Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Hakuna wa kuingilia kati' kwa mwanamke aliyehukumiwa kupigwa mawe
Juhudi za kuzuia mwanamke mdogo wa Sudan kupigwa mawe hadi kufa, baada ya kukutwa na hatia ya uzinzi, zinatatizwa na kutokuwepo kwa mawaziri wa serikali nchini humo.
Sudan imekuwa ikiongozwa na jeshi tangu mapinduzi ya mwaka mmoja uliopita.
Wanaharakati wanasema kijana huyo mwenye umri wa miaka 20 hakupata kesi ya haki na anapaswa kuachiliwa.
Afisa wa serikali alikubali kwamba kesi hiyo ilikuwa "mzaha" lakini akaongeza: "Hatuna waziri ambaye anaweza kuingilia kati kutaka aachiliwe."
Mwanamke huyo mdogo, ambaye alitengana na mumewe mnamo 2020 na kwenda kuishi na familia yake, alishtakiwa kwa uzinzi na mumewe mwaka mmoja baadaye. Alipatikana na hatia Juni 2022 na mahakama katika mji wa Kosti, katika jimbo la White Nile nchini Sudan.
Rufaa yake dhidi ya hukumu hiyo sasa imesikilizwa na hukumu ya mahakama inasubiriwa.
Sulaima Ishaq, ambaye anaongoza Kitengo cha Unyanyasaji dhidi ya Wanawake katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, aliambia BBC kwamba amekuwa akiwaambia maafisa katika mji mkuu, Khartoum, kwamba kesi hiyo ilikuwa na dosari, lakini ukosefu wa mawaziri wa serikali ulifanya iwe vigumu kusikiliza upande wake wa kesi .
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema mwanamke huyo, ambaye BBC haikumtaja kwa ombi la familia, hakupewa wakili wakati akiwa kizuizini na hakufahamu mashtaka dhidi yake.
"Tuna sababu za kuamini alilazimishwa kinyume cha sheria kutia saini hati ya kukiri kosa na polisi," anasema Mossaad Mohamed Ali, mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Afrika cha Mafunzo ya Haki na Amani (ACJPS).
Wakili wa mwanamke huyo, Intisar Abdala, aliambia BBC kuwa anatumai kuwa kufuatia rufaa hiyo, mahakama sasa "itafanya jambo sahihi" na kumwachilia mteja wake.
Sudan bado inatoa hukumu ya kifo kwa baadhi ya uhalifu wa hudud - makosa yaliyotajwa na Mwenyezi Mungu katika Quran. Hizi ni pamoja na wizi, uzinzi, na kunywa pombe, na huwa na adhabu kama vile kuchapwa viboko, kukatwa mikono na miguu, kunyongwa na kupigwa mawe.
Ahadi ya serikali mnamo 2015 ya kuondoa kifo kwa kupigwa mawe kama aina ya adhabu haikutekelezwa kamwe, mashirika ya haki za binadamu yanasema.
"Hata wanasiasa wahafidhina zaidi wanapinga kupigwa mawe," Sulaima Ishaq aliambia BBC. "Lakini mambo huchukua muda mwingi kubadilika hapa na kisha kwenda mahakamani, na wanawake ndio wanaoteseka."
Hala Al-Karib, mkurugenzi wa kikanda wa Mpango Mkakati wa Wanawake katika Pembe ya Afrika (Siha), alisema kuwa sheria za uzinzi za Sudan "zilitumika kwa njia isiyo sawa kwa wanawake".
Mtu wa mwisho anayejulikana na wanaharakati kuhukumiwa kifo kwa kupigwa mawe kwa shtaka la uzinzi alikuwa msichana anayeitwa Intisar El Sherif Abdalla. Yeye na mtoto wake wa miezi minne waliachiliwa mnamo 2012 kufuatia kampeni ya Siha na Amnesty International. Lakini Bi Al-Karib alisema huenda kukawa na visa vingine ambavyo havikuwa vimetambuliwa.
