Ukraine yasema imevikomboa vijiji 3 katika mashambulizi ya kukabili Urusi

Chanzo cha picha, Reuters
Ukraine imesema kuwa imevikomboa vijiji vitatu kusini-mashariki mwa nchi hiyo katika ushindi wa kwanza wa mashambulizi yake yaliyokuwa yakitarajiwa.
Picha kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha wanajeshi wa Ukraine wakisherehekea katika makazi jirani ya Blahodatne na Neskuchne katika eneo la Donetsk.
Naibu waziri wa ulinzi wa Kyiv alisema eneo la Makarivka karibu pia linakombolewa.
Siku ya Jumamosi, Rais Volodymyr Zelensky alithibitisha kwamba mashambulizi ya kukabiliana na Urusi yameanza.
Makaazi haya matatu yatakuwa ya kwanza kukombolewa tangu kutoa kauli yake, lakini sio ya kwanza kwa Ukraine kutwaa tena tangu Jumatatu, wakati baadhi ya vikosi vyake vilianza kusonga mbele kusini mwa nchi hiyo.
Moscow bado haijathibitisha kuanguka kwa kijiji chochote, badala yake inazungumza juu ya kuzima mashambulizi ya Ukraine katika eneo hilo.
Kwingineko, Ukraine inasema Urusi imelipua bwawa jingine katika eneo la Zaporizhzhia, kufuatia uharibifu wa jengo kuu la Nova Kakhovka siku ya Jumatatu, ambalo lilisababisha mafuriko makubwa.
Ukraine inasema bwawa hilo lililipuliwa na vikosi vya Urusi, ambavyo vimelidhibiti tangu Februari 2022.
Valeriy Shershen, msemaji wa jeshi la Ukraine, alisema vikosi vya Moscow vilichagua kulipua bwawa la pili karibu na kijiji cha Novodarivka, ambalo "lilisababisha mafuriko kwenye kingo zote mbili za mto Mokri Yaly".
Bw Shershen alisema Urusi ilikuwa ikilipua mabwawa kimakusudi katika eneo hilo ili kusimamisha harakati za Ukraine kuelekea maeneo yaliyokaliwa.
Hata hivyo, Urusi imekanusha kulilipua bwawa la Nova Kakhovka na badala yake imeilaumu Ukraine.
Maeneo yakiwa 'Chini ya bendera ya Ukraine tena'
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika picha zilizoshirikishwa na akaunti zinazounga mkono Ukraine kwenye mitandao ya kijamii, wanajeshi wangeweza kuonekana wakiinua bendera ya Ukraine nje ya jengo lililoungua huko Blahodatne.
Na mlinzi wa mpaka wa serikali alichapisha video zinazoonyesha vikosi vya Kyiv vikitangaza kwamba "Eneo la Neskuchne mkoa wa Donetsk liko chini ya bendera ya Ukraine tena", kabla ya kupiga kelele za kusherehekea "Mafanikio kwa Ukraine".
Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Ulinzi Hanna Maliar alidai katika video ya Telegram kwamba vikosi vya Ukraine pia vimechukua kijiji cha Makarivka.
Msemaji wa jeshi alisema mafanikio hayo yalikuwa ushindi wa kwanza wa ndani wa shambulizi hilo la kuikabili Urusi.
Ingawa kukamatwa kwa vijiji hivyo vitatu kunaonyesha maendeleo makubwa zaidi ya siku za hivi karibuni, ukubwa wa makazi hayo ni kidogo.
Blahodatne ilikuwa na wakazi 1,000 tu kabla ya vita.
Kijiji hicho, ambacho kimekuwa kitovu cha mapigano makali katika siku za hivi karibuni, kiko barabarani kuelekea mji wa Mariupol, na baadhi ya wachambuzi wamependekeza kuwa Ukraine inaweza kutaka kuuteka tena mji huo wa bandari katika miezi ijayo.
Wengine wamekisia kwamba Kyiv inataka kuvunja daraja la ardhini kati ya Crimea inayokaliwa na Donetsk, kuwatenga wanajeshi wa Urusi kwenye rasi hiyo.
Mashariki zaidi, wanajeshi wa Ukraine pia wanasemekana kusonga mbele karibu na mji ulioharibiwa wa Bakhmut, eneo lililokumbwa na vita kwa muda mrefu na yenye matukio ya umwagaji damu kati ya vikosi vya Ukraine na wanajeshi wa Urusi.
Maafisa wakuu katika Kyiv wamekataa kutoa maoni yao juu ya maeneo wanaofanya mashambulizo hayo.
Mkuu wa ujasusi wa Ukraine Kyrylo Budanov alitoa video siku ya Jumapili akirudia kauli mbiu ya "mipango ya kupenda ukimya", ambayo inaashiria usiri nyuma ya mashambulizi hayo ya makabiliano.
Kiwango cha operesheni za Ukraine bado hakijabainika, lakini taasisi yenye makao yake makuu nchini Marekani, Taasisi ya Utafiti wa Vita (ISW) ilisema Jumamosi kwamba vikosi vya Ukraine vinashambulia katika angalau maeneo manne ya vita.
Ukraine imekumbana na vikwazo wakati wa kuchunguza ngome za Urusi. Kundi la wanajeshi wa Ukraine waliliambia shirika la habari la AFP kwamba wamepoteza magari kadhaa mapya ya kivita ya Bradley yaliyotengenezwa Marekani katika shambulizi lililotokea kusini mashariki mwa mkoa wa Zaporizhzhia siku ya Alhamisi.
Magari sita kati ya tisa yaliharibika, walisema, na kuongeza kuwa wanahofia kuwa kuna mtu amevujisha taarifa za mipango yao.
Wachambuzi wameangazia ugumu unaokumba Ukraine katika kujaribu kupenya maeneo ambayo Urusi imekuwa ikijiimarisha kwa miezi kadhaa.
Lakini katika maeneo mengine wanajeshi wa Kyiv wanasemekana kutekeleza mashambulizi kwa kutumia vifaa vya kijeshi mwishoni mwa juma, huku vifaru vya Kijerumani vya Leopard-2 vikisemekana kutumwa.
Wakati huo huo katika eneo la Belgorod nchini Urusi, linalopakana na Ukraine, usafiri wa reli ulisitishwa baada ya treni ya mizigo kuacha njia Jumamosi usiku.
Maeneo ya mpakani ya Belgorod yamekumbwa na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani, makombora na mashambulizi ya kuvuka mpaka katika wiki zilizopita.
Kaskazini zaidi, gavana wa eneo la Kaluga, Vladislav Shapsha, alisema kumetokea ajali mbili za ndege zisizo na rubani - moja karibu na kijiji cha Strelkovka na nyingine msituni.
Hata hivyo, BBC haijathibitisha kwa uhuru matukio hayo.















