Rwanda yaanzisha mradi wa umwagiliaji kwa teknolojia ya simu ya mkononi

kilimo
Iliyochapishwa

Na Vyes Bucyana

BBC Swahili

Rwanda imeanzisha mradi wa kumwagilia mashamba kwa kutumia teknolojia ya simu ambapo mkulima anaweza kumwagilia mashamba yake bila kuwepo shambani.

Waanzilishi wa mradi huo wanasema unalenga wakulima zaidi ya elfu 60 mashariki mwa Rwanda, eneo ambalo mara nyingi linakabiliwa na matatizo ya ukame yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

BBC imekutana na Eric Karinganire, mjasiriamali aliyeanzisha mradi huo wa kumwagilia mazao kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya simu za mkononi akiwa ndani ya gari akifanya mipango yake ambayo pia haijamzuia kumwagilia shamba lake ambalo liko mbali na hapo alipo.

ggg
Maelezo ya picha, Eric Karinganire, mjasiriamali aliyeanzisha mradi huo

"Unavyoona niko ndani ya gari nikishughulikia mambo mengine,lakini Pamoja na hayo haijanizuia kumwagilia shamba langu nikibonyeza tu kwenye simu yangu……angalia hapa,…maji tayari nimeyafungua nikitumia simu. kwenye simu yangu unaweza pia kuona ni kiasi gani cha lita ambazo nimekwishatumia. kwa hiyo unaona kwamba hizi simu tunazotembea nazo zinaweza pia kufanya mambo mengine mengi.’’ alisema Eric Karinganire

Simu zinazotumiwa ni za android lakini hasa wanatumia aina ya MaraPhone zinazotengenezwa nchini Rwanda kama wadhamini wakuu wa mradi huo

Kila simu inawekwa programu [app] maalumu inayowezesha mkulima kumwagilia shamba lake popote alipo.

Eric Karinganire anasema maji yanayotumika yanachimbwa ndani ya ardhi milimani kwa kutumia mashine maalumu baada ya kupimwa ipasavyo.

"Ni maji tunayochimba ndani ya ardhi kwa kutumia mitambo maalumu lakini baada ya kuyafanyia vipimo na kuhakiki viwango na ubora, baadae tunayasambaza katika matanki ya maji ndani ya mashamba ya wakulima.‘’ anaeleza

umwagiliaji

Wazo la mradi huu lilitokana na kwamba katika eneo hili wakati wa jua kali wakulima hawafanyi chochote kutokana na ukame,hivyo huteseka na njaa kwa sababu hawawezi kumwagilia mimea yao wakisubiri kipindi cha mvua’’

ggg
Maelezo ya picha, Musabyimana Vestina - mkulima

Musabyimana Vestina ni mkulima ambaye tayari ameanza kutumia teknolojia hii, anasema kwamba wanatarajia itasuluhisha matatizo yanayowakabili katika umwagilia mashamba yao.

‘’Tulikuwa tunamwagilia mashamba yetu kwa kutumia vifaa vya kawaida kama ndoo ama sufuria lakini nina uhakika huu umwagiliaji wa kisasa ambao tumepata utafaa sana hasa kuondoa mihangaiko ya kwenda kutafuta maji maeneo ya mbali, hii ni afueni kwa mkulima na sio ;lazima nimwagilie nikiwepo shambani" anasema.

ggg
Maelezo ya picha, ‘’Tulikuwa tunamwagilia mashamba yetu kwa kutumia vifaa vya kawaida kama ndoo ama sufuria"

Hata hivyo, ni wazi kwamba si kila raia ataweza kumudu gharama za teknolojia hii katika umwagiliaji.

Kila mmoja atahitaji angalau dola 300 ikijumuisha tanki la maji na mabomba- ingawa wenye mradi wanasema kuna njia ya watu kupata mikopo kupitia taasisi za fedha.

Wamiliki wa mradi huo wanaeleza wasiwasi wao kwa sababu ni teknolojia inayotumia umeme na mtandao