Visiwa vinavyotoa mishahara mikubwa kuvutia wafanyakazi

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Mshahara mkubwa hutolewa kwa madaktari wanaofanya kazi katika visiwa vya Uist na Benbecula, ambavyo ni sehemu ya visiwa vya Hebrides katika eneo la mbali kabisa la United Kingdom.
Katika kisiwa kingine kiitwacho Rum, kilicho karibu na visiwa hivi, wazazi wanangoja walimu wawafundishe watoto wao. Waalimu watakaoonyesha nia ya kufanya kazi hapa watapewa mshahara wa pauni elfu 68.
Maeneo ya vijijini ya Scotland yanajaribu kuwavutia watu kwa kutoa mishahara ya juu ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa rasilimali watu.
Sehemu muhimu ya ajira hizi ni kuleta watu wapya kuishi na watu wa Visiwa vya Scotland na kuwapatia huduma wanazohitaji.
"Siku zote tunatarajia mtu atakuja," anasema Gordon Jamieson, mtendaji mkuu wa Huduma ya Kitaifa ya Afya ya Visiwa vya Magharibi.
"Tunatoa nafasi za ajira kwa wanandoa wa wataalamu wanaokuja hapa," alisema.
"Hasa kwa wataalamu wa afya, maeneo kama Uist na Benbecula si maarufu sana katika suala la ajira."
"Sio kila mtu anataka kuja katika kisiwa hiki cha mkoa wa Marumala, kuishi na watu na kufanya kazi hapa".

Chanzo cha picha, BENBECULA MEDICAL PRACTICE
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa sababu ya huduma za matibabu ambazo Benbecula inahitaji, Huduma ya Kitaifa ya Afya (NHS) inatoa ziada ya asilimia 40 ya mshahara ili kuwahimiza watu kufanya kazi katika maeneo haya ya mbali.
NHS inawaalika madaktari ambao wana shauku na hamu ya kufanya kazi vijijini kwenda huko. Madaktari wanaokuja hapa wanapaswa kuhudumia watu 4,700 katika visiwa sita.
Bodi ya afya inasema bonasi ni sehemu inayotolewa mbali na mshahara huo. Serikali pia hulipa gharama za usafiri za watahiniwa waliochaguliwa kutoka maeneo yao hadi visiwani.
“Wale wanaotaka kufanya kazi hapa lazima wawe na utu fulani," Jamieson anasema.
"Ndio maana tunawaheshimu watu kama hao. Watu kutoka kote ulimwenguni wanatazamiwa kuja hapa kupata uzoefu wa kutoa huduma za matibabu katika eneo hili," alisema.
Jamieson alisema kuna changamoto nyingi katika uteuzi wa madaktari na wauguzi wanaohitajika kutoa huduma za matibabu visiwani humo.
Alisema kwa sababu ya mishahara hiyo mikubwa, baadhi ya watu wanatarajiwa kubaki hapa na kuanza maisha.
“Tunawataka wanaokuja hapa watoe huduma endelevu na kuishi pamoja na wananchi wa hapa,” alisema.

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Watu 40 pekee wanaishi katika kijiji cha Kinloch kwenye Kisiwa cha Rum. Kuna wanafunzi watano wanasoma katika shule ya msingi katika kisiwa cha Rum. Umri wao ni chini ya miaka mitano hadi 11.
Halmashauri ya Nyanda za Juu inasema watatoa pauni elfu 62 kwa mwalimu mkuu anayekuja kufanya kazi hapa.
Baraza hilo lilisema baadhi ya watu wamejitokeza kufanya kazi. Hata hivyo, ilieleza kuwa mchakato wa kuajiri bado haujakamilika.
Kisiwa cha Rum ni safari ya boti ya dakika 90 kutoka bara. Umeme unazalishwa hapa kupitia miradi ya umeme wa maji.
Kisiwa hicho kina idadi kubwa ya kulungu wekundu. Sehemu kubwa ya ardhi katika kisiwa hicho inamilikiwa na Serikali ya Uskoti. Nyumba nne zilijengwa Kinloch miaka minne iliyopita.
Shirika la Rum's Community Trust linasema, zawadi wanazotoa zitavutia baadhi ya vijana na familia zao kuishi visiwani humo.

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Baada ya kutangaza pauni 53,000 kuajiri mwalimu wa kufundisha watoto 15 katika Shule ya Msingi ya Kilchon walipata maombi mengi.
Ilitangazwa kuwa mwalimu atakayekuja kufanya kazi katika shule ya msingi katika kisiwa kingine kilicho umbali wa maili 16 kutoka kisiwa cha Shetland mwaka 2022 atapewa mshahara wa pauni 62,000 na nyumba ya vyumba vitatu. Watu 28 wanakaa katika kisiwa hiki.
Halmashauri ya Nyanda za Juu inasema wanatoa mishahara na vivutio vingine mbalimbali kuajiri walimu kwa kuzingatia mambo kama vile eneo ilipo shule, idadi ya watu na miundombinu ya kisiwa hicho.
‘Pia inajumuisha gharama za kodi na usafiri,” walisema viongozi wa eneo hilo.
“Tunakaribisha maombi ya kudumu kwa nafasi zinazohitajika visiwani humo. Pia, tumetenga fedha kwa ajili ya kuwafundisha walimu wakuu waliochaguliwa hivi karibuni chini ya mpango wa uongozi wa pamoja. Tutatoa mafunzo sawa na hayo kwa walimu wa shule nyingine pia,” alisema msemaji wa baraza hilo.














