Uchaguzi Kenya 2022: Changamoto za wanasiasa wa kike wa mjini zinatofautiana na zile za wanasiasa wa vijijini?

Iliyochapishwa

Na Aboubakar Famau

BBC Swahili

Heka heka za uchaguzi zinaonekana kupamba moto nchini Kenya, wakati taifa hilo likijiandaa kuelekea katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mnamo tarehe 9 mwezi Agosti.

Kama ilivyo kwa mataifa mengine katika kipindi kama hiki, wanasiasa wamekua wakiusubiri muda huu kwa udi na uvumba ili wakutane na wafuasi wao na kunadi sera zao kwa lengo la kuvutia wapiga kura.

Ni katika hatua hii ambapo, baadhi ya wanasiasa hutumia kila njia wawezayo ambayo wanahisi itawaletea kura.

Baadhi huamua kutumia njia ambazo hazikubaliki, ikiwemo matusi dhidi ya wapinzani wao pindi wanapokuwa kwenye majukwaa ya kampeni na wengine hata rushwa.

Kwa kawaida, hali hii ina athari kwa makundi yote, ikiwemo wanawake na wanaume, lakini ni dhahiri kwamba, mara nyingi, wanasiasa wanawake kwa muda mrefu ndio wamekuwa waathirika wakubwa, hasa pale matusi yanapoelekezwa dhidi yao kupitia mitandao ya kijamii au majukwaa ya kisiasa.

Wachambuzi wa mambo, wamekuwa wakihusisha hali hii na ushiriki mdogo wa kina mama katika siasa.

Hata hivyo, katika hali isiyo ya kawaida, kampeni za uchaguzi wa mwaka huu, zinaonekana kuwa tofauti na zile za chaguzi zilizopita.  Na hii inatokana na jinsi idadi kubwa ya wanawake waliojitokeza na kuingia katika ulingo wa kisiasa.

Vyama vitatu vya kisiasa tayari vina wagombea wenza wa kike, huku hamasa kubwa pia ikionekana katika nafasi nyengine za uongozi kama vile za magavana na maseneta.

Wanaharakati wanafurahishwa

Baadhi ya wanaharakati nchini humo wanayaona haya kama ni matunda ya jitihada zilizofanyika za kuwajengea uwezo wanawake.

Daisy Amdany ambae ni mkurugenzi mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la CROWN TRUST anasema mwamko umekuwa mkubwa kutokana na jitihada ya miongo miwili dhidi ya unyanyapa kwa wanawake kwenye siasa.

Hatua ambayo imesababisha mabadiliko katika katiba Kenya kuhakikisha idadi ya wanawake imetiliwa maanani zaidi katika nafasi za ajira na uongozi na kuimarisha uwezo wa kina mama.

“Kuna mwamko tena mkubwa sana, kwa sababu hapo mwanzoni vyama vingi, hata wakati wanawake walikuwa wanajitosa, vyama vingi havikuwa vinawahusisha wanawake, ulikuwa unaona wakati wakiteua, wanawake wengi walikuwa wanaangushwa na hawafiki katika hatua ya kupigiwa kura, lakini tuko na wanawake wengi wameingia katika kinyang’anyiro, na hivi vyama vikubwa vimeweka kina mama.

Hii imechangiwa na kuendelea na harakati zetu za kusukuma sheria iweze kutekelezwa vilivyo, kwa sababu tunajua kwamba katiba yetu iko na kipengele ambacho inasema katika kila sehemu ya uongozi, hapawezi kuwa na zaidi ya thuluthi mbili ya jinsia moja,”anasema Daisy.

 

Kwa muda mrefu, kumekuwa na dhana kwamba, wanawake wanasiasa wa vijijini pekee ndio wanaokabiliwa na changamoto, huku ikifikiriwa kwamba wale waliopo mijini wana afueni. Lakini changamoto zinazowakabili wanasiasa wanawake vijijini hazitofautiani na wanawake wa mijini.

Uwezo wa kifedha

‘’ Kama huna fedha ,ni vigumu kushawishi wapia kura’’ Justina Wamae, Mgombea Mwenza Roots Pary

Suala la uwezo wa kifedha kwa wanasiasa wanawake nalo linaonekana kuwa miongoni mwa vikazo vinavyomzuia mwanamke kufanikiwa kupata ushindi katika ulingo wa siasa.

Hayo yamesemwa na Justina Wangoe Wamae, ambae ni mgombea mwenza kupitia chama cha Roots Party of Kenya.

Katika mahojiano maalumu, Justina amemwambia mwandishi wa BBC Aboubakar Famau swala la urithi au umiliki wa ardhi lina uwezo wa kuimarisha uchumi wa wanawake.

Ikiwa jami inayoongozwa zaidi na wanaume itabadili mtizamo wake na kutoa japo asilimia moja ya ardhi wanazomiliki,wanawake hasa vijijini, watakuwa na uwezo zaidi kuendesha shughuli zao za kiuchumi.

”Changamoto iliyopo kwa wanawake wanasiasa ni kwamba hatuna ile pesa, kwa hiyo ukiingia chama, unaambiwa uwe mpenzi wa kiongozi wa chama kwa sababu huna pesa, lakini wanawake wangekuwa na fedha zao kama wanaume, wangeweza kubishana na wanaume na kusema kama ni ada ya chama nitalipa, lakini tunatafuta msaada kwa sababu hatujiwezi kifedha,” anasema Justina.  

Wakati huo huo, hatua nazo zimeanza kuchukuliwa ili kuwalinda wanawake dhidi ya matusi lakini pia kuweka mazingira rafiki kwao.

Mathalan, kampuni ya teknologia ya Meta, imeweza kutoa taarifa elfu 37 zinazohusishwa kuchangia maudhui ya chuki miongoni mwa jamii. Taarifa hizo zilikuwa katika mtandao wa kijamii wa Facebook.

Meta imesema, imeajiri watu wa kuhakiki na kufuatilia maudhui zinazoweka kuelekea uchaguzi mkuu, ili kuhakikisha mchakato huo unafanyika kwa njia salama na ya amani.

Mwaka wa elfu mbili na kumi na saba (2017) ulikuwa mojawapo ya chaguzi zenye vurugu zaidi ambazo wanawake walishiriki na kulikuwa na ongezeko la visa vya utekaji nyara na unyanyasaji wa kijinsia. Wanawake walilengwa mahususi kwa njia za mitandao na katika kampeini ,wanawake wengi walijiondoa katika uchaguzi.

Wananchi

Kwa upande wake, baadhi ya raia wa Kenya wanaonyesha kufurahishwa na hali ya kisiasa inavyokwenda, hasa katika ushirikishwaji wa wanaweke.

 

Mkazi mmoja wa jijini Nairobi, aliyejitambulisha kwa jina la Mureithi, anasema, yeye anaunga mkono kabisa wanasiasa wanawake, kwa sababu nao ni sehemu ya jamii.

Caro, nae ambae anajishughulisha na biashara ya uwakala wa fedha, anasema, anawaunga mkono wanawake kwa sababu wao wanajua hali ya maisha watu wanayopitia.

Serikali ya Jubilee inayoondoka madarakani, ambayo inaongozwa na rais Uhuru Kenyatta ndio ya kwanza kuchaguliwa nchini Kenya chini ya katiba mpya ya mwaka elfu mbili na kumi, hata hivyo, wachambuzi wa mambo wanasema ndiyo iliyoshindwa kutekeleza baadhi ya vipengele ikiwemo kile cha kuhakikisha uwepo kwa thuluthi moja ya wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Hata hivyo, rais Kenyatta mara kadhaa ameonekana kutetea nafasi yake.

Kwa sasa, ni kusubiri na kuona, ni kwa kiasi gani, kina mama hawa wataibuka kidedea katika uchaguzi mkuu ambao wanawake bado wanaonekana kukabiliwa na ushindani mkubwa miongoni mwao na kutoka kwa wanaume.