Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kiongozi wa kijeshi wa Madagascar aapishwa kuwa rais
- Author, Sammy Awami
- Nafasi, BBC Africa
- Akiripoti kutoka, Antananarivo
- Author, Omega Rakotomalala
- Nafasi, BBC Monitoring
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Kanali Michael Randrianirina ameapishwa kuwa Rais mpya wa Madagascar katika Mahakama ya Katiba Kuu jijini Antananarivo.
Anamrithi Andry Rajoelina, rais wa zamani aliyeikimbia nchi na baadaye kuondolewa madarakani kufuatia maandamano ya kudai uwajibikaji zaidi.
Katika hotuba yake ya kuapishwa, Randrianirina aliahidi kutekeleza majukumu yake kwa haki na kujitolea kuilinda umoja wa kitaifa na haki za binadamu.
"Nitatekeleza kikamilifu, kwa ukamilifu na kwa haki majukumu makuu ya wadhifa wangu kama Rais wa Jamhuri ya Madagascar," alisema Randrianirina katika hafla ya kuapishwa katika Mahakama ya Katiba Kuu.
"Ninaapa kwamba nitaitumia mamlaka niliyopewa kwa uadilifu na kujitolea kwa nguvu zangu zote kulinda na kuimarisha umoja wa kitaifa na haki za binadamu," aliongeza.
Alitangaza kuwa jeshi limechukua madaraka, kuvunja taasisi zote isipokuwa Bunge la Taifa, na kwamba serikali ya mpito itaongoza hadi miaka miwili kabla ya uchaguzi mpya.
Haya yanajiri baada ya Umoja wa Afrika kutangaza vikwazo dhidi ya Madagscra wakieleza ukiukaji wa kikatiba.
Rais wa Mahakama ya Katiba Florent Rakotoarisoa ameikosoa jumuiya ya kimataifa kwa kuelezea hali ya Madagascar kuwa ni mapinduzi.
Alisema kuwa hakuna ukiukwaji wa katiba nchini Madagascar, badala yake analaumu katiba kwa kusababisha hali kuwa mbaya.
Vipaumbele vya Randrianirina
Rais mpya wa Madagascar, Kanali Michael Randrianirina, ametaja vipaumbele vyake, ambavyo ni pamoja na kuhakikisha usalama wa chakula na kuanzisha uchunguzi katika kampuni ya serikali ya maji na umeme, Jirama, ili kutatua changamoto zinazoendelea ndani ya shirika hilo.
Kanali Randrianirina alizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kuapishwa nje ya Mahakama Kuu ya Kikatiba jijini Antananarivo.
Rais alisisitiza kuwa mojawapo ya vipaumbele vyake kuu ni kuchunguza Jirama na kutatua masuala yanayoendelea kuathiri kampuni hiyo ya maji.
"Leo na kesho, tutachunguza hali ya Jirama-ni nini kinafanyika huko na matatizo gani yaliyopo sasa. Tathmini hii inalenga kuzuia matatizo ya siku zijazo. Hicho ndicho kipaumbele chetu cha kwanza cha kijamii.
Kipaumbele cha pili ni kilimo cha mpunga. Tunapoingia msimu wa kilimo, lazima tutathmini namna bora ya kuendelea.
Kipaumbele cha tatu ni uteuzi wa waziri mkuu na uundaji wa serikali.
Hivi ndivyo vipaumbele vyetu vikuu kwa sasa," alisema.
Kanali Randrianirina anamrithi Rais wa zamani Andry Rajoelina, ambaye aliikimbia nchi na baadaye kuondolewa madarakani kufuatia wiki kadhaa za maandamano ya kudai uwajibikaji zaidi kutoka kwa serikali yake.
Waandamanaji walikuwa na matumaini kwamba Rajoelina angejiuzulu na ili kutoa nafasi ya mabadiliko ya kidemokrasia.
Badala yake, aling'ang'ania madaraka, akiivunja serikali yake na kufanya mijadala mingi na makundi mbalimbali ya watu, juhudi ambazo hazikutosha kuwatuliza waandamanaji.
Maandamano hayo, yaliyoanza mwezi uliopita, yaliandaliwa na vuguvugu la vijana linalojulikana kama Gen Z - lililokasirishwa na ukosefu wa umeme na maji.
Kanali Randrianirina alikuwa mkuu wa kitengo cha jeshi cha Madagascar cha CAPSAT, wakati siku ya Jumanne wanajeshi wake walijiunga na maelfu ya waandamanaji kwenye mitaa ya mji mkuu.
Aliwaambia waandamanaji wa Gen Z kwamba anachukua mamlaka na kwamba jeshi litaunda serikali na kufanya uchaguzi ndani ya miaka miwili.
Watetezi wa demokrasia, ndani na nje ya nchi, wanatumai kuwa ahadi hii itatekelezwa.
Kabla ya kuapishwa kwa Ijumaa, aliongeza kuwa kufanya mageuzi katika tume ya uchaguzi na kusafisha orodha ya wapiga kura ni muhimu kabla ya uchaguzi mpya kufanyika, kulingana na tovuti ya habari ya L'Express de Madagascar.