Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Simulizi ya nahodha Mtanzania aliyeokoa raia 5000 vitani Msumbiji
Na Alfred Lasteck
BBC Swahili
Simulizi ya nahodha Mtanzania aliyeokoa raia 5000 vitani Msumbiji
“Tulisikia milio ya risasi, mabomu. baada ya muda mchache umeme ulikatika huku risasi zikiendelea kurindima. Hofu ilitanda miongoni mwa wasaidizi wangu kwenye chombo changu na walinishauri tuondoke. Niliwashauri tuwe na subra ili tuokoe watu,” anasimulia Nahodha Josiah Mwakibuja ambaye aliambatana na timu ya mabaharia 15.
Hiyo ndiyo hali waliyoikuta wakiwa kwenye harakati za kuokoa maelefu ya watu waliokuwa wahanga wa vita vilivyokuwa vikiendelea katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa nchi ya Msumbiji.
Alifikaje Msumbiji?
Mwaka 2021, meli ya Sea Star 1 ikiwa imetia nanga kwenye bandari ya Mombasa nchini Kenya kwaajili ya matengenezo madogo madogo, Nahodha Josiah alipata simu kutoka kwa mmiliki wa chombo hicho, Bashir Haroon akimtaka akashiriki kwenye zoezi la kuokoa watu waliokwamba kwenye Eneo la Palma na kuwapeleka kwenye kambi zilizopo Bandari ya Pemba, nchini Msumbiji.
Nahodha huyo, alitii maelekezo na kwa kile alichodai kuwa alikuwa anaenda kuokoa maisha ya watu. Aliita mabahari na kukutana nao Dar es Salaam na kisha kuanza safari.
Nahodha Josiah anasema, “Niliona ni maisha ya watu, wengi wanapoteza masiha na niliona nina kila sababu ya kuhakikisha ninashiriki kwenye uokozi. Sikuwa na mafunzo ya kijeshi lakini nilitosa chombo Kwenda kuokoa wahanga wa vita kwenye eneo ambalo kwa wakati huo halikuwa na usalama wa kutosha kutokana na mapigano ambayo yalikuwa yakiendelea.”
Nahodha huyo anasema, haikuwa rahisi kushawishi mabaharia aliokuwa akifanya nao kazi, kwanza kuridhia Kwenda kwenye eneo hilo lenye vita. Baadhi walikataa na hivyo kulazimika kutafuta mabaharia wengine na kisha kuanza safari kwenda Msumbiji.
Mapigano yalikuwa kila saa 24
Josiah anasema hali ilikuwa si nzuri, walisikia risasi kila baada ya muda.
Anasema, “Mapigano yalikuwa ni saa 24, kila baada ya muda mfupi asubuhi, mchana na usiku ilikuwa lazima usikie milio ya risasi, hali hiyo binafsi ilianza kunipa hofu lakini tuliamini kwamba tutaweza kusaidia wahanga.
Umeme mitandao ikakatika
“ Tulivyofika na kutia nanga kwenye kina kidogo cha maji, umeme ukakatika wakati mabishano ya risasi yakiendelea, sisi tuliendelea kuwasiliana na mamlaka za Msumbiji kujua tunachukua hatua gani. baada ya siku tatu hali ikiwa bado ni ngumu. Watu wangu waliendelea kuwa na taharuki mawasiliano nayo yakakatika,” anaeleza nahodha huyo.
Anasema hali hiyo, ilifanya watu visiwani Zanzibar na Tanzania kupata hofu kuwa huenda wameuwawa huko lakini baadaye familia zao zilielezwa kuwa wako salama.
Mgomo kwenye meli
Nahodha huyo anasema, alikuwa akifuatwa na mabaharia kwa nyakati tofauti na wakimtaka warudishe chombo Tanzania, wengine wakigoma na kusema kuwa hawawezi kuhatarisha maisha.
Anasema, ”Walinishawishi na mimi niliwashawishi kuwa tunaokoa maisha ya watu. Walikuwa wakipata taarifa za mitandao kwamba hali ilikuwa mbaya. Tuliweka nanga na niliwapa somo moja baada ya mwingine ili kuweka hali nzuri.
COVID 19 ikaongeza taharuki kwa mabaharia
Wakati sasa mamlaka zilipoelekeza watu kuanza kupelekwa kwenye boti, waligundulika kuwa baadhi ya mabaharia walikuwa na COVID 19 na hivyo wakalazimu kuwatenga mabaharia hao.
Anasema, hali ilizidi kuwa ngumu na mabaharia wengi walivunjika moyo, wengi wakiogopa jinsi gani COVID 19 ilivyokuwa hatari.
Baada ya zoezi la upimaji COVID kukamilika, waliweka gati ndogo kwaajili ya operesheni ya haraka ili watu waanze kuingia kwenye meli hiyo.
