Kwa nini wanaume wa Kihindi wanalalama kwa maumivu ya hedhi?

Hedhi na usumbufu unaokuja nao bado ni mada inayooneka kama mwiko katika sehemu nyingi za India. Lakini kampeni katika jimbo la kusini la Kerala nchini humo inalenga kubadilisha hilo.
Waandaaji wa mpango huo wanapeleka vifaa vya mfano vya kusisimua hedhi kwenye maduka makubwa na vyuo vikuu katika wilaya ya Ernakulam ili kutumiwa na wanaume na kupitia uzoefu wa maumivu ya hedhi wanayopata wanawake. Lengo ni kuhalalisha mazungumzo na mjadala kuhusu mada hiyo.
Video ya hivi majuzi ya kampeni hiyo ilionesha wanaume wakipepesuka na kupiga mayowe kwa maumivu huku wanawake wakitazama, na kuburudika.
"Inaleta uchungu (maumivu) sana. Sitaki kamwe kushuhudia hilo tena," anasema Sharan Nair, mshawishi wa mitandao ya kijamii ambaye alijaribu kutumia vifaa hivyo vya mfano vya kusisimua hedhi kwenye moja ya maduka makubwa.
Vifaa hivyo ni sehemu ya mradi unaoitwa Cup of Life ambao unalenga kusambaza vikombe vya hedhi bure na kupinga dhana potofu kuhusu hedhi.
Umezinduliwa na mbunge wa eneo hilo, Hibi Eden kutoka chama cha Congress pamoja na Indian Medical Association (IMA), ambayo inawakilisha madaktari.

Chanzo cha picha, Cup of Life
Afya ya wanawake, hasa masuala yanayohusiana na hedhi, ni mada ambayo haijajadiliwa sana nchini India. Katika maeneo mengi, wanawake bado wanachukuliwa kuwa wachafu wanapopata hedhi, na kuwekwa mbali na matukio ya kijamii na kidini, na hata jikoni.
Ingawa mtazamo huu umebadilika kidogo katika maeneo ya mijini, wanawake wengi bado hawajisikii vizuri na huru kujadili na waajiri wao au hata wanafamilia wa kiume kuhusu kipindi chao au maumivu makali ambayo wanapitia wakati wa hedhi.
Ingawa baadhi ya makampuni duniani ikiwemo kiasi India wameanza kutoa likizo ya muda kwa wanawake walio katika hedhi, ingawa bado mara nyingi ni mada yenye mgawanyiko.
Lakini waandaaji wa kampeni wana matumaini wanaweza kuibua mabadiliko katika eneo la Kerala, inayochukuliwa kuwa mojawapo ya majimbo yanayoendelea zaidi nchini India.
Vinafanyaje kazi?

Chanzo cha picha, CUP OF LIFE
Vifaa hivyo vya kusisimu vina nyaya mbili ambazo zinaweza kuunganishwa kwa watu wawili kwa wakati mmoja na unapobonyeza namba kubwa kutoka moja mpaka 10 ndivyo inavyoongeza kiwango cha maumivu. Moja kiwango kidogo, 10 kiwango kikubwa.
Bw. Nair anakumbuka kwamba wasichana waliojaribu kuwekewa kifaa hicho "hawakuhisi chochote" huku "wavulana, ikiwa ni pamoja na mimi, tukipiga kelele kwa maumivu makali".
Waandaaji wanasema kuwa simulizi hiyo iliibua mijadala ya uwazi katika vyuo vya wilaya ya Ernakulam.

Chanzo cha picha, CUP OF LIFE
Wazo hili si la kwanza. Mnamo Julai, kampuni moja yenye makao yake nchini Marekani, iliwahi kuhimiza wanaume kutumia vifaa kama hivyo kama zoezi la kujenga huruma dhidi ya wanawake wawapo kwenye hedhi.
Video za Tiktok kutoka kwa matukio haya ya kutumia vifaa hivi tangu wakati huo zimepata mamilioni ya maoni. Bw Eden anasema wazo la kampeni ya wilaya nzima lilikuja baada ya kuanzisha mpango wa kutoa maelfu ya vikombe vya hedhi bure kwa wanawake katika kijiji kiitwacho Kumbalangi.
Mapema mwaka huu, gavana wa Kerala alitangaza kijiji cha kwanza cha Kumbalangi India kisicho na pedi.
Kampeni hiyo iliyoanza miezi minne iliyopita na kuandaa shughuli kadhaa, imekamilika leo kwa usambazaji wa vikombe 100,000 vya hedhi katika harakati za kutengeneza rekodi ya ulimwengu.













