Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita vya Ukraine: Jinsi Urusi ilivyochukua eneo la kusini na kisha kukwama
Wakati Urusi ilipoivamia Ukraine mwaka mmoja uliopita, mojawapo ya mafanikio makubwa waliyopata hapo awali yalikuwa kusini mwa Ukraine. Ndani ya siku chache wanajeshi wa Urusi waliokuwa wakishambulia kutoka Crimea walikuwa wameteka eneo la Ukraine lenye kubwa kuliko Uswizi.
Mamlaka za Ukraine bado hazijaeleza ni nini kilienda vibaya kusini katika siku hizo za mwanzo. Ili kusaidia kufichua kilichotokea, BBC imezungumza na maafisa wa kijeshi, wanasiasa na wanaharakati.
Mnamo tarehe 22 Februari 2022 saa 19:15, katibu wa baraza la usalama la Ukraine Aleksey Danilov alipokea folda nyekundu yenye hati za siri. Walionya kwamba maisha ya rais yalikuwa chini ya tishio la karibu. Mara moja, Bw Danilov aliwasiliana na mkuu wa huduma za usalama, waziri wa mambo ya ndani, waziri mkuu na Rais Volodymyr Zelensky mwenyewe.
Lakini uongozi wa Ukraine uliacha kutangaza sheria ya kijeshi wakti huo. Hakukuwa na upangaji wowote wa wanajeshi. Wiki chache tu kabla, mamlaka ya Ukraine ilielezea maonyo ya nchi za Magharibi ya uvamizi wa Urusi kama "udanganyifu" na kutoa wito kwa kila mtu kuwa mtulivu.
Bw Danilov anasema serikali ilikuwa na taarifa za kina kuhusu uvamizi huo uliopangwa, ikiwa ni pamoja na tarehe zake. "Tulitarajia tarehe 22 Februari," anaelezea, akitoa ramani ya siri ya mkoa wa Kyiv. Ikichukuliwa kutoka kwa kamanda wa Urusi, anasema inathibitisha ripoti za kijasusi kwamba mpango wa awali wa Urusi ulikuwa kuivamia siku mbili mapema kuliko walivyofanya.
"Lengo letu lilikuwa ni kuepusha hofu yoyote ndani ya nchi. Kwa hiyo, ilikuwa muhimu kufanya yote hayo kuwa siri."
Ikiwa mamlaka za Ukraine zilijua mengi kuhusu mipango ya Moscow, kwa nini askari wa Kirusi waliweza kuingia katika eneo la Kherson lililo kusini haraka hivyo?
Sehemu ndogo na nyembamba ya ardhi hutenganisha peninsula ya Crimea kutoka Ukraine bara, na vilikuwa vizuizi vya asili kwa wanajeshi wa Urusi. Pia kulikuwa na mtandao mpana wa njia za umwagiliaji katika eneo la Kherson.
Vikosi vya Ukraine vilihitaji tu kuharibu madaraja yote huko ili kupunguza kasi ya kusonga mbele kwa Urusi. Lakini hilo halikutokea.
Bw Danilov anasema mamlaka kwa sasa wanachunguza hili, na hadi mchakato huo ukamilike hawawezi kutoa jibu: "Lakini hatufichi ukweli huu, hatuuweki kwenye droo."
Daraja la Chonhar linalovuka mlango wa bahari kati ya Crimea na Kherson lilikuwa limetegwa vilipuzi, mkuu wa majeshi wa Ukraine alithibitisha baada ya uvamizi huo. Lakini ilikataa mapendekezo kwamba vilipuzi viliteguliwa, ikisema kuwa uvamizi wa Urusi ulikuwa mara 15 kwa ukubwa wa vikosi vya ulinzi vya Ukraine.
Wakosoaji wamedai kuwa ilikuwa ni kwa sababu ya utawala huo wa Urusi kwamba daraja hilo lilipaswa kuharibiwa.
Ni wazi vikosi vya Ukraine havikuwa tayari kwa hali ambayo wanajeshi wa Urusi walivuka kwa urahisi katika eneo la kusini la Kherson.