Operesheni ya uokoaji
Nahodha huyo anasema, walijitahi kuwapa namba wote waliokuwa wanaingia ndani ya meli, kisha kila mmoja alipewa koti
Anasema awamu ya kwanza ya uokoaji walibeba watu takribani 2000. ”Meli yetu ina sehemu ya kuketi abiria 1500, kote kulijaa na ikatulazimu kuweka wengine kwenye eneo linaloweka mizigo…
”…kulikuwa na watoto, wakina mama wajawazito wengi, wazee. Walikuwa na taharuki na walilazimisha kuingia na yote ni kuwa kila mmoja alikuwa anapambania maisha yake,” anasema nahodha huyo ambaye mpaka mwisho wa zoezi alisema kuwa waliokoa watu zaidi ya 5000.
ASHUHUDIA WANAWAKE, WATOTO NA WALEMAVU WAKIUWAWA
Nahodha Josiah katika kitu ambacho hawezi kusahau ni kushuhudia mauwaji ya wanawake, watoto na wenye ulemavu huku wakikosa msaada.
"Kitendo kile kiliniumiza na kunipa nguvu kwamba natakiwa kuwasaidia bila kujali mazingira yaliyopo. Kutokana na mazingira kuwa hafifu nashukuru niliwashawishi wenzangu tuwasaidie wale watu walinisikiliza tukawaokoa wale watu hadi sehemu salama," alisema nahodha huyo.
Mmiliki wa meli aelezea
Mmiliki wa Kampuni ya Zan Ferries inayomiliki Sea Star 1, Bashir Haroon aliiambia BBC, kuwa uamuzi wake wa kupeleka chombo katika eneo hilo, lilijikita kwenye misingi ya ubinadamu na aliamini chombo hicho kilikuwa salama chini ya nahodha mzawa, Josiah.
Haroon alisema, ”Nilipomwambia nahodha kuhusu zoezi la uokoaji Msumbiji licha ya hali kule kuwa tete, aliniambia kuwa yuko tayari kwenda, Serikali ya Tanzania nayo ilikuwa tayari. Sikuona kama napoteza biashara kwa kukitosa chombo cha mamilioni ya dola kwenye hatri. Nilidhamini ubinadamu, utuu na Uafrika.”
Mmiliki huyo anaamini zoezi walilofanya halikuwa tu zoezi kama yalivyo mengine, lilihitaji ujasiri na kuwa sehemu ya kuthamini wazawa ambao walizimama mwanzo mwisho na kufanikisha kuokoa maisha ya watu wa Msumbiji.
Apongezwa kwa ushujaa wake
Akimuelezea nahodha huyo na wenzake, Mwenyekiti wa Bodi ya ZMA, Meja Jenerali, Said Shaaban Omar alisema, nahodha Josiah aliwashawishi wenzake bila kurudi nyuma na kufanikisha uokozi wa watu zaidi ya 5,000 kwa kuwapeleka hadi eneo salama la Pemba ya Msumbiji huku wakiwahudumia mahitaji ya msingi ikiwemo chakula na maji.
"Alihatarisha usalama wake kwani hali ya bahari haikuwa rafiki kuendesha chombo majini," alisema Omar.
Kwa upande wake, Juma Omera, Mkazi Kishiri jijini Mwanza, anampongeza nahodha Josiah na wenzake kwa kile alichodai ni moyo wa kipekee kwani siyo kila mtu ana uthubutu wa kujitoa na kuhatarisha uhai wake kwa ajili ya kunusuru maisha ya mwingine.
Katika hatua nyingine, Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) ziliwatunuku tuzo na zawadi Nahodha Josiah (40) sambamba na baharia, Amour Mussa Juma (39) ikiwa ni ishara ya kutambua ushujaa, umahiri na uzalendo kupitia matukio ya kujitoa mhanga waliyotenda katika kipindi cha mwaka 2021.
Aokoa kwenye matukio 60
Kwa mujibu wa Mamlaka nchini Tanzania, Josiah amehusika katika kufanikisha matukio ya uokozi zaidi ya 60 nchini yaliyotokea kati ya mwaka 2014 hadi 2023 katika bahari ya Hindi.
Katika tukio lingine, Aprili 15 mwaka huu, Josiah ambaye ni nahodha wa meli ya Sea Star 1 inayofanya safari zake kati ya Dar es Salaam, Unguja na Pemba akiwa na meli yake kutoka Pemba kwenda Unguja katika eneo la Mwana wa Mwana alimnasua mvuvi aliyekuwa amezama na kunasa majini huku akiomba msaada.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), Meja Jenerali, Said Shaaban Omar, “Ingawa meli ilikuwa imeshampita lakini nahodha Josiah aliwataarifu abiria katika meli kwamba kuna mvuvi amezama hivyo wasiwe na taharuki. Alimuokoa mvuvi huyo na kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi bandarini na kupokelewa akiwa hai.”
Alitaja tukio la Oktoba 26,2017, baada ya chombo cha Uvuvi cha Nurul Huda kilichokuwa na wavuvi 31 kudaiwa kupotea baada ya bahari kuchafuka ambapo, baharia Amour alijitosa na kuwapata wakiwa wamepoteza uelekeo baharini.