Ukraine lazima ipate msaada wa muda mrefu- mkuu wa Nato

Iliyochapishwa

Nchi za Magharibi lazima zijitayarishe kutoa msaada wa muda mrefu kwa Ukraine kwani Urusi haionyeshi dalili za kulegeza kamba, katibu mkuu wa Nato amesema.

Jens Stoltenberg aliiambia BBC kwamba msaada wa kijeshi utahakikisha kwamba Ukraine inasalia kama nchi huru na kuilazimisha Urusi kuketi na kujadiliana kusitisha vita.

Kiongozi wa Urusi anazituhumu nchi za Magharibi kwa kutumia Ukraine kuharibu nchi yake.

Makombora na ndege zisizo na rubani za Urusi zimeshambulia Ukraine mkesha wa Siku ya Mwaka Mpya.

Mpango wa uhamasishaji wa sehemu ya Urusi, ulioamriwa mnamo Septemba, ulionyesha kuwa Moscow haina nia ya kumaliza vita hivi sasa, Bw Stoltenberg aliambia kipindi cha World at One cha Radio 4.

"Vikosi vya Ukraine vilikuwa na kasi kwa miezi kadhaa, lakini pia tunajua kwamba Urusi imekusanya vikosi vingi zaidi, baadhi ya vikosi hivyo sasa vinafanya mazoezi," alisema.

"Yote hayo yanaonyesha kwamba wako tayari kuendeleza vita na pia kujaribu uwezekano wa kuanzisha mashambulizi mapya."

Hapo awali, Rais wa Urusi Vladimir Putin alitoa hotuba ya mwaka mpya, ambapo alijaribu kuwakusanya watu nyuma ya wanajeshi wake wanaopigana nchini Ukraine, akisema kuwa mustakabali wa nchi hiyo uko hatarini.

Mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelensky alimshutumu Bw Putin kwa kujificha nyuma ya wanajeshi wake badala ya kuwaongoza.

Makombora 12 kati ya 20 ya Urusi yalidunguliwa siku ya Jumamosi, mkuu wa majeshi ya Ukraine alisema.

Ndege nyingine zisizo na rubani 45 za kamikaze zilizotengenezwa na Iran zilidunguliwa karibu na Kyiv saa chache tu baada ya kuukaribisha Mwaka Mpya siku ya Jumapili, Jeshi la Wanahewa la Ukraine lilisema.

Mtu mmoja alifariki na makumi ya wengine kujeruhiwa katika mashambulio hayo.

Shambulio hilo aidha ulichochea hasira na chuki miongoni mwa raia wa Ukraine ambao tayari wamechoshwa na mashambulio ya angani ya Urusi.

Milipuko ilipotikisa mji mkuu, baadhi ya wakazi waliimba wimbo wa taifa, huku maafisa wakiishutumu Urusi kwa kuwalenga raia kimakusudi walipokuwa wamekusanyika kusherehekea Mwaka Mpya.

Andriy Nebitov, mkuu wa polisi wa Kyiv, alishirikisha mtandaoni picha ya ndege isiyo na rubani iliyoanguka na maneno "Heri ya Mwaka Mpya" yalioandikwa kwa Kirusi.

"Hiyo ndiyo kila kitu unachohitaji kujua kuhusu taifa la kigaidi na jeshi lake," aliandika kwenye Facebook, na kuongeza kuwa mabaki yalianguka katika uwanja wa michezo wa watoto.

Ingawa hakuna pande zote hazijaonyesha nia ya kulegeza kamba hivi karibuni, Bw Stoltenberg alisema Nato lazima ihakikishe Ukraine inasalia katika msimamo thabiti iwapo kutakuwa na mazungumzo kati ya pande hizo mbili.