Kwa hiyo, ilibidi warudi nyuma kutoka eneo hilo tangu mwanzo. Walipoondoka, ilichukua saa mbili kwa safu za magari ya kijeshi na askari kuvuka daraja la Antonivskiy karibu na jiji la Kherson, kulingana na Lt Evgeniy Palchenko, ambaye alitetea daraja la mto Dnipro.
Hiyo inaashiria Ukraine ilikuwa imekusanya idadi kubwa ya wanajeshi karibu na Crimea. Lakini madaraja yakiwa bado yamesimama, walizidiw kwa haraka na kushidnwa nguvu.
"Unawezaje kuzuia mashambulizi yao wakati hatukuwa na mifumo ya ulinzi wa anga?" Lt Palchenko anaeleza. "Ndege zao za kivita ziliruka na kudondosha mabomu, na kulipua kila kitu. Tulipoteza wanajeshi na vifaa vingi huko."
Kasi ilikuwa muhimu kwa mafanikio ya Urusi. Mbinu yao ilikuwa kupita miji mikubwa, kuizunguka na kusonga mbele. Walipanga kuchukua Mykolaiv katika siku mbili na Odesa katika siku tatu, anasema Meja Jenerali Dmytriy Marchenko, ambaye alitumwa kuandaa ulinzi wa Mykolaiv. Lakini mpango wa Urusi uliishia kufeli.
Jenerali Marchenko alipofika, bado hakukuwa na mpango wa kutetea jiji hilo. “Nilipouliza uko wapi niliambiwa bado hawajaweka ramani,” alisema.
Alichukua ramani ya barabara, akaigawanya katika sehemu nne na kuteua vitengo na makamanda kuwajibika kwa kila sehemu. Walitawatuma wanajeshi na haraka wakasajili maelfu ya watu. Wengi wa wageni walikuwa wamehudumu katika jeshi hapo awali.
Walianzisha vikundi vya kupambana na vifaru vilivyo na vifaa vya kurushia maguruneti na kupanga ishara ili kuonya wakati mizinga ya Urusi ilipokaribia. Tofauti na Kherson, madaraja katika mitaro ya umwagiliaji katika eneo hilo yaliharibiwa na vikosi maalum vilivyowekwa haraka vilivyoongozwa na Mbunge Roman Kostenko.
Wanajeshi wa Ukraine walipigana vikali kupunguza kasi ya Urusi karibu na daraja la Antonivskiy. Usiku wa manane tarehe 25 Februari, vikosi vya Urusi viliendelea na mashambulizi. Luteni Palchenko na kikosi chake cha mizinga walikuwepo kuwazuia.
"Kifaru changu kiligongwa mara chache, na mfumo ulikuwa chini. Kwa hiyo, tulipaswa kufanya kila kitu kwa mikono, kama katika mizinga ya T-34 wakati wa Vita Kuu ya Pili vya Dunia."
Vikosi vya Urusi vilikuwa vingi sana, kwa hivyo Lt Palchenko na kikosi chake walilazimika kurudi nyuma kutoka kwa daraja. Lakini alirudi huko mara kadhaa usiku huo. Vifaru vyake vilifunika askari wa miavuli wa Ukraine na kazi yao ilikuwa kuzuia askari wa Urusi kuvuka daraja.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 23 baadaye alitunukiwa tuzo ya heshima ya juu ya kijeshi nchini humo, Hero of Ukraine.
Upinzani wao ulimpa Mykolaiv siku chache zaidi kuandaa utetezi wake. Uratibu na mawasiliano kati ya timu za kijeshi na za kiraia ilimaanisha kuwa wakati huo ulitumiwa vizuri.
"[Gavana wa Mykolaiv] Vitaliy Kim alifanya kazi bora kwa kuwasiliana na watu ili kuandaa msaada," Meja Jenerali Marchenko anakumbuka. "Tulihitaji wachimbaji - walikwenda haraka na kuchimba [mitaro na mifereji]. Tulihitaji matofali ya zege za kuzuia tanki - katika nusu siku, yote yalifanyika."
Raia wa eneo hilo walifuatilia kila mara harakati za askari wa Urusi na kupitisha habari kwa wanajeshi wa Ukraine. Watu wa kawaida waliharibu magari ya kivita na kuchukua waanjeshi wafungwa, anasema Meja Jenerali Marchenko.
"Tulisimamisha majeshi ya Urusi kwa sababu watu walisimama," anaongeza.