Kwa nini mashambulizi ya Israel dhidi ya Hezbollah yafanyika sasa

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

"Vita vya maangamizi unayoweza kuyaelezea." Hivi ndivyo Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati alivyoelezea mashambulizi ya Israel dhidi ya nchi yake siku ya Jumatatu ambayo yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 550, wakiwemo watoto 50, na kuwajeruhi wengine zaidi ya 1,200 kusini mwa Lebanon, ambako kundi la wanamgambo wa Kishia la Hezbollah linaendesha harakati zake.

Ilikuwa ni siku mbaya zaidi katika mzozo kati ya Israel na Hezbollah katika miongo kadhaa.

Mashambulizi hayo yalionekana kuwa ishara kwamba Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amedhamiria kutekeleza ahadi yake ya kutafuta "uwiano wa usalama na mamlaka" katika mpaka wa kaskazini wa Israel na Lebanon.

Kwa karibu mwaka mmoja, Israel na Hezbollah zimekuwa zikikabiliwa na mzozo ambao umewalazimisha maelfu ya watu kuishi katika pande zote mbili za mpaka.

Pande zote mbili zinasema hazitaki vita hivyo viendelee, lakini mapambano ya makombora yanaendelea huku kila upande ukirushia makombora upande mwingine.

Tangu wiki iliyopita, hofu imekuwa ikiongezeka kwamba vita kamili vinaweza kuzuka katika Mashariki ya Kati, jambo ambalo linaweza kuyalazimisha mataifa ya kikanda kama vile Iran kuingilia kati kwa mataifa yenye nguvu kubwa kama vile nguvu Marekani.

Ongezeko la hivi karibuni la mashambulizi lilisababishwa na mfululizo wa mashambulizi yanayohusiana na Israel (serikali ya Israeli haijatoa maoni) kwa kutumia maelfu ya vifaa vya mawasiliano vinavyotumiwa na wanachama wa Hezbollah, ambavyo milipuko yake iliua watu 39 na kuwajeruhi maelfu.

"Hali nchini Lebanon ni tete na inatia wasiwasi, na nchi inatumbukia katika mgogoro wa ndani zaidi," Imad Salamey, profesa katika Idara ya Mafunzo ya Siasa na Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Marekani cha Lebanon (LAU), chenye makao yake mjini Beirut, aliiambia BBC Mundo.

Mtaalamu huyo wa kisiasa wa Lebanon anasema kuwa mgogoro wa sasa unamkumbusha vita vya awali kama vile vya mwaka 2006 na 1982, ambavyo pia vilisababisha idadi kubwa ya watu kuyakimbia makazi yao.

"Lakini wakati huu inaonekana kwamba kiwango cha kuhama kwa raia ni kikubwa zaidi wakati huu, Israel inashambulia maeneo makubwa zaidi ya watu," aliendelea.

Zahra Sawli, mwanafunzi kutoka mji wa kusini wa Nabatieh, alilazimika kutoroka nyumbani kwao siku ya Jumatatu.

"Niliamshwa saa 12 asubuhi na sauti ya makombora. Kufikia mchana mashambulizi yalianza kuongezeka na niliona makombora mengi katika eneo langu," alikiambia kipindi cha BBC cha Newshour.

"Tunatakiwa kwenda wapi? Watu wengi bado wamekwama mitaani," aliongeza.

Salamey anaonya kuwa mashambulizi ya Israel yanaitumbukiza Lebanon katika mgogoro mkubwa wa kibinadamu.

"Miundombinu ya kiuchumi na kijamii ya Lebanon, ambayo tayari imedhoofishwa na miaka ya ukosefu wa utulivu wa kisiasa na kiuchumi, sasa imo katika hatari ya kuporomoka zaidi ikiwa mgogoro utaongezeka."

Wakati serikali ya Israeli iko katika machafuko kutokana na vita vyake vikali dhidi ya Hamas huko Gaza, swali linaibuka: kwa nini mashambulizi dhidi ya Hezbollah yanatokea sasa?

Mabadiliko ya mkakati na taarifa muhimu juu ya Hezbollah

Tangu kuanza kwa mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza mwezi Oktoba mwaka jana ilipojibu mashambulizi ya Hamas katika ardhi ya Israel ambayo yalisababisha vifo vya watu 1,200 na mateka 250, hali nchini Lebanon imekuwa ikizorota.

Lakini wiki iliyopita kumekuwa na ukosoaji.

Mwandishi wa habari wa Lebanon Joyce Karam, na mhariri wa tovuti ya Al-Monitor, inayojulikana kwa habari zake za kina za Mashariki ya Kati, anaona kuwa kuna mabadiliko katika mkakati wa kijeshi wa Israeli, ambao unazingatia zaidi mpaka wake wa kaskazini na "kujaribu kutenganisha kile kinachotokea Lebanon " kutoka kwa vita huko Gaza.

"Lakini Hezbollah inakataa na inasisitiza kwamba lazima kuwe na usitishaji mapigano Gaza ili kutuliza hali katika mpaka wa Lebanon," Karam aliiambia BBC Mundo.

Imad Salamey wa Idara ya siasa na mafunzo ya kimataifa katika chuo Kikuu cha Marekani nchini Lebanon anaamini mabadiliko ya kimkakati ya Israeli yanaonyesha lengo pana ambalo ni kudhoofisha ushawishi wa Iran katika eneo hilo.

Lakini sababu kuu inaonekana kuhusishwa na ukweli kwamba jeshi la ulinzi la Israeli (IDF) liliona fursa kubwa ya kuidhoofisha na kuishambulia Hezbollah na ikaitumia kwa faida yake.

