'Unaweza kujificha wapi kifo kinapokuja kutoka angani?' maisha ya Gaza

Palestinians walk amid the rubble of destroyed and damaged building in the heavily bombarded city centre of Khan Yunis in the southern Gaza Strip following overnight Israeli shelling, on 10 October 2023

Chanzo cha picha, AFP

Iliyochapishwa

"Kwa kila shambulizi, ninahisi kama tetemeko la ardhi linatokea katika jengo - naweza kuhisi moyo wangu ukidunda kwa hofu na mwili wangu wote unatetemeka," Nadiya, ambaye hataki kufichua jina lake halisi, anasema.

Siku ya Jumatatu asubuhi, aliamshwa na sauti ya milango na madirisha yakivunjwa. "Mashambulizi ya makombora yalianza saa 08:00 asubuhi na kuendelea hadi usiku wa manane. Hayakusimama hata kwa sekunde moja."

Mama wa wavulana wawili - mmoja wa umri wa miaka mitano, mwingine wa miezi mitatu - alikuwa akiishi katika gorofa ambayo familia yake upande wa pwani ilikuwa imenunua na kuipamba.

Alikuwa peke yake na wavulana wakati mumewe - daktari katika shirika la kimataifa la misaada - alikuwa nje kusaidia majeruhi.

"Nini kinaendelea? Na itaisha lini?" kijana wake mkubwa aliuliza. Nadiya anasema njia pekee ya kujaribu kumtuliza ni kumwambia kwamba "Sauti ya mlipuko huja muda mfupi baadaye badala ya wakati halisi" - na hivyo ndivyo wanavyojua kuwa wako salama.

Ni aina ya taarifa ambayo hakuna mtoto wa miaka mitano anayepaswa kutarajiwa kuelewa, lakini kwa Nadiya, hii ndiyo njia bora zaidi wanayopaswa kukabiliana na hali ilivyo kwa sasa.

Milipuko hiyo bado inaleta madhara makubwa kwani mvulana wake wa miezi mitatu amekuwa akipata degedege na anakataa kula.

A fireball erupts after an Israeli air strike in Gaza City  on 9 October 2023

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Moto mkubwa ulizuka baada ya shambulizi la anga la Israeli katika mji wa Gaza

Kwa siku chache zilizopita, Nadiya amekataa kuondoka nyumbani kwake ambapo "kila kona ina kumbukumbu". Lakini Jumatatu usiku, alisikia majirani zake wakikimbia chini huku wakipaza sauti: "Kimbieni!Torokeni!"

Mama huyo kijana alisita kwa sekunde kadhaa, akili yake ikiwa na wakati mgumu kuamua achukue hatua gani. Kisha akabubujikwa na machozi ya kutojua cha kufanya na kujawa na hofu.

Aliondoka kwenye jengo hilo akiwa na watoto wake wawili, lakini anasema hakuweza kutambua eneo jirani kwani majengo karibu na mtaa wake yalikuwa yameporomoka na kuwa vifusi.

Sasa anajaribu kufika nyumbani kwa wazazi wake akikimbilia usalama, lakini anauliza: "Unaweza kujificha wapi kifo kinapokuja kutoka angani?"

Nadiya na wakaazi wengine wa Gaza ambao BBC imezungumza nao, wanasema ukubwa wa uharibifu wa Gaza haujawahi kutokea hapo kabla.

'Hakuna sehemu iliyo salama Gaza'

Pictures of a garden in Gaza before and after Israeli air strikes

Chanzo cha picha, Dina Faisal

Maelezo ya picha, Dina Faisal alituma picha hizi za bustani yake katika kitongoji cha Rimal - hapo awali kulichukuliwa kuwa moja ya sehemu salama zaidi huko Gaza - kabla na baada ya shambulio la anga la Israeli.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika kitongoji cha pwani cha Rimal, Dina mwenye umri wa miaka 39 alikuwa akijikinga na mashambulizi ya anga ya Israel akiwa na mama yake, baba yake, dada yake na wapwa wawili katika jumba lao lenye bustani.

Eneo hili kwa kawaida ni la makazi tulivu kiasi cha kilomita 3 (maili mbili) kutoka katikati mwa jiji.

Siku ya Jumatatu alasiri, familia ilianza kusikia makombora kuzunguka kitongoji.

"Tulifikiri tulikuwa salama ndani ya nyumba, lakini ghafla na bila onyo lolote kutolewa, madirisha yalianza kuvunjika, milango ikagongwa na kuruka," Dina anasema. "Sehemu za paa zilishuka karibu na vichwa vyetu."

Wakiwa katika hali ya mshtuko, walisalia ndani ya nyumba iliyoharibiwa huku mashambulizi sita zaidi ya anga yakishambulia eneo hilo, wanasema.

Mara tu hali ilipoanza kuwa tulivu, Dina na familia yake walitoroka kuokoa maisha yao, na kuacha kila kitu nyuma.

Walikimbia hadi hospitali ambapo walitibiwa majeraha yao - Dina anasema walikuwa na bahati majeraha yao hayakuwa ya kina.

Waliporudi kwenye nyumba hiyo kuchukua vitu vyao, ilikuwa imemalizwa kabisa.

Sasa wanaishi kwa muda na familia nyingine, na Dina bado anajaribu kukabiliana na mshtuko wa "kupoteza nyumba yetu, kumbukumbu zetu na mahali ambapo tulikuwa tunajisikia salama".

"Hakuna sehemu aliye salama katika eneo la Gaza," anaongeza.

Hospitali zinawakati mgumu kuokoa maisha

A Palestinian man sits in front of a charred building as a fire rages through its interior, following Israeli air strikes in Gaza City's Rimal district on 10 October 2023

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, A charred building in Gaza City's Rimal district

Katika hospitali ya Alshifaa, kituo kikubwa zaidi katika ukanda huo wenye watu wengi, mwenyekiti Dk Mohamed Abo Suleima anasema hali ni mbaya.

"Takriban watu 850 wameuawa na zaidi ya 4,000 kujeruhiwa," anasema.

Hospitali imekuwa ikitegemea jenereta za umeme kwa kuwa umeme umekatika na uliosalia unaweza kuendelea kwa siku tatu zaidi, anasema.

Kwa vile Israeli imetangaza kuziba kabisa Gaza, maji yaliyotiwa chumvi sasa ni haba ndani ya hospitali.

Dk Abo Suleima anasema kwa sasa wanatanguliza matumizi ya maji safi kwa "kesi za kuokoa maisha" huku wakilazimika kufunga idara zingine hospitalini kusaidia kuokoa maisha.

A man walks through rubble in a heavily bombarded neighbourhood following overnight Israeli air strikes on Gaza City's Shati refugee camp early on 9 October 2023

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Mwanamume akipita kwenye vifusi katika sehemu iliyoshambuliwa kwa mabomu katika kambi ya wakimbizi ya Shati katika Gaza City.

Daktari huyo anahofia usalama wa wagonjwa wake, lakini pia wafanyakazi wake – anasema magari ya kubebea wagonjwa yalilengwa na daktari aliuawa akiwa njiani kuelekea hospitalini.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), idadi ya watu waliotoroka makazi yao imeongezeka kwa kasi katika muda wa saa 24 zilizopita na zaidi ya Wagaza 187,000 sasa wametoroka makazi yao kutafuta hifadhi.

Huku mashambulizi makubwa ya mabomu yakiendelea, shirika hilo limeweza kuwahifadhi watu 137,500, lakini lina wasiwasi kwamba hivi karibuni litafikia uwezo wake kamili.

Maduka hayana chakula

Ishaq, 27, alikuwa akiishi na mama yake mzee, baba yake, shemeji yake na watoto wake watano katika kitongoji cha Shujaiyya.

Baada ya Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu kuiambia nchi yake kuwa wanaingia kwenye "vita virefu na vigumu" kufuatia mashambulizi ya Hamas siku ya Jumamosi, Ishaq na familia yake walitarajia kitakachotokea.

Walikusanya vitu vyao vya thamani zaidi na kila mmoja akiwa amebeba begi dogo, wakatafuta hifadhi katikati ya jiji.

Wakiwa njiani, familia hiyo yenye watu 20 ilijaribu kutafuta vitu vya msingi kama vile mboga ili kuvihifadhi kwa ajili ya siku zijazo lakini maduka yalikuwa hayana chochote kwani watu wengi wa Gaza walikimbilia kufanya manunuzi mara tu walipopata habari kuhusu mashambulizi ya Jumamosi.

Waliishia kujificha katika jengo la makazi katikati mwa jiji, pamoja na familia nyingine dhidi ya mashambulizi ya anga.

"Tulikaa huko kwa saa 48 bila umeme wala maji," Ishaq anasema. Kisha Jumatatu jioni, alipokea ujumbe kutoka kwa jeshi la Israeli kuhama jengo hilo katikati ya usiku.

Kutoroka kwao kulichochewa na mashambulizi ya anga.

"Tulichoweza kuona karibu nasi ni mabaki ya majengo".

Walitembea kaskazini mwa katikati ya jiji hadi kwenye moja ya makazi ya kawaida tulivu, lakini wakaona kwamba huko pia "majengo mengi yalikuwa tayari yamebaki vifusi".

Ishaq na familia yake wamejificha kwa zaidi ya saa 12 katika ghorofa ya chini ya ardhi yenye giza nene ya jengo lililoharibiwa kiasi pamoja na familia nyingine 10."Tunaishi kwa hofu kabisa ya nini kitatutokea saa zijazo na tunaomba usalama," anasema.

Bado hawajui la kufanya au waende wapi.

(Hakuna hata mmoja wa wachangiaji ambao BBC ilizungumza nao aliyetaka picha yao itumike.)