Kanisa lapatikana 'likimtoa' mapepo mvulana mmoja

Exterior of a UCKG church
    • Author, By Katie Mark
    • Nafasi, BBC Panorama
  • Iliyochapishwa

Tawi la Uingereza la kanisa la Christian church limenaswa kisiri kwenye video likijaribu ''kumtoa mapepo'' kijana wa miaka 16.

Mchungaji wa Kanisa la Universal Church of the Kingdom of God (UCKG) alionekana akikariri kile kinachoonekana kama "maombi makali" ili kumtoa mapepo mvulana huyo.

BBC Panorama pia iliambiwa na kijana ambaye zamani alikuwa akishiriki mapenzi ya jinsia moja kwamba alifanyiwa "maombi makali" akiwa na umri wa miaka 13 kujaribu kumrudisha sawa.

Kanisa la UCKG linasema watoto walio na umri wa chini ya miaka 18 hawaruhusiwi katika huduma za "maombi makali" na "haifanyi tiba ya uongofu".

Uchunguzi wa BBC Panorama umebaini:

Kanisa linawaambia washirika wake kuwa linaweza kusaidia kutibu matatizo ya afya ya akili kwa kuwafukuza pepo wabaya

Kiongozi wa kanisa nchini Uingereza anaelezea kifafa kama "tatizo la kiroho"

UCKG ina matawi kote ulimwenguni, yakiwemo 35 nchini Uingereza, ambako imesajiliwa kama shirika la hisani. Inasema ina zaidi ya washiriki 10,000 kote nchini na inajielezea kama kanisa la Kipentekoste la Kikristo.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Maombi ya kuwafukuza pepo wachafu si ya kawaida katika ulimwengu wa Kikristo. Baadhi ya makanisa huyaita ukombozi au kutoa pepo - ingawa neno hili la pili si neno ambalo UCKG hutumia.

Dk Joe Aldred, askofu wa Kipentekoste ambaye anafanya kazi ya kuleta pamoja tamaduni mbalimbali za Kikristo, anasema: "Kanisa la Uingereza linawatoa pepo katika kila jimbo. Swali ni jinsi inavyofanywa."

"Maombi yenye nguvu" katika UCKG kwa kawaida huhusisha mchungaji kumwekea mikono washirika na kuwaombea pepo mbaya aondoke kwenye miili yao. Kanisa linasema kuwa linaendesha maombi hayo katika ibada zinazoitwa "utakaso wa kiroho" kila wiki ili "kuondoa chanzo cha matatizo".

UCKG ilichunguzwa kufuatia mauaji ya mtoto wa miaka minane Victoria Climbie, ambaye aliteswa hadi kufa na shangazi yake mkubwa na mwenzi wake.

Wiki moja kabla ya kifo chake mwaka wa 2000, wanandoa hao walikuwa wamempeleka Victoria - ambaye alikuwa akionyesha dalili za unyanyasaji - kwenye tawi la kanisa hilo.

Mchungaji mmoja alisema alifikiri huenda amepagawa ndio maana akapendekeza apelekwe kwenye ibada ambapo alifanyiwa"maombi makali". Baadaye, kabla ya ibada kufanyika, mchungaji alimwambia shangazi yake Victoria ampeleke hospitali.

Ripoti ya Tume ya Misaada ilionyesha kwamba "ukubwa wa hali ya Victoria haukutambuliwa kikamilifu au kuripotiwa kwa mamlaka husika" siku chache kabla ya kifo chake. Ilisema "ilikuwa na wasiwasi" kanisa halina sera rasmi ya ulinzi wa watoto.

Kufuatia ukosoaji huo, kanisa lilianzisha sera ya ulinzi. Sasa, inaahidi kutofanya maombi ya nguvu kwa mtu yeyote chini ya miaka 18.

BBC Panorama ilitembelea huduma ya kikundi cha vijana cha UCKG huko Brixton, kusini mwa London, iliyohudhuriwa na vijana wakubwa kwa wadogo.

 Ibada iliyoongozwa na Askofu Edir Macedo, mwanzilishi wa UCKG
Maelezo ya picha, Ibada iliyoongozwa na Askofu Edir Macedo, mwanzilishi wa UCKG

Kanda ya video iliyorekodiwa kisiri inaonyesha mchungaji akiwagawanya watu kwenye makundi kulingana na umri wao.

Mvulana, ambaye alimwambia mwandishi wa siri kwamba alikuwa na umri wa miaka 16 wakati huo, anaonekana akipokea kile kinachoonekana kama "maombi makali" kutoka kwa mchungaji. "Mungu wangu, acha moto wako uteketeze roho mbaya inayojificha," mchungaji anasema.

Kichwa cha mvulana huyo kinashikiliwa na mchungaji, kisha anaomba pepombaya ambayo imemuingia kijana huyo iondoke.

BBC ilimwonyesha Jahnine Davis, ambaye anakaa kwenye jopo huru la serikali la kuwalinda watoto.

Anasema: "Kwa kuzingatia kwamba kifo cha Victoria Climbie kilitokea zaidi ya miongo miwili iliyopita kulingana na picha ulizoshiriki, UCKG inatakiwa kujiuliza ni kiasi gani wamejifunza ktokana na tukio hilo.

"Sera za kulinda ni ni muhimu lakini hazina maana yoyote kama hazitekelezwi. Hazina maana."

Katika taarifa, UCKG ilisema: "Maombi ya nguvu... hasa yanafanywa katika huduma maalum za uokoaji" na "mtu yeyote aliye chini ya umri wa miaka 19 haruhusiwi" kushiriki. Ilisema inapinga vikali madai kwamba imekiuka sera yake ya ulinzi.

Ikiwa na zaidi ya matawi 30 nchini Uingereza, Kanisa la Universal Kingdom of God linadai kubadilisha maisha.

BBC Panorama ilizungumza na wanachama 40 wa zamani wa UCKG - baadhi yao waliondoka miaka kadhaa iliyopita, wengine katika miezi michache iliyopita.

Sharon alijiunga na ofisi ya tawi ya London Stratford alipokuwa na umri wa miaka 19.

Anasema alimwambia mchungaji kuhusu mfadhaiko wake wa kiafya na anasema hakuwahi kumshauri kutafuta usaidizi wa kitaalamu.

Alifanyiwa "maombi makali", anasema - kinyume na sera ya ulinzi ya UCKG, ambayo inasema hazipaswi kufanywa kwa watu wenye matatizo ya afya ya akili.

"Ilifika mahali niliogopa sana kwenda kwenye huduma hizo kwa sababu nilikuwa mmoja wa walengwa wakati wote," Sharon anasema.

Kanisa linasema "maombi yenye nguvu" hayakusudiwi kuwa ya kuogopesha au kudhuru na hakuna anayepaswa kuhisi kulengwa. Pia inasema ikiwa inafahamu kuwa "masuala ya afya ya akili yanahusika", "timu yake ya ulinzi husaidia kutathmini wanaostahili kuombewa".

BBC pia imezungumza na mshiriki wa zamani wa UCKG, "Mark" - ambaye aliomba kutotajwa jina kwa kuhofia jinsi kanisa litakavyochukulia hatua yake. Anasema alifanyiwa "maombi ya nguvu" kutoka akiwa na umri wa miaka 13 kujaribu kumweka sawa.

“Walipogundua kuwa nashiriki mapenzi ya jinsia moja walianza kuniambia kuwa ni shetani anayesababisha niwe hivyo, na kwamba natakiwa kuhudhuria ibada ya Ijumaa ambapo wangemtoa pepo huyo,” anasema.

Mark anasema maombi hayo yalifanyika kila wiki kwa zaidi ya miaka minne na kwamba alijaribu kujiridhisha kuwa anavutiwa na wanawake. "Ningelia hadi usingizi unibebe nilale," anasema. "Na ilikuwa wakati mgumu sana kwa sababu kiasi cha chuki binafsi kilikuwa kikubwa."

UCKG iliambia BBC kuwa "haifanyii tiba ya kubadilisha watu" na kwamba "maombi makali hayatolewi kwa masuala ya ngono au usawa wa kijinsia". Inaongeza kuwa "inakaribisha watu bila kuzingatia mwelekea wao wa kijinsia".

Katika ibada ya uponyaji iliyorekodiwa kisiri na BBC ambapo "maombi ya nguvu" yalifanyika, Askofu James Marques - kiongozi wa UCKG nchini Uingereza - anawaambia waumini baadhi ya magonjwa ni tatizo la kiroho na matatizo ya afya ya akili yanahusishwa na pepo mbaya.

Alimwambia mwandishi wa habari wa siri: "Unyogovu ni tatizo la kiroho. unyogovu unasababishwa na pepo mbaya."

Pia alisema, “Tunafahamu kuwa kifafa ni tatizo la kiafya lakini katika Biblia Bwana Yesu alitoa pepo mbaya ambaye alikuwa anasababisha kifafa.Hivyo tunaweza kuelewa kuwa kifafa kiuhalisia ni tatizo la kiroho ambalo lina udhihirisho wa kimwili unaoonekana. "

Katika taarifa, UCKG ilisema "sala zenye nguvu" kamwe "hazitolewi kama mbadala wa matibabu au... usaidizi wa kitaalamu".

Washiriki wengi wa zamani waliozungumzwa na BBC wanasema walipata changamoto sana kuachana na kanisani hilo.

Rachael, ambaye aliacha kanisa na sasa anaongoza kampeni dhidi ya UCKG, akionya juu ya hatari anayosema inaleta kwa vijana wengine.

BBC reporter Katie Mark taking part in a UCKG service with Pastor Miguel Conte
Maelezo ya picha, Mwandishi wa BBC Katie Mark akishiriki ibada ya UCKG sna mchungaji Miguel Conte

"Wanasema, 'Je, unamkumbuka yule msaidizi aliyekuwa ameketi hapa? Naam, waliacha kanisa na sasa wanapata talaka. Sasa wana saratani.'

Sharon anasema alionyeshwa video ya mshirika wa zamani ambaye alihusika kwenye ajali ya pikipiki iliyoonyesha "viungo vyao vyote vikiwa nje".

Anaongeza: "Walisema hivi ndivyo inavyotokea unapotoka kanisani, shetani atakuja na kuchukua roho yako."

Katika hafla iliyorekodiwa kwa siri na BBC, Alvaro Lima - mmoja wa maaskofu wa UCKG - anawaambia wafuasi kwamba mara tu baada ya kuondoka kanisani, "mama yangu aliugua sana, kutokana na saratani ya mapafu".

Lakini, alisema, baadaye alirudi kanisani "na sasa saratani inapungua na anazidi kupata nafuu".

UCKG iliiambia BBC kuwa "haitumii mbinu za kutisha", "inatokana na ibada (ya hiari)" na "haina nia yoyote ya kulazimishwa".

Kanisa linasema idadi kubwa ya washirika wake wa sasa wanaithamini kwa kazi nzuri inayofanya.

Lakini baadhi ya washirika wa zamani ambao BBC ilisema nao wanasema hawatarudi kwenye kanisa hilo.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi