Zifahamu nchi 10 zenye bajeti kubwa zaidi Afrika 2025

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 3

Leo, Juni 12, 2025, ni siku muhimu kwa mataifa ya Afrika Mashariki. Tanzania, Rwanda, Kenya, na Uganda yanawasilisha na kupitisha bajeti zao za kitaifa, zikionesha vipaumbele vyao vya kiuchumi na mipango ya maendeleo.

Katika eneo hili, Kenya inasimama kama kinara mkubwa, huku bajeti yake ya 2025/2026 ikiiwa kubwa pengine zaidi ya Uganda na Tanzania zikiunganishwa. Mataifa haya yamepanga kuongeza matumizi kwa jumla ya dola bilioni 5 katika kipindi cha miezi 12 hadi Juni 2026, ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Bajeti ya Uganda inaonekana zaidi kuelekezwa kwenye masuala ya uchaguzi, ikiwa na matumizi makubwa kwenye usalama na utawala, ikionesha vipaumbele tofauti vya kitaifa.

Bajeti ya Tanzania yenyewe haijakuja na miradi mikubwa, imebaki kuendeleza miradi mikubwa ya kimkakati inayoendelea ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR na miundombinu ya barabara, ikiwemo ya mwendo kasi katika jiji la Dar es salaam.

Muelekeo wa bajeti kwa nchi zingine za Afrika ukoje?

Kwa ujumla mataifa ya Afrika yanaendelea kujitahidi kufikia utulivu wa kiuchumi na maendeleo, huku bajeti za kitaifa zikicheza jukumu muhimu katika kuunda sera na vipaumbele.

Bajeti za kitaifa za mwaka 2025 barani Afrika zinaakisi dhamira ya ukuaji wa uchumi, upanuzi wa miundombinu, na maendeleo ya kijamii.

Ugawaji wa bajeti za 2025 unaonesha uwekezaji mkubwa katika miundombinu, huduma za kijamii, na mabadiliko ya kiuchumi kote barani.

Haya ni mataifa 10 Bora barani Afrika kwa bajeti kubwa kitaifa, 2025

1. Afrika Kusini - Dola bilioni 141.4

Afrika Kusini inaongoza kwa bajeti kubwa zaidi barani Afrika kwa mwaka 2025, ikiwa na ugawaji wa kuvutia wa dola bilioni 141.4. Bajeti ya nchi hiyo inaipa kipaumbele miundombinu, huduma za kijamii, na maendeleo ya kiuchumi.

2. Algeria - Dola bilioni 126

Algeria inafuata kwa karibu ikitenga bajeti ya dola bilioni 126, ikionesha uwekezaji mkubwa katika sekta ya nishati na ulinzi.

3. Misri - Dola bilioni 91

Misri inashika nafasi ya tatu kwa dola bilioni 91, ikielekeza fedha kwenye elimu, afya, na miundombinu ya umma.

4. Morocco - Dola Bilioni 73

Morocco pia inaonekana wazi katika orodha hii, ikiwa na bajeti ya kitaifa ya dola bilioni 73.

5. Angola - Dola bilioni 37.847

Angola inashika nafasi ya tano na bajeti ya dola bilioni 37.847, hasa ikichangiwa na mapato yake ya mafuta.

6. Nigeria - Dola bilioni 36.7

Nigeria, taifa lenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika, lina bajeti ya dola bilioni 36.7, likilenga kubadilisha uchumi na miundombinu.

7. Kenya - Dola bilioni 32.65

Kenya inafuata na bajeti ya dola bilioni 32.65, ikipa kipaumbele elimu, afya, na ukuaji wa uchumi. Kama ilivyoelezwa, bajeti hii inazidi kwa mbali zile za majirani zake wa Afrika Mashariki, Uganda na Tanzania.

8. Libya - Dola bilioni 26

Libya, licha ya changamoto za kisiasa, inaendelea kudumisha bajeti ya dola bilioni 26.

9. Ivory Coast - Dola bilioni 25.22

10. Tunisia - Dola bilioni 25.16

Ivory Coast na Tunisia zinamalizia orodha ya mataifa kumi bora, zikiwa na bajeti za dola bilioni 25.22 na dola bilioni 25.16 mtawalia, zote zikilenga kukuza utulivu wa kiuchumi na maendeleo.

Bajeti hizi za kitaifa za 2025 zinasisitiza dhamira ya Afrika katika ukuaji wa uchumi, upanuzi wa miundombinu, na maendeleo ya kijamii. Huku nchi zikikabiliana na changamoto kama vile mfumuko wa bei, usimamizi wa deni, na kuyumba kwa kisiasa, ugawaji huu wa bajeti utakuwa muhimu katika kuunda mandhari ya kiuchumi ya baadaye ya bara hili.

Orodha hii ni kwa mujibu wa Business Insider Africa.