Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi wanaoishi na ulemavu wa kuskia wanavyotambua sauti za mabomu Gaza
- Author, Marwa Gamal
- Nafasi, BBC- Cairo
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Fadel Karaz, mwalimu wa lugha ya alama, anazunguka sehemu mbalimbali za Ukanda wa Gaza ulioharibiwa vibaya na vita, akijitahidi kuwafikia watu wanaoishi na ulemavu wa kusikia.
Safari yake humfikisha katika hema la Iman Shallah, anayejulikana pia kama Umm Mohammed, ambaye anatusimulia kuhusu watoto wake wawili walio na ulemavu wa kuskia kwa kutumia lugha ya alama ambayo Fadel huitafsiri:
"Nina hofu kubwa kwa ajili yao… Iwapo kutatokea shambulio karibu nasi, hawawezi kulisikia na wanaweza kujeruhiwa."
Kwa maneno haya mafupi lakini yenye uzito mkubwa, Umm Mohammed anadhihirisha hali ngumu inayowakabili zaidi ya watu 20,000 wenye ulemavu wa kusikia katika Ukanda wa Gaza, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
Kwa watu hawa, hatari haionyeshi ishara mapema huja kwa ghafla, na huwafanya kuwa kundi lililo hatarini zaidi.
Lakini changamoto ya Umm Mohammed haiko tu kwenye ulemavu wa kusikia.
Amefiwa na mume wake, aliyekuwa mtegemezi mkuu wa familia, pamoja na binti yake.
Sasa, akiwa peke yake kwenye hema la wakimbizi katikati ya jiji la Gaza, analea watoto watatu wawili wao wakiwa na ulemavu wa kuskia.
Anaeleza kwa uchungu hali ya maisha yao:
"Tunachopitia wakati huu wa vita ni kigumu mno. Ninapowaona watoto wangu wakijaribu kutoka nje ya hema, ninajaribu kuwapigia kelele lakini sauti haitoki, kwa sababu nina ulemavu wa kuongea, na wao hawawezi kusikia. Hofu hii ya kila siku inanilazimisha kuwazuia wasitoke, kwa sababu siwezi kuwatahadharisha kuhusu hatari za nje. Na kila mara najiuliza: Nikiruhusu watoke, halafu mashambulizi yatokee, nini kitatokea kwao?"
Fadel Karaz: sikio la watu wanaoishi na ulemavu wa kuskia
Ni kutokana na mateso haya ndipo Fadel Karaz, anayefundisha lugha ya alama kwa miaka 33, aliamua kujitolea kwa njia ya kipekee katika vita.
Anazunguka kambi za wakimbizi, akiwaelimisha watu wanaoishi na ulemavu wa kuskia namna ya kutambua ishara za hatari na mbinu za kujiokoa:
"Uzoefu wangu umenifanya kuwa karibu sana na jamii ya walemavu wa kuskia.
Sasa, nawatembelea kambini kuwaelekeza jinsi ya kutambua wakati mashambulizi yanaendelea kupitia mabadiliko ya tabia ya watu waliowazunguka."
Mbali na kufundisha wenye ulemavu wa kusikia, Fadel pia huwafundisha majirani wa watu hawa misingi ya lugha ya alama, ili waweze kuwasaidia kwa wakati wa dharura. Anafanya haya yote bila malipo:
"Niliamua kuwasaidia Umm Mohammed na watoto wake nilipomwona akihitaji msaada. Alikuwa amepoteza kila kitu, na hii ndiyo wakati ambao anahitaji mkono wa msaada zaidi."
Fadel anatambua kwamba changamoto zinazotokana na vita huenda zaidi ya hatari ya ulipuaji wa bomu moja kwa moja; wanagusa shughuli na mambo ya kimsingi ya maisha ya binadamu.
Fadel anakumbuka tukio lililomgusa sana alipomtembelea Umm Mohammed katika hema lake:
"Siku moja nilipokuwa katika ziara zangu za kutembeela watu wanaoishi na uleavu wa kuskia katika shule iliyogeuzwa kambi nilikutana na Umm Mohamed. Kutokana na joto kali sana, nilimwomba maji. Akanijibu kwa huzuni kuwa yeye na watoto wake hawakuwa na hata tone la maji."
Alipouliza sababu, Umm Mohammed alimweleza kuwa:
"Gari la maji likifika, dereva hupiga honi kuwaamsha watu wachukue maji. Lakini mimi sisikii honi hiyo, hivyo hukosa maji kila mara." asema Fadel.
Fadel anasema hali hii ilimchochea kuanzisha mpango wa kuwafundisha majirani wa familia hiyo lugha ya alama ili waweze kumjulisha Umm Mohammed wakati maji yanapofika.
Pia hujitahidi kumletea maji binafsi mara kwa mara, ingawa hawezi kila siku.
"Suluhisho bora lilikuwa ni kuanzisha mawasiliano kati yake na majirani zake, kwa kutumia lugha ya alama."
Mbali na msaada wa kila siku, Fadel anafundisha mbinu muhimu za kuishi katika mazingira ya vita.
Mohammed Shallah, mtoto wa miaka 12, ambaye anaishi na ulemavu wa kuskia anasema;
"Mwalimu Fadel amenifundisha nisitoke nje nikiona watu wakikimbia wakati wa milipuko. Nisubiri hadi iwe salama. Sijui ingekuwaje kama asingekuwepo."
Ingawa anatambua hatari anazokumbana nazo kila anapotoka, Fadel anasema:
"Kila ninapoelekea kutembelea familia ya wanaoishi na ulemavu wa kusikia, hujiuliza: je, kutakuwa na mashambulizi njiani? Lakini ari ya kweli ya kuwaokoa huzidi hofu yoyote niliyonayo kwani Ukanda wa Gaza ni hatari."Hii ni kulingana na Fadel
"Watoto wanaoishi na ulemavu wa kuskia": Mkono wa kusaidia kutoka chini ya vifusi"
Jitihada za mtu mmoja hazitoshi peke yake.
Fadel Karaz anapata uungwaji mkono kutoka kwa Jumuiya ya Watoto Wetu wanaoishi na ulemavu wa kusikia, shirika pekee linaloendelea kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu wa kusikia katika Ukanda wa Gaza, licha ya makao yake makuu kubomolewa na mashambulizi.
Fadi Abed, mkurugenzi wa shirika hilo, athibitishia BBC;
"Tulilazimika kuhamia eneo jipya ili kuendeleza huduma kwa sababu mahitaji ni makubwa sana. Tulianzisha madarasa ya dharura ndani ya mahema, yaliyotengenezwa na watu wanaoishi na ulemavu.."
Walitengeneza samani, meza na viti kwa ajili ya wanafunzi. Watu waliokuwa wamenyang'anywa kazi zao walipata nafasi ya kuchangia tena, wakawa mfano wa kuigwa wa ujasiri na ubunifu.
Takwimu za kushtua: Mlipuko wa matatizo ya kusikia
Mbali na simulizi hizi za changamoto za watu wanoishi na ulemavu wa kuskia, Fadi Abed anaangazia takwimu za kushtua, kulingana na tafiti za uwanjani zilizofanywa na chama, zikifichua hali mbaya ya kiafya inayoathiri watu wenye matatizo ya kusikia katika Ukanda wa Gaza.
Kwa mujibu wa utafiti wa jumuiya hiyo:
- Zaidi ya 35,000 ya watu huko Gaza sasa wanakabiliwa na matatizo ya kusikia – ya muda au ya kudumu.
- Matatizo yameongezeka mara tatu tangu kuanza kwa vita.
- Asilimia 83% ya watu waliokuwa na vifaa vya kusaidia kusikia wamevipoteza kutokana na kuhama mara kwa mara, ukosefu wa vipuri, au uharibifu.
- Vifaa vipya vimezuiwa kuingia Gaza, licha ya uhitaji mkubwa.
Msururu wa simulizi hizi zinaingiliana ili kuchora picha halisi ya ukweli wa wale walio kimya katika vita vinavyoendelea katika Ukanda wa Gaza: mama Iman, ambaye anajaribu kuwa ngao ya ulinzi kwa watoto wake; mtoto Mohammed, ambaye anakabiliwa na hatari kwa kupenya ufahamu wa kuona; mkufunzi wa lugha ya ishara Fadel, ambaye hupanua madaraja ya mawasiliano kwa mikono yake kwa wote wanaomhitaji; na Fadi, ambaye anaongoza shirika linalojaribu kujenga upya maisha kutokana na vifusi vya vita. Kila mmoja wao, kwa upande wake, na kutoka kwa nafasi yake, anasimulia sura tofauti ya vita, na ushuhuda wa wazi.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid