Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ulimwengu unasemaje kuhusu mdahalo wa urais wa Marekani?
Mdahalo wa kwanza kati ya Kamala Harris na Donald Trump ulifuatiliwa kwa karibu sio tu nchini Marekani bali pia katika mataifa tofauti duniani.
Mjadala huo uliofanyika Philadelphia ulikuwa na mababishano makali kuhusu sera ya kigeni kati ya wagombea hao wawili wa urais.
Kutoka Beijing hadi Budapest, hivi ndivyo mjadala ulivyopokelewa, kulingana na waandishi wa habari wa kigeni wa BBC.
Kutajwa kwa Putin kuliikera Kremlin
Na Steve Rosenberg, Mhariri wa Urusi, Moscow
Kamala Harris alimwambia Donald Trump kwamba Rais Putin ni "dikteta ambaye angemla kama chakula cha mchana."
Maneno "kumla mtu kama chakula cha mchana" (au kifungua kinywa, au chakula kingine chochote) hayapo kwa Kirusi. Lakini jambo moja utakalokuta huko Moscow ni hamu ya matokeo ya uchaguzi wa Marekani ambayo yanainufaisha Urusi.
Ikulu ya Kremlin itakuwa imebainisha (kwa furaha) kwamba katika mjadala huo Trump alikwepa swali la iwapo anataka Ukraine ishinde vita.
"Nataka vita vikome," Trump alijibu.
Kinyume chake, Harris alizungumzia juu ya "ulinzi wa haki" wa Ukraine na kumshutumu Vladimir Putin kwa "kutishia Ulaya yote".
Baadaye Kremlin ilidai kukerwa na kutajwa kwa Putin katika mjadala huo.
"Jina la Putin linatumika kama moja ya zana za vita vya ndani nchini Merekani," msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov aliniambia.
"Hatupendi hili na tunatumai wataliondoa jina la rais wetu katika hili."
Wiki iliyopita Putin alidai kuwa anamuunga mkono Harris katika uchaguzi huo na kusifia "kicheko chake."
Baadaye mtangazaji wa runinga ya serikali ya Urusi alifafanua kwamba Putin alikuwa "mkejeli kidogo" katika maoni yake.
Mtangazaji huyo alipuuzilia mbali ustadi wa kisiasa wa Harris na kupendekeza angekuwa bora zaidi akiandaa kipindi cha mapishi cha TV.
Ninajiuliza: je, kingeangazia “madikteta” wanaokula wagombea urais wa Marekani “kama chakula cha mchana”…?
Mashaka huko Kyiv juu ya maoni ya Trump
Na Nick Beake, Mwandishi wa Ulaya, Kyiv
Kushindwa kwa Donald Trump kutoa jibu, alipoulizwa kwenye jukwaa la mjadala kama alitaka Ukraine kushinda vita, huenda hakujashangaza watu hapa lakini kunaongeza wasiwasi wao juu ya kile ambacho muhula wa pili wa Trump utaamanisha kwao.
Trump kwa muda mrefu amekuwa akijigamba kuwa anaweza kumaliza mzozo huo ndani ya saa 24, matarajio ambayo raia wengi wa Ukraine wanadhani yangemaanisha makubaliano mabaya sana na Kyiv kulazimishwa kuachana na ardhi kubwa ambayo Urusi imenyakua katika miaka miwili na nusu iliyopita.
Kinyume chake, Waukraine watakuwa wameridhishwa na majibu ya Kamala Harris, bila ishara kwamba angetoka kwenye msimamo wa sasa wa uungwaji mkono wa Marekani.
Alijisifia sifa kwa jukumu ambalo tayari amechukua, akisema alishiriki taarifa muhimu za kijasusi na Rais Zelensky kabla ya uvamizi wa Urusi.
Pia alidai msimamo wa Trump ungekuwa mbaya kwa Ukraine ikiwa bado angekuwa katika Ikulu ya White. "Kama Donald Trump angekuwa rais, Putin angekuwa ameketi Kyiv."
Hadharani, mawaziri wa sasa wa Ukraine na wakuu wa majeshi wamekuwa kimya kuhusu mjadala huo. Mapambano ya uchaguzi wa Marekani ni mapambano ambayo hawahitaji kuzingatia huku wakikabiliwa na mapigano ya kweli nyumbani.
Ni Rais Zelensky tu ambaye ameangazia hadharani ushindi wa Trump ungemaanisha nini kwa Waukraine.
Akizungumza na BBC mwezi Julai, alisema itamaanisha "kazi ngumu, lakini sisi ni wachapakazi".
Matamshi ya Trump kuhusu Taliban
Na Lyse Doucet, Mwandishi wa kimataifa
Vita virefu zaidi vya Marekani vilimalizika mnamo Agosti 2021 wakati ilipokimbilia kuwaondoa wanajeshi wake wa mwisho, na kuwahamisha maelfu ya raia, huku Taliban ikiingia Kabul kwa kasi ya kushangaza.
Hatua hiyo iliangaziwa kwenye mjadala na, haishangazi, maswala yalikwepwa, kupuuzwa na kupotoshwa.
Harris aliepuka kujibu swali "je unawajibikia lolote kwa jinsi hatua hiyo ulivyotekelezwa?".
Kama mwandishi ambaye alifuatilia kwa karibu mvutano huo wa machafuko, sikuwahi kusikia kwamba makamu wa rais alikuwepo wakati maamuzi yalipofikiwa katika wiki hizo za mwisho. Lakini aliweka wazi kuwa alikubaliana na uamuzi wa Rais Biden kuondoa wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan.
Trump alijigamba kwamba alizungumza kwa ukali na "Abdul", "mkuu wa Taliban" ambaye bado "ni mkuu wa Taliban."
Alionekana kuashiria Abdul Ghani Baradar, ambaye alitia saini mkataba wa Marekani kijiondoa nchini humo. Lakini hakuwahi kuwaongoza Taliban, na amekuwa nje ya uwanja tangu Taliban ilipochukua hatamu ya uongozi.
Kutajwa kwa ''Abdul'' kulizua wimbi la kejeli mtandaoni huku watu wanaoitwa Abdul wakijipata wakichangia hoja, na wengine wakiuliza "Abdul ni nani?"
Wagombea wote wawili waliangazia mpango mbaya wa Taliban. Ukweli ni kwamba timu ya Trump ilijadili mpango wa kuondoka; timu ya Biden iliidhinisha mpango huo.
Trump alisema mpango huo ulikuwa mzuri kwa sababu "tulikuwa tukitoka".
Hakukuwa na njia nyingine zuri ya kufanya hivyo. Lakini kuondoka kuligeuka kuwa maafa na pande zote zinafaa kulaumiwa.
Harris anawakilisha kutokuwa na uhakika kwa Beijing
Na Laura Bicker, Mwandishi wa China, Beijing
Kamala Harris hajulikani na viongozi hapa na hajajulikana, hata baada ya mjadala.
Hana rekodi yoyote juu China na kwenye jukwaa la mjadala alirudia tutamko lake kwamba Marekani, sio China, ingeshinda shindano hilo kwa Karne ya 21.
Makamu wa rais anawakilisha kitu ambacho China haipendi - kutokuwa na uhakika.
Ndiyo maana Rais Xi hivi majuzi alitumia ziara ya maafisa wa Marekani kutoa wito wa "utulivu" kati ya mataifa hayo mawili yenye nguvu, huenda ulikuwa ujumbe kwa makamu wa rais wa sasa.
Mtazamo uliopo kati ya wasomi wa China ni kwamba hataenda mbali sana na njia ya polepole na thabiti ya kidiplomasia ya Rais Biden.
Lakini kwenye jukwaa la mjadala aliendelea na shambulio hilo na kumshutumu Donald Trump kwa "kuuza teknolojia (chips) za Marekani kwa China ili kuwasaidia kuboresha na kufanya jeshi lao kuwa la kisasa".
Donald Trump ameweka wazi kuwa ana mpango wa kutoza ushuru wa 60% kwa bidhaa za China.
Hii itaongeza ushuru alioweka kama rais ambaye alianzisha vita vya kibiashara mnamo 2018. China ililipiza kisasi, na tafiti nyingi zinaonyesha hatua hiyo ilikuwa na athari za kiuchumi kwa pande zote mbili.
Hili ndilo jambo la mwisho ambalo China inaitaka hivi sasa inapojaribu kutengeneza na kuuza nje bidhaa ili kunusuru uchumi wake.
Kwa viongozi wa China, mjadala huu haukufanya lolote kubadili msimamo kwamba Trump anawakilisha kitu kingine ambacho hawapendi - kutotabirika.
Lakini kwa kweli, kuna matumaini kidogo hapa kwamba sera ya Marekani kuhusu China itabadilika kwa kiasi kikubwa, bila kujali ni nani anayeingia Ikulu ya White House.
Kinyang'anyiro cha Ikulu ya Marekani kilifuatiliwa kwa makini Mashariki ya Kati
Na Paul Adams, Mwandishi wa kimataifa, Jerusalem
Hapa Mashariki ya Kati, kinyang'anyiro cha kuwania Ikulu ya Marekani kinafuatiliwa sana.
Huku vita vya Gaza vikiendelea na makubaliano ya kusitisha mapigano ikiwa bado hayajapatikana, baadhi ya wakosoaji wa Benjamin Netanyahu wanashuku kuwa waziri mkuu wa Israel anajivuta kimakusudi hadi baada ya uchaguzi, kwa matumaini kwamba Trump atakuwa na huruma zaidi kwa Israel kuliko Harris.
Kuna mvuto wa historia labda inakaribia kujirudia.
Mnamo 1980, timu ya kampeni ya Ronald Reagan ilishukiwa kuitaka Iran isiwaachilie mateka wa Kimarekani walioshikiliwa Tehran hadi baada ya kumshinda Rais Jimmy Carter, akisema Reagan angeipa Iran makubaliano bora.
Je, kitu kama hicho kinaweza kutokea sasa? Kwa hakika wapinzani wa Netanyahu wanaamini kuwa yeye sasa ndiye kikwazo kikuu cha mpango wa kusitisha mapigano.
Harris amedokeza kuwa anaweza kuwa mkali zaidi kwa Israeli kuliko Joe Biden, jambo ambalo Trump ameshikilia, akisema jana usiku kwamba makamu wa rais "anachukia Israeli".
Wapalestina, wenye mashaka makubwa juu ya Donald Trump lakini wamesikitishwa na kutokuwa na uwezo wa serikali ya Biden kusitisha vita huko Gaza, labda wana mwelekeo wa kumuona Harris kama mdogo kati ya maovu mawili.
Kwa muda mrefu wameachana na dhana yoyote ya Marekani kama wakala mwaminifu katika Mashariki ya Kati, lakini watakuwa wamegundua kwamba Harris, tofauti na Trump, anasema amejitolea kwa serikali ya Palestina.
kusifiwa kwa Orban kwapokelewa kwa msisimko Hungary
Na Nick Thorpe, Mwandisi wa Ulaya ya Kati, Budapest
Donald Trump alimmiminia sifa waziri mkuu wa Hungary.
"Viktor Orban, mmoja wa wanaume wanaoheshimiwa sana, wanamuita mtu mwenye nguvu. Ni mtu Smart..."
Vyombo vya habari vinavyounga mkono serikali ya Hungary viliangazia pongezi hizo. "Utambuzi mkubwa!" aliandika kichwa cha habari huko Magyar Nemzet.
Lakini tovuti ya habari muhimu ya serikali 444 ilimnukuu Tim Walz, mgombea mwenza wa Harris.
"Yeye [Trump] aliulizwa kutaja kiongozi mmoja wa ulimwengu ambaye alikuwa pamoja naye, na alisema Orban. Hayo ndiyo tu tunayohitaji kujua.
Viktor Orban alimuunga mkono Trump kuwa rais mnamo 2016 na anamuunga mkono tena katika uchaguzi huu wa Novemba.
Wawili hao walikutana kwa mara ya pili mwaka huu nyumbani kwa Trump huko Florida mnamo Julai 12, baada ya Orban kutembelea Kyiv, Moscow na Beijing mtawalia.
Serikali ya Orban inaunga mkono ushindi wa Trump na uwezo wake wa kumaliza vita vya Ukraine haraka.
"Mambo yanabadilika. Ikiwa Trump atarudi, kutakuwa na amaniHilo litafikiwa bila mchango wa Ulaya," Balazs Orban, mkurugenzi wa kisiasa wa Viktor Orban, aliiambia BBC mnamo Julai.
Maelezo zaidi kuhusu uchaguzi wa Marekani
- Muongozo: Yote unayostahili kujua kuhusu kura ya urais
- Uchambuzi: Wajue wagombea wa urais Marekani waliogombea wakiwa gerezani
- Maelezo: 'Je, ni Mwafrika au Mhindi?': Trump ahoji utambulisho wa rangi wa Harris
- Maelezo: Je, sera za Trump na Harris zitakuwaje kuhusu Mashariki ya Kati?
- Soma zaidi kuhusu: Kamala Harris | Donald Trump | Uchaguzi Marekani
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi