Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwa nini Urusi inajaribu kuisingizia Ukraine kuhusika na mauaji ya tamasha la Moscow?
Ilianza kama kidokezo.Vitisho.Lakini sasa na shutuma za moja kwa moja.
Mamlaka ya Urusi inashikilia kwa ukali kauli kwamba Ukraine na nchi za Magharibi zilipanga mauaji ya mwezi uliopita kwenye jumba la tamasha la jiji la Crocus nje ya mji wa Moscow na kusababisha vifo vya watu 145.
Kundi la Islamic State lilidai haraka kuhusika na shambulio hilo. Lakini mara baada ya watu wanaoshukiwa kuwa na silaha kuzuiliwa, Rais Vladimir Putin aligusia uhusiano wa shambulio hilo na Ukraine.
Mwishoni mwa wiki Kituo cha runinga cha serikali ya Urusi kilitangaza video za mahojiano ya washukiwa hao wanne, raia wote wa Tajikistan.
Mmoja wa watu hao alisema kwenye kanda hiyo kwamba mpango wa baada ya shambulio hilo ulikuwa ni "kuelekea Kyiv".
Maneno yao yanapaswa kuchukuliwa kwa tahadhari kubwa. Wakati wa kufikishwa mahakamani baada ya kukamatwa watu hao walionyesha daalili za kuteswa.
Mwandishi wa televisheni ya Urusi akiwasilisha ripoti hiyo aliendelea kutoa madai kadhaa ya kushangaza:
"Kufuatia shambulio la kigaidi vyanzo vya Magharibi na 'mawakala wa kigeni' wengi wa Urusi walianza kuhamisha mtazamo kutoka kwa uhusiano wa Ukraine na kuuelekeza kwa , Islamic State ."
Nchini Urusi wakosoaji wengi wa Kremlin wanachukuliwa kuwa "mawakala wa kigeni" kwa madai ya kupokea ufadhili kutoka nje ya nchi au tu kuonekana kuwa "chini ya ushawishi wa kigeni".
"Mabadiliko ya mwelekeo wa shutuma " kwa IS halikuwa jambo la kushangaza.
Sio tu kwamba kundi hilo lilitangaza kuwa ndilo lililohusika na shambulio hilo, lilikuwa limetoa video ya shambulio hilo.
Kwa upande wake, Ukraine ilikuwa imekanusha kuhusika kwa njia yoyote na shambulio hilo. Zaidi ya hayo, Marekani na inasemekana, Iran ilikuwa imeonya Moscow juu ya uwezekano wa mashambulizi katika ardhi ya Urusi.
Katika ripoti yake ya dakika 13, Televisheni ya serikali ya Urusi haikutaja madai ya kuhusika kwa IS.
Lakini mwandishi wa habari, alitoa tuhuma hii isiyo na msingi - kwamba vyombo vya habari vya Magharibi "vilikuwa na huruma zaidi kwa wale waliofanya shambulio la kigaidi ambalo liliua zaidi ya watu 140 wasio na ulinzi, kuliko waathiriwa ..."
Lilikuwa ni jaribio la wazi la kuyachafua mataifa ya Magharibi machoni pa umma wa Urusi.
Huu ni 'ukweli mbadala' . BBC haijapokea agizo kama hilo. Mashirika ya kimataifa ya vyombo vya habari yaliripoti kwa upana matokeo mabaya ya ufyatuaji wa risasi na katika Jiji la Crocus.
Kuhusu huruma, wanadiplomasia wengi wa Magharibi walitembelea wizara ya mambo ya nje ya Urusi kutia saini kitabu cha maombolezo na, baadaye, wakaweka maua kwa ajili ya waathiriwa nje ya Jiji la Crocus.
Hilo halijawazuia maafisa wa Urusi kupanga kuilaumu Ukraine na Magharibi.
Alexander Bortnikov, mkuu wa huduma ya usalama ya FSB, aliiambia Televisheni ya Urusi:
"Tunaamini kwamba hatua hiyo ilitayarishwa na Wanamgambo wenye itikadi kali za Kiislamu wenyewe na iliwezeshwa na huduma za kijasusi za Magharibi. Huduma za kijasusi za Ukraine zinahusiana moja kwa moja na hili."
Wiki iliyopita Rais Putin alidai kuwa "Urusi haiwezi kuwa lengo la mashambulizi ya kigaidi ya wafuasi wa itikadi kali za Kiislamu. Sisi ni nchi inayoonyesha mfano wa kipekee wa utangamano wa dini mbalimbali na umoja wa kidini na kijamii'
Hata hivyo ni mwezi uliopita tu ambapo FSB iliripoti kuwa ilikuwa imezuia njama ya IS ya kushambulia sinagogi la Moscow.
Kwa hivyo kwa nini uongozi wa Urusi unaonekana kudhamiria kuihusisha Ukraine na Magharibi kwa mauaji katika Jiji la Crocus?
Hapa kuna baadhi ya sababu zinazowezekana:
Usibadilishe maadui
Tangu uvamizi kamili wa Kremlin dhidi ya Ukraine, Warusi wameongozwa kuamini kwamba maadui wao wakuu ni Ukraine na "Magharibi yote kwa pamoja".
Ni ujumbe ambao mamlaka hapa haiataki kuubadilisha. Baada ya yote, kama umma wa Urusi utaamini kwamba itikadi kali za Kiislamu ni tishio kubwa kwa usalama wao kuliko serikali ya Ukraine au viongozi wa Magharibi, wanaweza kushangaa kwa nini Moscow haijazingatia tishio hilo na imechagua, badala yake, kupigana na Ukraine. .
Kuelekeza macho kwingine
Mwezi uliopita Rais Putin alipuuza hadharani onyo ya ubalozi wa Marekani kwamba shambulio la watu wenye itikadi kali hapa "linakaribia".
Aliitaja tahadhari hiyo ya ugaidi kuwa "yenye hila fulani na yenye nia ya kutisha na kuyumbisha jamii yetu". Shambulio la ukumbi wa tamasha la Crocus City lilifuata siku chache baadaye.
Maafisa wa Marekani baadaye walielezea wazi kwamba taarifa za kijasusi walizoshiriki na mamlaka ya Urusi zilikuwa "kuhusu tukio halisi, za wakati unaofaa na za kuaminika".
Kulaiumu Kyiv na Magharibi linaweza kuwa jaribio la kuvuruga tahadhari kutoka kwa hoja ya habari gani iliyowasilishwa na ni jinsi mamlaka ya Urusi ilivyoifanyia kazi.
Kisingizio cha kuzidisha mzozo
Kudai kwamba Kyiv na Magharibi zilihusishwa na shambulio hilo, kunaipa Moscow kisingizio cha kuzidisha vita vya Ukraine -ikiwa itaamua kuongeza mashambulizi.
Lakini wadadisi wengine wanaionya mamlaka ya Urusi kwamba, kwa mfumo wa kisiasa, kutambua asiyekuwa adui kama hasimu kunaweza kuwa ni kosa kubwa.
"Hivyo ndivyo mfumo wa aina hii kawaida hufa," anaamini mwanasayansi wa kisiasa Vladimir Pastukhov, mshirika mkuu wa utafiti katika Chuo Kikuu cha London.
"Wanazingatia mtu wanayemwona kama adui mkuu na wanamkosa adui halisi mahali pengine. Kwa sasa [mamlaka] itaelekeza nguvu zao kwa Ukraine, Magharibi. Na watafungua mlango wa nyuma. Ni kupitia mlango huu wa nyuma. ambapo hatari halisi itatokea."
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Yusuf Jumah