Cameroon waibuka washindi wa kombe la WAFCON 2026

    • Author, Rob Stevens
    • Nafasi, BBC Sport Africa
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Cameroon ilipata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Malawi, timu iliyokuwa ikishiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza, na kutwaa taji lao la kwanza kabisa la Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (Wafcon).

Goli la kichwa kutoka kwa Marie Ngah Manga liliipa timu ya 'Indomitable Lionesses' uongozi katika dakika ya 20, na Naomi Eto akaongeza bao la pili kwa shuti kali la volei dakika ya 30 jijini Rabat, Morocco.

Timu hiyo kutoka Afrika ya Kati ilifunga bao la tatu katika dakika ya tatu ya muda wa nyongeza wa kipindi cha kwanza, ambapo Eto alimzunguka kipa wa Malawi, Mercy Sikelo, na kumpa pasi safi mshambuliaji Ngah Manga ili afunge bao lake la tano katika michuano hiyo.

Malawi, timu iliyokuwa na nafasi ya chini zaidi duniani (ya 153) miongoni mwa washiriki wa Wafcon 2026, ilifika fainali kutokana na uwezo mkubwa wa kushambulia wa dada wawili, Tabitha na Temwa Chawinga.

Hata hivyo, nyota hao wawili wa timu ya 'Scorchers' walidhibitiwa vyema na safu ya ulinzi ya Cameroon, ambayo ilihakikisha kuwa timu hiyo kutoka Kusini mwa Afrika haitimizi ndoto yake ya safari ya kushangaza kwenye michuano hiyo.

Ngah Manga alipoteza nafasi nzuri ya kufunga mabao matatu, na kujihakikishia tuzo ya kiatu cha dhahabu peke yake,dakika tatu baada ya kipindi cha pili kuanza, alipompita kipa Sikelo lakini akapiga shuti nje akiwa umbali wa yadi sita huku lango likiwa wazi.

Timu ya 'Scorchers' ilipata nafasi yake bora zaidi muda mfupi baada ya dakika ya 60, ambapo kipa wa Cameroon, Michaely Bihina, aliokoa shuti la chini la Tabitha Chawinga kabla ya mdogo wake kugeuka na kupiga nje mpira uliorudi uwanjani.

Mafanikio ya Cameroon yanavutia zaidi ikizingatiwa kuwa timu hiyo, inayofahamika kama 'Indomitable Lionesses', ilikosa michuano ya Wafcon ya mwaka 2024 na kushindwa kufuzu kwa fainali hizo baada ya kupoteza kwa jumla ya mabao 3-1 dhidi ya Algeria katika raundi ya pili ya mchujo.

Hata hivyo, timu hiyo kutoka Afrika ya Kati ilifanikiwa kuingia kwenye michuano hiyo kutokana na nafasi yake katika viwango vya dunia, baada ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kuongeza idadi ya timu shiriki katika fainali hizo kutoka 12 hadi 16.

Rais wa FIFA, Gianni Infantino, alikuwepo kukabidhi kombe hilo akishirikiana na mwenzake wa CAF, Patrice Motsepe, na Cameroon,ambayo hapo awali ilishapoteza fainali tatu za Wafcon,ilijipatia pia kitita cha dola milioni 2 (pauni milioni 1.48) kama zawadi ya ushindi, huku ikiwa timu ya nne tu kutwaa taji hilo baada ya Nigeria, Equatorial Guinea na Afrika Kusini.

Timu zote mbili zitashiriki Kombe la Dunia la Wanawake la FIFA la mwaka 2027 nchini Brazil, zikiungana na timu nyingine zilizofika nusu fainali ya Wafcon, Algeria na Morocco.

"Tunafurahi sana," alisema Ngah Manga kupitia kituo cha E4.

"Tumefanya kazi kwa bidii kubwa kwa miaka yote hii ili kufika hapa. Tunajivunia sana hatimaye kuwa mabingwa."

Indomitable Lionesses watumia fursa ya makosa yaliofanywa na upinzani

Timu zote mbili zilionekana kuwa na wasiwasi katika dakika za awali, huku timu hiyo ya Kusini mwa Afrika ikijaribu mara kwa mara kumfikishia mipira ya mbele Temwa Chawinga, mbinu iliyofanya kazi vizuri katika ushindi wao wa nusu fainali dhidi ya Algeria.

Goli la ufunguzi lilipatikana baada ya Sikelo kukosea kukadiria mpira wa krosi uliopigwa na Eto kutoka upande wa kulia, na mpira wa kichwa wa Grace Mendoua kuelekea upande wa pili wa lango ulipoguswa na kipa wa Malawi na kugonga mwamba wa juu.

Ngah Manga alikuwa tayari kuuwahi mpira huo uliorudi uwanjani kutoka umbali wa mita mbili na kuufunga, Cameroon, ambao wako nafasi 82 ​​juu ya wapinzani wao katika viwango vya ubora, hawakuangalia nyuma tena.

Timu ya 'Indomitable Lionesses' iliongeza bao la pili wakati Malawi iliposhindwa kuondoa mpira wa kona, na Eto alijizungusha kabla ya kupiga shuti la moja kwa moja lililoingia kona ya chini upande wa kulia.

Sikelo anaweza kulaumiwa kwa bao la tatu kwani aliamua kutoka golini kwake kujaribu kuuwahi mpira uliopigwa na Genevieve Ngo Mbeleck, lakini Eto alimuwahi, akafika pembeni mwa uwanja na kupiga krosi ambayo Ngah Manga aliifunga kwa kichwa kwenye wavu wazi kutoka umbali wa mita mbili.

Valentine Nguele alianza kuifundisha Cameroon mwezi Juni lakini ameunda timu imara iliyoishangaza Nigeria kwa kuifunga 1-0 katika robo fainali na kisha kuifunga mwenyeji Morocco kwa mikwaju ya penalti katika nusu fainali.

Bihina alikuwa nyota katika mechi hizo zote mbili, akifanya kazi nzuri ya kuokoa michomo tisa dhidi ya 'Super Falcons' na kisha kudaka penalti katika muda wa ziada pamoja na mikwaju mingine mitatu katika hatua ya mikwaju ya penalti dhidi ya timu hiyo ya Afrika Kaskazini.

Kipa huyo wa Benfica mwenye umri wa miaka 22 hakuhitajika sana kufanya kazi kubwa katika fainali hiyo kwani upinzani wa Malawi ulianza kupungua.

Cameroon walikaribia kuongeza bao la nne mwishoni mwa mchezo, lakini shuti la Eto kutoka pembeni lilidakwa vizuri na Sikelo, kabla ya Mendoua kupiga kichwa kutokana na kona kuelekea upande wa pili wa lango lakini mpira ukatoka nje.

Katika muda wa majeruhi, mchezaji wa akiba wa 'Indomitable Lionesses', Gabrielle Onguene, aliingiza mpira wavuni lakini bao hilo lilikataliwa kwa sababu ya sheria ya kuotea, na akaonyeshwa kadi kwa kuvua jezi yake wakati akishangilia. Rais wa Shirikisho la Soka la Cameroon, Samuel Eto'o, alishangilia kwa bashasha kubwa kila bao akiwa jukwaani katika Uwanja wa Moulay Hassan, huku benchi la ufundi na maafisa wa timu hiyo wakikimbilia uwanjani mara baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa ili kusherehekea taji lao la kwanza la WAFCON, baada ya kupoteza fainali za miaka ya 2004, 2014 na 2016, ambazo zote walifungwa na Nigeria.

Uamuzi wa kupanua fainali umethibitishwa kuwa sahihi

Kabla ya fainali, mashindano haya yalifafanuliwa kwangu kama 'Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake la enzi yetu', na kwa hakika yalikuwa hivyo.

Mbali na nchi mwenyeji Morocco, hakuna ambaye angeweza kutabiri timu hizo nne za mwisho au timu mbili ambazo hatimaye zingetinga fainali.

Uamuzi wa CAF wa kupanua mashindano hayo na kujumuisha mataifa 16 umeonekana kuwa sahihi, ukizipa fursa timu nyingine,tofauti na vigogo kama Nigeria na Afrika Kusini,kuonyesha uwezo wao na kupunguza pengo la kiwango kati yao na timu bora zaidi barani humo.

Hatimaye, kizazi hiki kipya cha wachezaji wa Cameroon kilionyesha ubora wa hali ya juu dhidi ya Malawi, Monique Ngock aling'aa tena katika eneo la kiungo na kuzuia pasi zilizoelekezwa kwa kina dada Chawinga,pasi ambazo zilikuwa na matokeo makubwa katika safari yao kuelekea fainali.

Uwezo wa Michaely Bihina wa kudaka mipira pia ulikuwa kivutio kikubwa cha mashindano haya, huku ndoto ya timu hiyo, iliyoshika nafasi ya 153 duniani, ikifikia tamati ya ghafla kutokana na udhaifu katika safu ya ulinzi ulioambatana na wasiwasi.

Hata hivyo, timu zote mbili zina kibarua cha kujiandaa kwa Kombe la Dunia la Wanawake mwakani, zikiungana na Morocco pamoja na Algeria, ambayo itashiriki kwa mara ya kwanza sambamba na Malawi.

Timu ya 'Fennecs' ya Farid Benstiti inaweza kusemwa kuwa imepiga hatua kubwa zaidi ya maendeleo tangu mashindano ya Wafcon yaliyopita miezi 13 iliyopita, na kuna matarajio makubwa kwa timu hizo nne za Afrika zitakazoshiriki michuano hiyo nchini Brazil mwakani.