Mlima Kilimanjaro: Mamlaka Tanzania zashirikiana na wananchi kuzima moto   

Iliyochapishwa

Mamlaka nchini Tanzania kwa kushirikiana na wananchi wanapambana kuzima moto uliozuka kwenye eneo la Karanga lilipo njia ya kupanda kilele cha Mlima Kilimanjaro.

 Chanzo cha moto huo ulioanza Ijumaa usiku bado haujafahamika.

 Moto huo umezuka kwenye njia ya kupanda mlima ya Mwika, mojawapo ya njia maarufu za kuelekea juu ya mlima huo mrefu zaidi Afrika.

  Kamishna wa Mamlaka ya Hifadhi Tanzania (Tanapa), William Mwakilema  amesema kuwa zoezi la kuzima moto huo linaendelea na linashirikisha askari wa hifadhi, wananchi na wadau wengine.

 "Taarifa zinaeleza moto huo unawaka ukanda wa Moorland, ambao mimea yake ikishika moto huwa ni hatari na tayari Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) na Hifadhi ya Kilimanjaro (Kinapa) wametuma vikosi kwenda kuukabili," alisema Kamishna huyo.

 Mashuhuda katika eneo hilo wanasema hewa nzito ya moshi na miali mikubwa ya moto inaonekana.

 Mlima Kilimanjaro ambao uko zaidi ya mita 5,800 kutoka usawa wa bahari ni miongoni kivutio cha kipekee barani Afrika.

Kisa cha moto katika Mlima Kilimanjaro mwaka 2020

 Hii si mara ya kwanza moto kutokea kwenye maeneo ya  Mlima Kilimanjaro.

Mnamo 2020, moto uliwaka kwa zaidi ya wiki na kuharibu maelfu ya hekta za msitu inayozunguka mlima huo.

 Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii wakati huo Hamisi Kigwangalla alieleza kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa upepo, nyasi kavu na vichaka vimekuwa changamoto kubwa na kuwa wataanza kutumia ndege na helikopta na ndege katika shughuli za kuzima moto huo.

Tanapa ilieleza kuwa  ukaguzi wa helikopta ulibainisha kuwa eneo kubwa lililoathirika na moto lilikuwa limedhibitiwa na kuwa maafisa kutoka idara ya zimamoto na Tanapa walifika katika meneo yote ambayo yaliathirika ili kudhibiti moto huo.

 

 Athari za moto katika Mlima Mlima Kilimanjaro mwaka 2020

Taarifa ya  Tanapa ilibainisha kuwa, moto huo uliathiri eneo la kilomita 95.5 sawa na asilimia 5 la hifadhi lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1700.