Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tunachokijua kuhusu shambulio jipya la ndege isiyo na rubani huko Moscow
Meya wa Moscow Sergei Sobyanin alithibitisha ripoti za mashuhuda wa ndege zisizo na rubani kuanguka katika majengo ya ghorofa huko kusini-magharibi mwa jiji hilo, na Gavana wa Mkoa wa Moscow Andrei Vorobyov alithibitisha mifumo ya ulinzi wa anga kuangusha ndege zisizo na rubani ziliingia mji mkuu.
Wizara ya Ulinzi ya Urusi inadai kwamba ndege nane za UAV zilihusika katika shambulio hilo. Ujumbe kuhusu hilo ulikuja wakati kuna mashambulizi makubwa ya makombora yanaendelea huko Kyiv kwa siku ya tatu mfululizo.
Nini hasa walichokisema Sobyanin na Vorobyov?
"Leo asubuhi, kutokana na shambulio la UAV, uharibifu mdogo umetokea katika majengo kadhaa. Huduma zote za dharura za jiji ziko kwenye eneo la tukio. Wanachunguza mazingira ya tukio. Kwa sasa, hakuna mtu yeyote aliyepatikana kujeruhiwa vibaya. Tafadhali amini vyanzo rasmi tu na usieneze habari ambazo hazijathibitishwa, "- Meya wa Moscow aliandika saa 7:21 katika mtandao wake wa telegram.
Muda mfupi baadaye, gavana wa mkoa wa Moscow aliandika: "Asubuhi ya leo, wakazi wa baadhi ya maeneo ya mkoa wa Moscow waliweza kusikia sauti za milipuko - zilikuwa sauti za ulinzi wetu wa anga. Ndege kadhaa zisizo na rubani zilishambuliwa wakati zikikaribia kuingia Moscow. Nawataka wakazi wote kuwa watulivu."
Wakazi wa mkoa wa Moscow waliona vigumu kubaki watulivu, walipoamka kutokana na sauti za milipuko. Video kadhaa zilizo na ndege zisizo na rubani zilisambaa kwenye mtandao wa Telegraph na mitandao mingine ya kijamii. Ripoti za milipuko na shughuli zinazodaiwa za ulinzi wa anga zilitoka Odintsovo, Barvikha, Krasnogorsk na maeneo mengine yaliyo karibu na Moscow.
Huko Moscow, mashuhuda waliripoti kwamba ndege zisizo na rubani ziligonga maeneo matatu huko Leninsky Prospekt na Mtaa wa Profsoyuznaya, na vile vile kwenye Mtaa wa Atlasnaya huko New Moscow, ambayo ni, nje ya mji wa Moscow.
Kabla ya matangazo ya meya na gavana, mashirika ya serikali yalihusisha mashambulizi ya Moscow na shambulio la ndege zisizo na rubani. "Taarifa zinachunguzwa kuhusu hali ya majengo ya pamoja ya makazi ya ghorofa mbalimbali yaliyoko Leninsky Prospekt, 92, building 1 na Mtaa wa Profsoyuznaya, jengo la 98, jengo la 6," chanzo cha TASS kilisema.
"Hapo awali, ndege zisizo na rubani zinaweza kuwa sababu."
Mpatanishi wa RIA, Novosti alisema kuwa ndege moja isiyo na rubani iligonga sakafu ya juu ya jengo la makazi huko Profsoyuznaya, 98, na kuharibu makazi kadhaa ya watu.
Mkazi wa nyumba hiyo kwenye Leninsky Prospekt, katika mazungumzo na shirika hilo, alifafanua kwamba ndege isiyo na rubani ilipiga ndani ya ghorofa kwenye ghorofa ya 14, ambapo kulikuwa na watu watatu, hakukuwa na mlipuko, hakuna mtu aliyejeruhiwa.
Ndege isiyo na rubani ya tatu ilianguka kwenye jengo la makazi la ghorofa 24 kwenye Mtaa wa Atlasova huko New Moscow.
Sobyanin aliripoti juu ya kuhamishwa kwa wakaazi kadhaa katika nyumba mbili tu, bila kutaja wapi.
Kauli ya Wizara ya Ulinzi ya Urusi
Wizara ya Ulinzi ya Urusi baadaye ilisema kwamba Kiev ilifanya "shambulio la kigaidi" kupitia ndege zisizo na rubani "kwenye maeneo ya jiji la Moscow."
Kwa mujibu wa Idara ya jeshi la Urusi, ndege nane zisizo na rubani zilihusika katika shambulio hilo.
"ndege zote za adui zimeangushwa," Wizara ya Ulinzi ya Urusi inasema.
