Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
WARIDI WA BBC: 'Unene huu umenipa umaarufu na nimejikubali'
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
Janet Wambui ni mwanamke wa miaka 41, mzaliwa wa Kenya . Kutokana na muonekano wake wa kuwa na mwili mnene kupita kiasi tangu akiwa binti mdogo alipewa majina mengi ambayo ameendelea kuyatumia kama msanii nchini humo. Mwili wake umesaidia kuwa msanii kutokana na nafasi anazoigiza zinazohitaji mwanamke mwenye umbo kubwa.
Ni kwanini wananiita ‘momo au biggie’
Mama huyu wa watoto wawili anasema kuwa amekuwa na mwili mkubwa tangu alipokuwa mtoto mdogo, anapoulizwa iwapo unene huu ni kitu ambacho kiko kwenye familia yao anasema kuwa huenda alirithi muonekano huo kutoka kwa baba yake mzazi ambaye pia ni mnene wa mwili .
”Kwetu tumezaliwa tukiwa watoto sita, mmoja wetu alifariki kwa hiyo tumesalia watano, ila kwa wote mimi ndio mtoto pekee niliyezaliwa mnene nadhani kwamba nilirithi kwa baba yangu, ila halinisumbui kabisa ”anasema Wambui.
Anasema kuwa jina lake maarufu la MOMO lilitokana na hatua yake ya kuingia kwenye sanaa ya kuigiza katika nyimbo za kiasili za jamii ya Agikuyu nchini Kenya. Video ya kwanza ambayo ilimpatia umaarufu aliigiza kama mwanamke mnene, wimbo wenyewe ukifahamika kama MOMO unaeleza pandashuka za kuwa mwanamke mnene, baada ya wimbo huo kuzinduliwa ndipo watu nchini Kenya walianza kumfuatilia kama msanii.
”Nadhani wengi walikuwa wanazuzuliwa na muonekano wangu , ni kitu ambacho nilikizoea tangu nikiwa binti mdogo .Nilizoea kutizamwa kila nilipokuwa ninatembea. Na kwa hiyo sijaona ugumu wa kuwa mnene bali nafurahi kwani ni muonekano ambao umenipa nafasi ya kutafuta riziki ”anasema Wambui.
Baada ya wimbo huo wa Momo , alianza kupata nafasi kadha wa kadha za kuigiza ikiwemo kwenye baadhi ya tamthilia za Kenya, na pia kuigiza nafasi ambazo zinaangazia maisha ya watu wanene katika vipindi na wasanii mbalimbali nchini Kenya.
Maisha ya utotoni
Mwanadada huyu anazungumza kwa njia ya kujikubali anaposimulia maisha yake ya utotoni , alilelewa kama watoto wengine ila anakumbuka kuwa yeye alikuwa mnene tangu alipoingia shule ya chekechea, shule ya msingi na hata sekondari .
”Nakumbuka mama akiniwekea bakuli mbili za chakula, kwa kuwa shule yetu ilikuwa mbali nilikuwa natembea huku nikila chakula changu , bakuli ya pili ilikuwa ni chakula cha mchana na mama alihakikisha kuwa mwalimu alikuwa anakiweka nisije nikakila chote ”anakumbuka Wambui
Shuleni anasema kuwa hakupata ugumu , kwani alikubalika na waalimu na hata wanafunzi. Aidha anasema kuwa hatua ya kwanza ya mtu kukubalika na wengine licha ya utofauti wake na watu wanaomzunguka ni pale yeye mwenyewe anapojikubali na kuishi bila wasiwasi wa muonekano wake .
Huku akitabasamu anaeleza kuwa mambo ambayo aliyafurahia katika shule ya sekondari ilikuwa pamoja na kuwa aliteuliwa kama kiranja wa bweni , anasema kuwa muonekano wa mwili mnene ulimuweka kwenye nafasi nzuri ya kuwa kiongozi ambaye alikuwa anahakikisha kuwa wanafunzi wenzake wanamfuatilia sheria za bweni na hata za shule kijumla.
”Nikiwa sekondari , nilikuwa nafurahi kwa kuwa unene wangu ulizuia wanafunzi kuiba nguo zangu kwani hazingewatosha , nilikuwa mwanafunzi mnene zaidi shuleni sasa mwanafunzi akiiba nguo zangu au soksi atazivalia wapi ”anasema Wambui
Maisha ya utu uzima
Wambui anasema kuwa aliolewa pindi tu baada ya kukamilisha shule ya sekondari na alijaaliwa kupata watoto wawili , japo hajakuzia mengi kuhusiana na mahusiano yake na kwanini walitengana na mume wake anakubali kuwa mahusiano huwa na changamoto nyingi licha ya hayo alijizatiti kuwalewa wanawe wa kiume kwa njia iliyobora sana .
Kwa upande wa Afya yeye anasema kuwa hadi sasa hajajikuta akipitia changamoto zozote za kiafya na kuwa anauwezo wa kufanya kazi zake zote bila usaidizi wa watu .
Kinachoonekana kuwa changamoto kwake ni baraka.
Wambui anasema kuwa mtazamo wa wengi katika jamii ni kuwa wanawake kwa waume ambao wana unene wa kupitiliza ni watu wanyonge na ambao hawapendi kufanya kazi .Ila kwake anasema kuwa hakuna kazi zozote ambazo zinamlemea , kwa mfano anasema kuwa katika fani ya kuigiza huwa anatakikana kufanya mbwembwe za hapa na pale na hakuna ambacho kinamshinda.
Licha ya maisha ya kujikubali ni kuwa hajakosa watu katika jamii ambao wanamsimanga kwa muonekanano wake .
”Nilikuwa katika sherehe moja, pindi nilipoingia yule mshereheshaji akaniona na kusema , ‘huyu mama hahitaji chakula tayari ameshiba ‘! maongezi kama hayo kwa kawaida yalifaa kunikasirisha ila mimi nacheka tu , mbona nikasirike na mtu anazungumza anachokifikiria moyoni ”anasema Wambui.
Kile ambacho kingekuwa changamoto katika upande wa kusaka mavazi yake kwani anafaa kuvaa mavazi makubwa, anasema kuwa uzoefu wake na wachuuzi na wauza nguo unampa nafasi ya kupata nguo bila bugudha yoyote , katika pita pita zake mitaani anasema utasikia mchuuzi amesema yake ”hii hapa dada ni saizi ya kwako ”.
Anacheka kwa mara nyengine tena anapozungumza kuhusu msisitizo wake anapotembelea maeneo mbalimbali ya kuwa watu wahakikishe kuwa viti anavyokalia ni imara, kwani uzito wake umesababisha kuvunjika kwa viti vingi hasa vya pastiki .
Sawa na kitanda anacholalia anasisitiza kuwa lazima kiwe kimesitiriwa na mbao imara na za kutosha, na mwishowe inapowadia wakati wa kutumia usafiri wa umma Wambui anasema kuwa amekubali kuwa yeye ni mnene na kwa hiyo yuko radhi kulipa nafasi ya watu wawili na haoni shida kwa kufanya hivyo.
Yote tisa kumi Wambui anasema kuwa amekuwa na mpango wa kuanzisha miradi inayohusu wanawake na mabinti ambao ni wanene katika jamii ilikutoa nasaha na motisha kwani anaelewa kuwa wakati mwengine watu hubaguliwa sana kwa muonekano kama wake, na mara nyingi wanakuwa watu wa kukaa nyumbani kwa kuogopa kutangamana na watu ..