Buni au vijiji jirani. Lakini mamia ya watu wameachwa bila makazi, na sasa wanaishi katika mahema.
Peerzada anasema nyumba nyingi zimefunikwa na matope na uchafu mwingine na watu wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji ya kunywa na vitu vingine muhimu.
"Watu wanahitaji masweta na mablanketi ili kupata joto kwani kuna baridi sana. Litashuka chini ya sifuri kuelekea mwisho wa Septemba. Watu hawawezi kuishi kwenye mahema."
"Hatujaathirika kwa hiyo tunatoa msaada"
Mubeen Ansar anatoka wilaya ya Gujrat huko Punjab. Haijaathiriwa na mafuriko, kwa hivyo anafanya awezavyo kusaidia wale wanaohitaji.
"Kwa kweli hakuna mafuriko katika eneo letu. Hakukuwa na mvua nyingi. Sasa tunawaomba watu wetu kuwasaidia wengine walio katika shida."
Mubeen amekuwa akikusanya michango kutoka kwa wakazi 300 wa kijiji chake, Gumti.
"Tunatumia mitandao ya kijamii kuwaomba watu wa kijiji chetu wanaofanya kazi nje ya nchi kuchangia. Pia tunakusanya vifaa vya msaada katika msikiti wetu."
Ansar anasema shehena ya vifaa vya msaada kama vile nguo, blanketi na vyakula kama vile mchele na kunde tayari vimetolewa.
“Tunapanga kununua vyakula vya watoto na bidhaa za usafi kwa wanawake,” anasema.
Pia wameweza kuchangisha takriban $2,000 taslimu kusaidia waathiriwa wa mafuriko.
Ansar na kikundi chake cha wafanyakazi wa kujitolea sasa wanafanya kazi juu ya jinsi bora ya kupata msaada huu kwa vijiji vilivyoathirika zaidi.