Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Amritsar: Mji wa India ambako watu hawalali njaa
Amritsar, mji wa Kaskazini mwa India wenye wakazi milioni mbili, ni maarufu kwa mambo mengi; vyakula vitamu, mji mkongwe na hekalu la kuvutia la dhahabu – sehemu takatifu kwa dini ya Sikh. Ila kile kinachoyazidi hayo yote, kuanzia hekalu na watu mtaani, ni hisia za ukarimu ambazo zina muingiliano na kuanzishwa kwa mji huo.
Amritsar ulianzishwa karne ya 16 na kiongozi wa kiroho (guru) wa Sikh, na unapatikana katika mkoa wa Punjab ambako Usikh ndiko ulikotokea. Dini hiyo inajuulikana kwa utamaduni wa ‘kuhudumia,’ – huduma ya kujitolea kuhudumia wengine bila ya kutarajia malipo.
Wafuasi wa Sikh duniani kote hutoa huduma katika mahekalu, kwa kufanya matendo ya kawaida kama vile kusafisha sakafu, kutoa chakula, na kusimamia ulinzi katika hekalu. Wengine hutoa huduma katika maisha yao binafsi, kwa matendo ya ukarimu na misaada.
Aprili 2021, wakati Covid-19 ilipoharibu familia kote India, jamii ya Sikh ilianzisha wito wa kutoa mitungi ya oxygen na vifaa vingine vya matibabu kwa wenye uhitaji.
"Kuhudumia kwa dini ya Sikh, haina maana wakati wa wito na mwongozo tu, ni tendo la kila siku,” anaandika Jasreen Mayal Khanna katika kitabu, “Kuhudumia: Busara za Kisikh ili Kuishi vyema kwa kutenda mazuri,” (Seva: Sikh Wisdom for Living well by Doing Good.)
“Jina jingine la kuhudumia ni upendo,” anasema Abhinandan Chaudhary (23), ambaye amekuwa akitoa huduma na familia yake tangu akiwa na miaka nane. “Mafunzo ya msingi ni mtu kuwa msiri na kukinai, kwamba ukitoa huduma kwa mkono wa kushoto hata mkono wa kulia haupaswi kujua.”
Hiyo ni namna bora ya kuishi - katika ulimwengu huu ambao ubinafsi na ubepari unazidi kuongezeka.
Roho ya ukarimu katika Usikh inaweza kuonekana kote ulimwenguni. Wakati wa karantini ya Covid-19, wafuasi wa Sikh walijitolea katika mahekalu huko England kutoa maelfu ya milo kwa wafanyakazi wa huduma ya taifa ya afya (NHS). Katika majiji mbalimbali Marekani walipika maelfu ya milo na kuitoa bure.
Katika migogoro au hali ya dharura, wafuasi wa dini hiyo wamekuwa wakikusanya nguvu zao na kusaidia wenye uhitaji, iwe kimbunga kimepiga Canada au kimepiga New Zealand.
Katika mji wa Amritsar
Huko Amritsar, eneo muhimu la dini ya Sikh, utimizaji wa kuhudumia hufanywa kwa kiwango kikubwa zaidi. Inajulikana kote India kwamba hakuna mtu anaye lala na njaa Amrtsar. Siku zote kuna chakula moto tayari kwa yeyote anayetaka kula katika hekalu la dhahabu. Eneo takatifu kwa dini ya Sikh.
Mlo katika Hekalu la Dhahabu ni bure, jiko la jumuiya ambalo ni kubwa zaidi duniani linalohudumia watu 100,000 kwa siku – siku saba kwa wiki. Kila mmoja anakaribishwa kula, bila ya ubaguzi, maadamu wanahitaji hifadhi na chakula. Chakula kinapatikana masaa 24 kwa siku.
Mpishi kutoka New York, Vikas Khanna ambaye aligawa mamilioni ya milo kote India wakati wa karantini ya Uviko 19, anaeleza, “nilizaliwa na kukulia Amritsar, kuna jiko kubwa la jumuiya na kila mmoja hupata kula. Mji wote unaweza kula huko. Njaa niliipata hapa New York, wakati nahangaika nikianza maisha.”
Kama ilivyo katika maeneo yote ya ibada ya Kisikh, Hekalu la Dhahabu linaendeshwa vizuri na adabu kwa nguvu kubwa ya watu wanaojitolea – ambao huhudumia chakula cha kawaida lakini kitamu; mchuzi wa adesi na chapati, mchuzi wa mbaazi na mtindi katika sahani za bati.