"Dalili zote ni kwamba Israel ilikuwa na taarifa muhimu kuhusu msimamo wa Hezbollah, ambazo ziliipa fursa ya kuishambulia kwa usahihi na kuharibu miundombinu yake ya kijeshi," Salamey alisema.

Mashambulizi dhidi ya vifaa vya mawasiliano (hager na simu za upepo), mabomu ambayo yamewaua wanamgambo kadhaa, pamoja na mamia ya raia na mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya miundombinu ya shirika hilo kusini mwa Lebanon ni ushahidi wa mafanikio ya Israel.

Kuhusisha kurudi kwa Walebanon makwao na mashambulizi ya Israel

Tangu kuanza kwa wimbi la hivi karibuni la mashambulizi ya Israel nchini Lebanon, ambayo yamejumuisha mashambulizi ya mabomu katika mji mkuu wa nchi hiyo, Beirut, Benjamin Netanyahu amesema mara kwa mara kwamba kurejea kwa wakazi 60,000 katika makazi yao kaskazini mwa Israel ni lengo la vita.

Netanyahu amesema serikali yake iko tayari kuchukua "hatua zozote muhimu kurejesha usalama."

IDF, kwa upande wake, imeonya kuwa mashambulizi dhidi ya wanamgambo wa Kishia wa Lebanon "yataendelea na kuongezeka."

Kwa Salamey, mashambulizi hayo mapya pia yanaweza kuwa njia mpya ya serikali ya Israel ya kuweka masharti ya kurejea na usalama wa raia wa Lebanon waliohamishwa hivi karibuni wakati wa kurejea kwa Waisraeli kaskazini mwa nchi yao.

Pia inaambatana na kuanza kwa mwaka wa shule nchini Israel, suala ambalo Joyce Karam alisema limeongeza shinikizo kwa serikali ili kuwafanya watu waliohamishwa katika maeneo ya mipakani kurudi nyumbani.

"Fursa" ya wakati

Wengine pia wanafikiri kuwa muda wa mashambulizi ni muhimu kwa Israeli.

"Serikali ya Israel inaweza kuchukua fursa ya wakati huu, wakati umakini wa jumuiya ya kimataifa unalenga mahali pengine, kupunguza nguvu za Hezbollah bila kukabiliwa na uchunguzi mkali ," alisema Imad Salamey.

"Ukweli kwamba Marekani inashughulika na uchaguzi pia ni jambo linaloisaidia Israeli," Karam anaongeza.

Marekani, Uingereza na washirika wengine pamoja na wakosoaji wa Israel wanaamini kwamba njia pekee ya kutuliza hatari hii ni kwa kusitisha mapigano huko Gaza.

Na Hassan Nasrallah, kiongozi wa Hezbollah, ameweka wazi kuwa mashambulizi dhidi ya Israel yataendelea hadi pale makubaliano ya kusitisha mapigano yatakapofikiwa.

Mhariri wa BBC wa kimataifa Jeremy Bowen anaandika kutoka Jerusalem kwamba vita vya Gaza vinaungwa mkono na Waisraeli, lakini Netanyahu bado hajapendwa miongoni mwa wapiga kura.

Uamuzi wake wa kuongeza mashambulizi yake nchini Lebanon ni hatari: Hezbollah bado ina majeshi yenye nguvu ambayo yanaweza kusababisha uharibifu mkubwa.

Shirika hilo pia litaendelea kutegemea msaada wa mfadhili wake mkuu, Iran, rais wa Iran Masoud Pezeshkian alithibitisha Jumatatu.

Itakumbukwa kwamba kundi hilo liliibuka mwanzoni mwa miaka ya 1980 baada ya Israel kulikalia eneo la kusini la Lebanon wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Lebanon. Tangu wakati huo limekuwa ikipokea msaada wa silaha na fedha kutoka Iran.

Kusitisha mapigano au suluhisho la kidiplomasia

Katika kipindi cha wiki moja iliyopita, tumeona Israel ikipanua mashambulizi yake ya anga dhidi ya Hezbollah ili kujumuisha maeneo na hata nyumba ambako inadai kuwa kuna makombora ya masafa marefu.

Siku ya Jumanne, IDF ilifanya mashambulizi mapya ya anga dhidi ya ngome ya Hezbollah kusini mwa Beirut, ambapo kwa mujibu wa ripoti za awali, watu sita waliuawa na wengine 15 kujeruhiwa.

Kwa mashambulizi haya, ambayo anayafafanua kama "ya kuchagua," labda inataka kupunguza nguvu za adui yake.

Lakini Hezbollah pia imeongeza malengo mapya ya mashambulizi nchini Israel, kama vile mji wa Haifa, ambao ni wa tatu kwa ukubwa nchini humo na bandari kubwa ya kibiashara katika bahari ya Mediterania.

Wachambuzi wengi wanakubaliana kuwa vita kamili bado vinaweza kuepukwa, kwani si Iran, Israel wala Hezbollah wanataka kupigana.

Israel inafahamu kuwa kuendeleza vita itamaanisha kuanzisha uvamizi wa ardhini wa gharama kubwa na wa uharibifu kusini mwa Lebanon na matokeo mabaya.

Suluhisho la mgogoro wa sasa litapatikana kwa njia ya diplomasia.

"Israel na Lebanon zinaweza kufikia makubaliano ya kutuliza mvutano kwenye mpaka kwa kuwafukuza wapiganaji wa Hezbollah kutoka Mto Litani, ambao ni muhimu kwa Israeli," anaeleza Joyce Karam.

"Hezbollah inataka usitishaji mapigano huko Gaza haraka, lakini uwezekano wa hilo kutokea unazidi kuwa mdogo."

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Seif Abdalla