Ni mchezaji yupi huenda akahamia klabu nyingine?

Chanzo cha picha, Getty Images
Huu ni wakati wa mwaka ulio na shughuli nyingi katika ulingo wa soka la kulipwa.
Baada ya miezi kadhaa ya uvumi kuhusu ni mchezaji yupi anaweza kwenda wapi, dirisha la usajili la Januari sasa limefunguliwa na baadhi ya tetesi hizo zinaweza kuwa kweli hivi karibuni.
Tumekusanya baadhi ya taarifa zinazozua gumzo mitandaoni na ambazo zinaweza kuthibitishwa wiki chache zijazo.
Kalvin Phillips (Manchester City)
Anahusishwa na: Newcastle, Juventus

Chanzo cha picha, Getty Images
Kalvin Phillips alifunga bao lake la kwanza akiwa na Manchester City walipoilaza Red Star Belgrade kwenye Ligi ya Mabingwa mnamo Desemba 13, lakini kuna uwezekano huenda akarefusha muda wake katika uwanja wa Etihad.
Newcastle wamekuwa wakihusishwa na tetesi za kutaka kumnunua kiungo huyo wa kimataifa wa Uingereza, huku miamba wa Italia Juventus pia wakiripotiwa kuwania saini yake.
Jadon Sancho (Manchester United)
Anahusishwa na: Borussia Dortmund
Kwa muda mrefu mustakabali wa Jadon Sancho Old Trafford umekuwa wazi, baada ya mshambuliaji huyo kuondolewa kwenye kikosi cha kwanza kutokana na mzozo kati yake na mkufunzi wa Manchester United Erik ten Hag.
Klabu yake ya zamani ya Borussia Dortmund imetajwa kama mahali pengine pa kwenda lakini mshahara unaonekana kuwa kikwazo kikuu.
Mchezaji mwenzake Donny van de Beek alijiunga na Eintracht Frankfurt ya Bundesliga wakati dirisha la uhamisho lilipofunguliwa tarehe 1 Januari.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 atajiunga kwa muda uliosalia wa msimu huu, akiwa na chaguo la kubadilisha uhamisho huo kuwa mkataba wa kudumu.
Aaron Ramsdale (Arsenal)
Anahusishwa na: Chelsea, Newcastle

Chanzo cha picha, Getty Images
Mchezaji wa kimataifa wa Uingereza Aaron Ramsdale alipoteza nafasi yake ya mlinda lango wa Arsenal kwa David Raya mwezi Septemba.
Tunapoelekea michuano ya Uropa msimu ujao, anaweza kutafuta uhamisho wa Januari ili kuhakikisha anacheza soka la kawaida la kikosi cha kwanza.
Chelsea na Newcastle zote zimehusishwa kutaka kumnunua Ramsdale.
Conor Gallagher (Chelsea)
Anahusishwa na: Tottenham
Conor Gallagher amekuwa akiichezea Chelsea mara ya kwanza msimu huu na hata kuwa nahodha wa timu hiyo mara kadhaa, jambo ambalo linashangaza kwamba huenda akaelekea kwingine Januari.
The Blues wanasemekana kuhitaji kusawazisha vitabu baada ya matumizi makubwa ya fedha katika kipindi cha miezi 18 iliyopita na Gallagher anaweza kutolewa kufanikisha hilo.
Kiungo huyo wa kati wa Uingereza anaaminika kupatikana kwa takribani kitita cha £50m na amekuwa akihusishwa na uhamisho wa kwenda kwa wapinzani wa Chelsea wa London Tottenham.
Ivan Toney (Brentford)
Anahusishwa na: Arsenal
Arsenal ililegalega katika mbio za kuwania ubingwa wa ligi kuu Disemba 28 walipofungwa 2-0 nyumbani na West Ham - mchezo ambao uliangazia hitaji la mtu kuweka kimyani nafasi nyingi walizotengeneza. Kikosi cha Mikel Arteta kilijaribu kufunga mara 30 huku nane zikilenga kuingia wavuni .
Mshambuliaji wa Brentford, Ivan Toney kwa muda mrefu amekuwa akitajwa kuwa mchezaji wa kwanza aliyepewa kipaumbele Januari ili kuimarisha safu ya ushambuliaji ya Arsenal.
Toney bado anatumikia marufuku yake ya miezi minane kutojihusisha na soka kwa kukiuka sheria ya Kamari za Shirikisho la Soka lakini anatarajiwa kurejea Januari 17.
Joao Palhinha (Fulham)
Anahusishwa na: Arsenal, Bayern Munich, Liverpool

Chanzo cha picha, Getty Images
Fulham ilijaribu kuzima hamu ya klabu zinazomuwania kiungo Joao Palhinha kwa kumpa mkataba mpya mwezi Septemba, lakini hatua hiyo huenda ikatibuliwa Januari hii.
Klabu za Arsenal, Bayern Munich na Liverpool zote zinataka kumnunua mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno.
Fulham wamedhamiria kutomruhusu kuondoka kwa bei nafuu na inaaminika wanataka karibu pauni milioni 60 kumwachia mchezaji huyo.
Thomas Partey (Arsenal)
Anahusishwa na: Juventus
Majeraha yamepunguza mechi za Thomas Partey katika klabu ya Arsenal msimu huu na huku Mikel Arteta akiaminika kuhitaji kuwauza wachezaji ili kufadhili wawasili mwezi Januari, kiungo huyo anaweza kuachia nafasi.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 amerejea mazoezini baada ya tatizo la misuli kumweka nje kwa miezi miwili na amekuwa akihusishwa na kuhamia kwa miamba ya Italia Juventus.
Trevoh Chalobah (Chelsea)
Anahusishwa na: Crystal Palace, Bayern Munich, Roma
Sawa na Conor Gallagher, Trevoh Chalobah huenda akalazimika kuondoka Chelsea Januari ili kuwasaidia kusawazisha vitabu.
Beki huyo hajaichezea The Blues msimu mzima baada ya kupata jeraha la paja wakati wa maandalizi ya msimu mpya.
Chalobah huenda akahamia nje ya nchi, huku Bayern Munich na Roma wakiripotiwa kumnyatia, ingawa Crystal Palace pia wanavutiwa naye.
Emile Smith Rowe (Arsenal)
Kiungo huyo wa kati wa Uingereza amerejea Arsenal hivi majuzi baada ya kupona jeraha lakini anaweza kuhama Januari ikiwa Mikel Arteta atahitaji kurekebisha mambo ili kuimarisha kikosi chake.
Aston Villa wamehusishwa na uwezekano wa kumpata mchezaji pamoja na pesa taslimu, huku mwenzake Douglas Luiz akitarajiwa kuhamia upande mwingine.
Raphael Varane (Manchester United)
Anahusishwa na: Real Madrid, Bayern Munich
Mkataba wa beki huyo unamalizika mwishoni mwa msimu huu, kwa hivyo Manchester United wanaweza kushawishika kumuuza wakati wa uhamisho wa Januari.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 30 amekuwa akihusishwa na tetesi za kurejea Real Madrid, lakini Bayern Munich pia inasemekana kuingia kwenye mbio za kumsajili.
Uhamisho unaweza kutegemea orodha ya majeruhi ya Manchester United, huku mabeki wao kadhaa wakiwa nje.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na lizzy masinga












