Rasmus Hojlund: Mchezaji anaepigiwa hesabu na Manchester United

Chanzo cha picha, Getty Images
Ulinganisho kati ya Erling Haaland na Rasmus Hojlund uko wazi. Wote wana urefu wa futi 6 na rangi ya nywele zao inafanana. Wote wawili hawana huruma wakati wa kushambulia. Mwanzoni mwa msimu mpya wa Ligi Kuu, wote wanaweza kuwa wanacheza vilabu vya Manchester.
Akizungumza siku ya Jumatatu, meneja wa United, Erik ten Hag alisema klabu hiyo imepiga hatua kutafuta mshambuliaji mpya.
Hojlund, 20, anasalia kuwa shabaha ya wazi zaidi ya United, ingawa Mashetani Wekundu wanasita kufikia dau la Atalanta la pauni milioni 60 kwa mchezaji huyo wa kimataifa wa Denmark.
Je, ataleta nini kwenye safu ya ushambuliaji katika Ligi Kuu ya Uingereza na United, na anaweza kushindana na Haaland?
Baada ya kutumia ujana wake katika timu ya Boldklubben af 1893 na Brondby, Hojlund hatimaye aliingia rasmi katika soka la kulipwa huko Copenhagen, na akacheza mchezo wake wa kwanza akiwa na miaka 17 mwaka 2020.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati akiendelea kuimarika, aliondoka ligi ya Denmark, Januari 2022 akiwa ameshindwa kufunga katika mechi 19 za ligi - ingawa ni mechi mbili tu alizoanza katika kikosi cha awali.
Alijiunga na timu ya Austria ya Sturm Graz - hatua ambayo iliboresha uwezo wake. Katika kipindi cha pili cha msimu wa 2021-22, Hojlund alifunga bao kila baada ya mechi moja, akifunga mara tisa katika mechi 17 alizoanza.
Hojlund alivutia kwa mguu wake wa kushoto wenye hatari na akili yake awapo mchezoni. Kiwango chake kilipelekea kuhamia Italy katika klabu ya Atalanta kwa kitita cha pauni milioni 15, mara 10 zaidi ya kile ambacho Sturm Graz ilimlipa mwezi Januari.
Msimu uliopita alifunga magoli 20 katika mechi 47 akiwa na timu hiyo ya Serie A na Denmark, ambayo alicheza mechi yake ya kwanza Septemba.
Mnamo Machi, alifunga magoli matano katika mechi mbili za kufuzu Michuano ya Uropa kwa Denmark, ikiwa ni pamoja na kufunga mabao matatu dhidi ya Finland.
Hojlund analingana vipi na Haaland?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Uwezo anao, lakini unapolinganisha magoli na ya Haaland, Hojlund ameachwa mbali sana.
Haaland alifunga mabao 36 katika mechi 35 alizocheza Manchester City kwenye ligi wakati wa msimu uliopita - bao moja kila dakika 77. Katika Serie A, Hojlund alitingisha wavu kila baada ya dakika 204.
Haaland alikuwa na msimu uliovunja rekodi, ni mkubwa kwa miaka miwili kumzidi Hojlund, anachezea mabingwa wa Ulaya – Man City. Katika msimu wa pili - Haaland alifanikiwa kufunga mabao 12 katika mechi 25 alizoicheza katika timu ya Molde.
United wanahitaji mshambuliaji wa kati. Huku Anthony Martial akitumia muda mwingi wa msimu uliopita akiwa nje ya uwanja kutokana na jeraha, Rashford amekuwa kinara wa timu hiyo.
United iliamua kutomsajili mchezaji wa Burnley, Wout Weghorst kwa mkataba wa kudumu mwanzoni mwa dirisha la uhamisho. Pia, wamekataa kutoa pesa kwa Kylian Mbappe wa Paris St-Germain na Harry Kane wa Tottenham, ambao wote ni wanasoka wa kiwango bora.

Chanzo cha picha, Getty Images
Hojlund anaweza kupikwa na kufaa katika kikosi cha kwanza cha United. Akiungwa mkono na mawinga kama vile Marcus Rashford, Alejandro Garnacho na Jadon Sancho, United inaweza kujivunia moja ya wachezaji wa mbele wenye kasi zaidi kwenye ligu kuu ya Uingereza.
Vilevile Hojlund ana pasi nzuri na anapiga chenga zaidi ya Haaland - wastani wa miguso 10 zaidi kwa kila mechi. Kwa maana, ana sifa za winga - nambari tisa.