Ndege tatu zisizo na rubani hazikushambuliwa, kwa hivyo huenda zimegonga majengo ya mkazi hayo, ilisema taarifa hiyo.
"Ndege tatu zilipotezwa muelekeo kwa njia ya vita vya kielektroniki na kushindwa kupiga malengo waliyokusudia," taarifa kwa vyombo vya habari iliyochapishwa kwenye mtandao wa Telegram inasema. "Ndege zingine tano zisizo na rubani ziliangushwa na mfumo wa kombora na bunduki wa Pantsir-S katika mkoa wa Moscow." .
Kituo cha Telegraph cha Baza hapo awali kilidai kwamba takriban ndege 25 zilihusika katika shambulio la asubuhi, nyingi zilipigwa risasi,hasa katika mikoa ya Istra, Krasnogorsk na Odintsovo.
Mashambulizi ya Kiev
Taarifa za ndege hizo zisizo na rubani kugonga majengo ya makazi huko zikisambaa huko Moscow, mji wa Kyiv, Ukraine ulikuwa chini ya mashambulizi makubwa ya anga kwa usiku wa tatu mfululizo. Hili tayari ni shambulio la 17 tangu mwanzo wa mwezi Mei, lakini mashambulizi yamezidi kuongezeka zaidi.
Siku ya Jumapili usiku, mamlaka ilisema mashambulizi hayo, yalihusisha ndege zisizo na rubani 50 za Shahed kamikaze, lilikuwa shambulio kubwa zaidi tangu kuanza kwa vita, na kuua mtu mmoja. Siku ya Jumatatu usiku, pamoja na ndege hizo, roketi zilitumiwa pia, lakini hakukuwa na majeruhi.
Siku ya Jumanne usiku, Urusi ilitumia ndege zisizo na rubani 20 kushambulia Kyiv, ambazo zilipigwa risasi, maafisa wa jiji walisema. Katika wilaya ya Goloseevsky, kutokana na kuanguka kwa uchafu kwenye jengo la makazi ya ghorofa nyingi, moto ulizuka kwenye sakafu mbili za mwisho.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, mtu mmoja alifariki na watatu kujeruhiwa. Wizara ya Ulinzi ya Urusi haikutoa maoni yoyote juu ya hili.
Baada ya shambulio la Kremlin
Hii sio mara ya kwanza kwa ndege zisizo na rubani kushambulia Moscow. Usiku wa Mei 3, 2023, ndege zisizo na rubani mbili ziligonga juu ya jumba la Seneti huko Kremlin. Mamlaka za Urusi zilidai kuwa zilidondoshwa na kulitaja tukio hilo kuwa ni shambulio la kigaidi na jaribio la kumuua Rais Vladimir Putin. Mamlaka ya Ukraine ilikanusha kuhusika na shambulio la Kremlin.
Ndege hizo zisizo na rubani zilizoanguka zilipatikana mapema mwaka huu katika maeneo tofauti ya mkoa wa Moscow.
Akizungumzia kuonekana tena kwa ndege hizo kwenye anga ya Moscow na kugonga majengo yao ya makazi ya watu, Sobyanin alisema kuwa hakuna mtu aliyejeruhiwa vibaya, watu wawili walitafuta msaada wa matibabu, lakini hakuna aliyelazwa hospitalini. Msaada ulitolewa papo hapo. Inaelezwa kuwa msongamano wa magari ulitokea kando ya Mtaa wa Udaltsova kutoka Mtaa wa Leninsky hadi Mtaa wa Mikhail Pevtsov.
Televisheni ya serikali haikuupa umuhimu mkubwa shambulio hilo jipya, mchambuzi wa kisiasa Mikhail Vinogradov anabainisha.
"[Channel] Rossiya-24 inaonyesha marudio ya kuchosha kuhusu maendeleo ya biashara ndogo ndogo, maelezo mafupi ya taarifa za Sobyanin yasiyokamilika - lakini bado haiwekwi wazi. Inaonekana kwamba iliamuliwa kuyapa umuhimu maoni ya Sobyanin, lakini si habari yenyewe ya shambulio. Na zaidi ya yote - kuna ramani tu za mashambulizi kwenye eneo la Ukraine," Vinogradov aliandika katika kituo chake cha Telegram.
'Viwanja vya ndege vya Moscow vinafanya kazi kama kawaida', Shirikisho la Usafiri wa Anga lilisema baada ya shambulio jipya la ndege isiyo na rubani kwenye mji mkuu wa Urusi.
Kamati ya Uchunguzi ya Urusi "inachunguza ukweli wa kuanguka kwa ndege hizo kwenye majengo huko Moscow," ambayo matokeo yake, kulingana na taarifa ya vyombo vya habari kutoka TFR, yamesababisha "uharibifu mdogo."