Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwanini tafiti za matibabu zilitumia zaidi wanaume kuliko wanawake?
Wanasayansi kwa muda mrefu walidhani kuwa wanyama wa kike wangetoa majibu sawa na ya wanaume katika majaribio ya kitafiti. Miaka kumi iliyopita, ukisoma ripoti ya kisayansi ya utafiti unaohusisha panya, mara nyingi walitumia wanyama wa kiume pekee.
Leo hii hali hiyo inabadilika. Tafiti zaidi na zaidi zinatumia wanyama wa jinsia zote katika majaribio. Kwa hivyo, maarifa mapya yanaibuka kuhusu tofauti za kijinsia. Tafiti pia zinaonyesha tofauti za kijinsia katika masuala ya matibabu ya binadamu.
Kwa mfano, wanawake wana uwezekano mara mbili wa kugunduliwa na sonona kuliko wanaume. Na tofauti za kijinsia pia ziko wazi juu ya namna dawa za kupambana na msongo wa mawazo zinavyofanya kazi.
Wanawake na wanaume
Kuwatenga wanawake kwenye majaribio kulileta matokeo mabaya kwa afya ya wanawake. Mfano mmoja ni athari za dawa—yale matokeo mabaya yasiyotarajiwa baada ya kutumia dawa, kama vile kichefuchefu, maumivu ya kichwa, kifafa, na matatizo ya moyo.
Wanawake kwa kawaida huwa na hatari mara mbili kudhurika na athari mbaya za dawa (ingawa wanaume wako katika hatari kubwa ya aina fulani za athari). Sababu moja ni kwamba wanawake, kwa umbile ni wadogo kuliko wanaume.
Sababu nyingine ni kuwa homoni za wanawake na shughuli za mmeng’enyo, hubadilisha utendaji kazi wa dawa kwa wanawake.
Kwa nini wanawake walitengwa?
Wanawake kwa kiasi kikubwa hawakujumuishwa kwenye majaribio kwa sababu ya mzunguko wao wa hedhi. Kubadilika kwa viwango vya homoni hufanya data kuwa ngumu kufasiri. Viwango vya homoni za kike hupanda na kushuka. Hii inaweza kuathiri kazi ya ubongo, tabia na majibu ya dawa.
Pia, kipaumbele cha wanaume katika majaribio ya kimatibabu kimetokea kwa sababu wanawake wa umri wa kuzaa wanaweza kuwa wajawazito na bado hawajui. Mfano dawa ya Thalidomide.
Dawa hiyo ilitengenezwa miaka ya 1950 kama dawa ya usingizi - lakini haikuwa imejaribiwa kwa wanyama wajawazito au wanadamu. Upesi madaktari waligundua kwamba thalidomide inaleta matatizo ya ukuaji wa watoto waliozaliwa na mama wanaotumia dawa hiyo.
Kwa makadirio watoto 10,000 walizaliwa duniani kote wakiwa na mikono na miguu dhaifu na kasoro nyingine.
Mambo yanakuwa mazuri?
Kutokana na miaka mingi ambayo wanawake wametengwa, bado kuna mengi ambayo hatujui. Kuna uwanja unaokua wa utafiti unaochunguza mwingiliano kati ya dawa na mzunguko wa hedhi, ujauzito, homoni na uzazi wa mpango.
Kwa mfano, baadhi ya dawa za kuzuia kifafa zinaweza kupunguza ufanisi wa dawa za uzazi wa mpango, wakati dawa za uzazi wa mpango zinaweza kupunguza ufanisi wa baadhi ya dawa za kifafa katika kukidhibiti.
Nchini Marekani, ushirikishwaji wa wanawake katika majaribio ya kimatibabu umekuwa wa lazima kuanzia 1990. Takribani miaka 30 baadaye, tafiti zinaonyesha kuwa nusu ya washiriki katika majaribio yaliyofadhiliwa na Taasisi ya Kitaifa za Afya (NIH) kwa sasa ni wanawake.
2014, NIH, moja kati ya taasisi zinazofadhili tafiti za matibabu ulimwenguni, ilitangaza kwamba maombi yote ya ruzuku lazima yajumuishe tafiti za kiume na za kike. Sera hii tangu wakati huo imepitishwa na wafadhili wakuu wa tafiti katika nchi nyingine, kama vile Canada na Umoja wa Ulaya.