Salman Rushdie aondolewa kwenye mashine ya kupumulia, sasa anaweza kuongea

Chanzo cha picha, Reuters
Mwandishi Salman Rushdie ametolewa kwenye mashine ya kupumulia na anaweza kuzungumza tena, siku moja baada ya kudungwa kisu.
Bw Rushdie, 75, alishambuliwa alipokuwa akizungumza katika tukio moja kwenye jimbo la New York na alikuwa katika hali mbaya.
Amekabiliwa na vitisho vya kuuawa kwa miaka mingi kutokana na kuandika riwaya yake The Satanic Verses, ambayo baadhi ya Waislamu wanaona kuwa ni ya kufuru.
Mwanamume aliyeshtakiwa kwa shambulio la Ijumaa amekana shtaka la kujaribu kuua, na amerejeshwa rumande bila dhamana.
Hadi Matar, 24, anadaiwa kukimbilia jukwaani na kumdunga kisu Bw Rushdie takriban mara 10 usoni, shingoni na tumboni.
Kufuatia shambulio hilo, Bw Wylie alisema mwandishi huyo wa riwaya alikuwa amekatika mishipa ya fahamu katika mkono mmoja, kuharibika kwa ini lake, na kuna uwezekano angepoteza jicho lake pia. Henry Reese, ambaye alipaswa kumhoji Bw Rushdie kwenye hafla hiyo, alipata jeraha dogo kichwani. Yeye ndiye mwanzilishi mwenza wa shirika lisilo la faida ambalo hutoa hifadhi kwa waandishi waliohamishwa kutokana na kupata vitisho mbalimbali.
Kabla ya shambulio hilo, Bw Rushdie alikuwa anakaribia kutoa hotuba kuhusu jinsi ambavyo Marekani imekuwa kimbilio kwa waandishi kama hao.
Mwandishi huyo wa riwaya alilazimishwa kujificha kwa takriban miaka 10 baada ya kitabu The Satanic Verses kuchapishwa mwaka 1988. Waislamu wengi walionyesha hasira zao, wakisema kwamba ni dharau kwa Mtume Muhammad juu ya imani yao.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Alikabiliwa na vitisho vya kuuawa na kiongozi wa wakati huo wa Iran, Ayatollah Ruhollah Khomeini alitoa fatwa , akitaka Rushdie auwawe na kutoa dola $3m kwa mtu ambaye angefanikiwa kumuua.
Mshukiwa aliyemshambulia mwandishi huyo aliyesifiwa siku ya Ijumaa hafahamiki sana.
Bw Matar, kutoka Fairview, New Jersey, alizaliwa Marekani kwa wazazi waliohama kutoka Lebanon, afisa mmoja wa Lebanon ameambia vyombo vya habari.
Uhakiki wa akaunti zake za mitandao ya kijamii umedokeza kwamba anaunga mkono sababu za Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRG), NBC News iliripoti.
Polisi hawajafichua nia yake au kile uchunguzi wa mkoba na vifaa vya elektroniki vilivyopatikana katika kituo hicho unaweza kuwa na matokeo.
Hata hivyo, hakuna uhusiano wowote ambao umeanzishwa kwa uhakika na IRG , kisiasa na kiuchumi lenye uhusiano wa karibu na Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, na viongozi wengine wengi waandamizi.
Bw Rushdie alizaliwa Bombay, India mwaka wa 1947. Alipelekwa katika shule ya bweni nchini Uingereza kabla ya kwenda kusoma historia katika Chuo Kikuu cha Cambridge.
Mnamo 2007, alipewa heshima ya kuwa nguli wa safihi.
Kumekuwa na wingi wa watu wanaomuunga mkono, huku tukio hilo likilaaniwa vikali kama shambulio dhidi ya uhuru wa kujieleza.