"Wanawake na makundi ya haki za binadamu nchini yana rasilimali ndogo na kunaweza kuwa na mamia ya kesi ambazo hatuzijui."
Chini ya serikali ya mpito iliyochukua mamlaka nchini Sudan baada ya uasi dhidi ya Rais Omar al-Bashir mwaka wa 2019, sheria ya "utaratibu wa umma" ambayo ilidhibiti mienendo ya wanawake na mavazi ilifutwa. Hata hivyo, mwandishi wa habari wa Sudan Zeinab Mohammed Salih ameripoti kwamba "polisi wa maadili" waliokuwa wakishika doria mitaani na kutekeleza sheria hii wamerejea kufuatia mapinduzi ya mwaka mmoja uliopita.
Pia kuna ripoti kwamba wafuasi wa Bashir wameajiriwa tena na serikali ya utawala uliyoingia madarakani baada ya mapinduzi.
"Tulikuwa na matumaini kwamba serikali ya mpito ya Sudan ingeanzisha mabadiliko katika mfumo wa sheria wa Sudan, ambao unaendelea kuwafanya wanawake na wasichana kuwa wahalifu waziwazi na kuchangia utii wao na ukosefu wa usawa," alisema Hala Al-Kirab. "Lakini tulikuwa wajinga."
Mnamo 2021, Sudan pia ilitia saini Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Mateso.
"Chini ya Mkataba huo, mateso yanafafanuliwa kama kusababisha mtu kuteseka kwa makusudi na makali," alisema Mossaad Mohamed Ali wa ACJPS. "Kupigwa kwa mawe ni mojawapo ya aina mbaya zaidi za mateso."
Mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa na ya ndani yanayotaka kuachiliwa kwa mwanamke huyo pia yameelezea hukumu ya kupigwa mawe kuwa "ukatili, unyama na udhalilishaji".
Wakili Intisar Abdala ndiye mtu pekee ambaye ameruhusiwa kumtembelea kijana huyo mwenye umri wa miaka 20, ambaye amezuiliwa kwa miezi kadhaa katika gereza la wanawake katika Jimbo la White Nile.
"Mwanamke huyo yuko katika hali nzuri ya kiafya lakini inaeleweka kuwa ana wasiwasi sana. Hakuna mengi zaidi ninaweza kusema kama mwanasheria mwanamke ambaye anaishi na kufanya kazi kusaidia wanawake wengine katika eneo la kihafidhina kama Kosti," alisema.
Aliongeza kuwa msichana huyo alikuwa "msichana wa kawaida na wa kijijini kutoka kwa familia ya kitamaduni, ya kidini, ya kilimo" na kwamba wazazi wake hawakumtelekeza.
"Tunasubiri hukumu kutoka kwa mahakama ya rufaa lakini hakuna anayeweza kusema ni lini hiyo itakuja. Kusubiri ni chaguo letu pekee."
Wale wanaofanya kampeni ya kuachiliwa kwa mwanamke huyo wanasema watakaribisha shinikizo la kimataifa.
"Tuna wasiwasi kwamba mahakama ya rufaa haitatoa uamuzi kwa upande wa mwanamke kijana. Tunawaokoa wanawake kutokana na sheria hizi wakati jumuiya ya kimataifa inapaza sauti yake na kuongeza shinikizo kwa serikali ya Sudan, na hilo lazima litokee tena katika kesi hii," alisema Hala. Al-Karib.
"Huu unaweza kuwa uamuzi wa kushtua ulimwenguni, lakini hautushtui."
BBC ilienda kwa mahakama ya jinai ya Kosti kwa maoni yake, lakini haijapata jibu.
Haikuwezekana kumuuliza Waziri wa Sheria majibu rasmi kwa sababu nafasi hiyo haijajazwa.
Msemaji wa ubalozi wa Sudan mjini London alisema: "Tunafahamu fika kesi hii na kwa kadri tunavyojua, huu sio uamuzi wa mwisho wa mahakama. Tumewasiliana na mamlaka ya haki nchini Sudan kuhusiana na suala hili, na tunasubiri majibu yao. ."