Langya: Watu 35  waambukizwa Virusi vipya mashariki mwa Uchina

ggg

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Virusi vya Langya vimegunduliwa kutoka kwa panya
Iliyochapishwa

Wanasayansi wanafuatilia virusi vipya vinavyotokana na wanyama mashariki mwa China ambavyo vimeambukiza takriban watu kadhaa.

Virusi hivyo vya Langya henipavirus (LayV) vimekutwa kwa wagonjwa 35 katika mikoa ya Shandong na Henan. Wengi walikuwa na dalili kama vile homa, uchovu na kikohozi.

Wanadhaniwa kuambukizwa virusi kutoka kwa wanyama. Hakuna ushahidi hadi sasa kama LayV inaweza kusambaza miongoni mwa binadamu.

Watafiti wamegundua virusi hiyo mara nyingi kwa wanyama aina ya panya

Ugunduzi huo umeangaziwa katika barua iliyoandikwa na watafiti kutoka China, Singapore na Australia na kuchapishwa katika Jarida la afya la New England la mwezi huu.

Mmoja wa watafiti, Wang Linfa kutoka Singapore, aliliambia gazeti la serikali la China Global Times kwamba kesi za LayV zilizopatikana hadi sasa hazijasababisha vifo au athari mbaya sana, kwa hivyo "hakuna haja ya kuogopa".

Hata hivyo, Bw Wang alisema, bado kuna haja ya kuwa macho kwani virusi vingi vilivyopo kimaumbile huwa na matokeo yasiyotabirika vinapoambukiza binadamu.

Wanasayansi walisema LayV ilipatikana kwa 27% kwa wanyama aina ya shrew waliopimwa, na kupendekeza mamalia kama hao wanaweza kuwa na "uhifadhi wa asili" wa virusi. Takriban 5% ya mbwa na 2% ya mbuzi pia walipatikana na ugonjwa huo.

Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Taiwan kilisema Jumapili kuwa "kinazingatia sana" maendeleo ya LayV.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

LayV ni aina ya virusi vya henipa, jamii ya virusi vya zoonotic ambavyo vinaweza kuruka kutoka kwa wanyama hadi kwa wanadamu.

Virusi vya Zoonotic ni vya kawaida sana lakini vimevuta umakini zaidi tangu kuanza kwa janga la Covid.

Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani kilisema wanasayansi wanakadiria kuwa magonjwa matatu kati ya manne mapya au yanayoibuka ya kuambukiza kwa watu hutoka kwa wanyama.

Umoja wa Mataifa hapo awali ulikuwa umeonya kwamba dunia itashuhudia magonjwa mengi kama hayo kutokana na kuongezeka kwa unyonyaji wa wanyamapori na mabadiliko ya hali ya hewa.

Baadhi ya virusi vya zoonotic vinaweza kuwa hatari kwa wanadamu. Hizi ni pamoja na virusi vya Nipah ambavyo vina milipuko ya mara kwa mara kati ya wanyama na wanadamu huko Asia, na virusi vya Hendra ambavyo viligunduliwa kwa mara ya kwanza kwa farasi huko Australia.

Virusi vingine vinavyohusiana na henipa pia vimepatikana kwa panya, popo na sungura.