Takribani watu 50 wapoteza maisha katika vijiji karibu na mji wa Mai Mahiu

Iliyochapishwa

Takriban watu 50 wamefariki dunia nchini Kenya baada ya bwawa kuvunja kingo zake kufuatia mvua kubwa na mafuriko, afisa wa shirika la msalaba mwekundu amesema.

Watu katika vijiji karibu na Mai Mahiu, yapata kilomita 60 kutoka mji mkuu, Nairobi, walisombwa na maji walipokuwa wamelala.

Juhudi za uokoaji zinaendelea kuwatoa watu kwenye tope, huku kukiwa na hofu kwamba huenda idadi ya waliofariki ikaongezeka.

Zaidi ya watu 100 wameuawa katika mafuriko ambayo yameharibu sehemu za Kenya katika mwezi uliopita.

Sauti ya kishindo iliwaamsha watu alfajiri ya Jumatatu huku wimbi la maji likitiririka kutoka kwenye bwawa lililopasuka la mto eneo la Mai Mahiu.

Wakazi walizungumza juu ya usiku wa juhudi kubwa za kuwaondoa watu kutoka kwa mafuriko na kuwachimba kutoka kwenye matope.

Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya limejiunga na shughuli za utafutaji na uokoaji, huku meneja wake wa kushughulikia dharura, Anthony Muchiri, akiambia BBC kwamba idadi ya waliofariki imeongezeka hadi 50.

"Hili ndilo janga baya zaidi kuwahi kunipata katika taaluma yangu," alisema, akiongeza kuwa sio tu kwamba nyumba za watu zilisombwa, lakini piasehemu muhimu ya maisha yao.

Kati ya miili iliyopatikana kufikia sasa, 17 ni ya watoto, kamanda wa polisi Stephen Kirui alisema, akinukuliwa na shirika la habari la Reuters.

Vijiji vidogo vya Kamuchiri na Kianugu vilikuwa miongoni mwa vilivyobeba mzigo mkubwa wa maafa hayo.

"Maji yalikuja kwa kasi kutoka Bwawa la Old Kijabe na kusomba nyumba na magari mengi. Hatujawahi kuona mafuriko makubwa kama haya tangu tulipozaliwa hapa Mai Mahiu," David Kamau aliiambia BBC.

Mkazi mwingine, Peter Muhoho, alisema kuwa wengi wa majirani zake walisombwa na maji katika kijiji cha Kianugu chenye takriban nyumba 18.

Serikali imeahirisha kufunguliwa kwa shule kote nchini Kenya huku mvua zaidi ikitarajiwa kunyesha, kulingana na idara ya utabiri wa hali ya anga .

Zaidi ya watu 130,000 wamekimbia makazi yao kutokana na mafuriko hayo, huku watu wengi wakipata hifadhi shuleni.

Mvua kubwa pia imenyesha katika nchi jirani za Tanzania na Burundi.

Takriban watu 155 wameuawa nchini Tanzania tangu Januari.

Nchini Burundi, karibu watu 100,000 wamekimbia makazi yao.

Idadi ya waliopoteza maisha haijulikani, lakini tovuti inayohusishwa na Umoja wa Mataifa inaripoti kuwa watu 68 waliuawa katika mji mkuu, Bujumbura, tarehe 10 Februari pekee baada ya mvua kubwa kuharibu nyumba 3,500.

Mwandishi wa BBC anayeshughulikia utabiri wa hali ya hewa Chris Fawkes anasema kuwa mojawapo ya vichochezi vikubwa vya mvua ni Dipole ya Bahari ya Hindi (IOD).

IOD - ambayo mara nyingi huitwa "Indian Niño" kwa sababu ya kufanana kwake na sehemu yake ya Pasifiki - inaelezea tofauti ya halijoto ya uso wa bahari katika sehemu tofauti za Bahari ya Hindi.

Wakati wa awamu chanya, maji katika Bahari ya Hindi magharibi yana joto zaidi kuliko kawaida na hii inaweza kuleta mvua kubwa bila kujali El Niño.

Hata hivyo, wakati wote IOD chanya na El Niño hutokea kwa wakati mmoja, kama ilivyokuwa mwaka jana, mvua katika Afrika Mashariki inaweza kuwa kali.

Mojawapo ya mifumo chanya ya IOD kwenye rekodi ililingana na mojawapo ya mifumo thabiti zaidi ya El Niño mwaka wa 1997 na 1998, huku mafuriko makubwa yakiripotiwa. Haya yalisababisha vifo zaidi ya 6,000 katika nchi tano katika eneo hilo.