Watu hukaa kwa kukunja miguu katika sakafu ndani ya ukumbi mkubwa ambao unaweza kubeba watu 200 kwa wakati mmoja, wanawake na wanaume, vijana na wazee, masikini na matajiri.
Wakati watu wengine huomba kuongezwa chakula, wengine humaliza na kuondoka. Kila baada ya dakika kumi na tano, au zaidi, wahudumu wa kujitolea, husafisha ukumbi kwa raundi nyingine. Ni mzunguko usio kwisha wa kuhudumia na kula.
Pembeni ya hekalu hilo, watu katika mitaa, urafiki, ukarimu, kusaidiana ndio uhalisia wa Amritsar. Tulipo tembelea, tabasamu zilitufuata. Ukionekana tu umepotea au kuchanganyikiwa ni rahisi kuona mtu anakufuta na kukuuliza ikiwa anaweza kukusaidia. Tulipotembea nyakati za usiku, mpita njia tusiyemjua alitwambia tuwe waangalifu na mabegi yetu katika maeneo yenye watu wengi.
Tulipowasili Kesar da Dhaba, mkahawa maarufu – wenye foleni kubwa, watu walijibanza pembeni karibu na meza ili kutupa nafasi ya kupita. Hisia za kukaribishwa na kushirikishwa zilikuwa wazi. Jicho la urafiki na tabasamu lilitosha kwa watu kutuita, kula na kuzungumza kuhusu maisha yao.
“Nilikulia Amristar, kulikuwa na hisia za maisha ndani ya jamii kubwa,” anasema Rahat Sharma, ambaye alizaliwa na kukulia huko. “Nilikulia kucheza michezo ya kificho ficho katika hekalu la Dhahabu, ambako sote tulikuwa tunatoa huduma.”
“Kila mmoja alikuwa mwangalizi wa mwingine, waumini wa Sikhi na Uhindu, imani kuu katika mji, zimekuwa pamoja kwa muda mrefu, licha ya mikinzano ya tofauti za kisiasa.”
Mji unavutia ingawa ni mkongwe, vichochoro vyembamba vinauzunguka mji, makutano ya barabara na viwanja vidogo, mji uko hai na masoko yenye watu. Ingawa, katikati ya moyo wa ukarimu wa Amritsar na tabia njema, kuna historia mbaya ambayo ni sura muhimu inayounda mji huu, pia na dini ya Sikh.
Amritsar na nyakati za dhiki
Likiwa ni jiji la pili kwa ukubwa katika Punjab, Amritsar mara nyingi ulikuwa ni kitovu ya mikutano na maandamano wakati wa ukoloni wa Uingereza. Tukio moja lililogeuka msiba, ni 1919 , majenerali wa Uingereza walipotoa amri ya kufyatua risasi katikati ya mkutano wa amani, baadaye yalijuulikana kama mauaji ya Jallianwala Bagh, takribani watu 1,500 walifariki.
Vilevile, Uingereza ilipoondoka India – 1947, vurugu zilizopeleka kugawika kwa India ziliathiria kwa kiasia kikubwa Amritsar, kutokana na eneo hili kuwa karibu na mpaka mpya uliochorwa. (Kwa sababu hiyo, makumbusho pekee kuhusu kugawika India, yalifunguliwa Amritsar 2017.)
1984, Amritsar kwa mara nyingine ilikuwa sehemu ya maafa. Operesheni ya kijeshi iliyoamriwa na Waziri Mkuu, Indira Gandhi ilihusisha kuvamia Hekalu la Dhahabu, kuwatoa wanaotaka kujitenga. Ilipelekea kuuawa kwa Gandhi na walinzi wake wawili miezi michache baadaye, na kufuatiwa na mauaji ya maelfu ya masikh kote India.
Ni muhimu kwa Sikh kuhifadhi kumbukumbu za matukio hayo, hadithi za mashahidi wa Kisikh ni kumbukumbu kubwa katika tamaduni zao, huwasoma katika swala na ibada.
“Lakini matukio haya hayakuelezwa ili kuhamasisha chuki au kutafuta kulipiza kisasi. Ni kutilia mkazo kwamba urithi wetu ni ulinzi wa nchi.” Khanna ameandika.
Inapendeza zaidi kuona jamii iliyoumia sana na kumbukumbu za kutisha, inatoa sana na kukubali watu wote. Kwa mujibu kwa Khanna tabia hii ni jumla ya Usikh.
“Guru Nanak, (mwanzilishi wa Usikh), alitoa kama huduma wimbo wa Sikh. Sikh huchagua kukinai kama sehemu ya maisha yao, ikichochewa na matendo na maneno ya viongozi wao wa kidini.”
Utamaduni wa kukubali watu na kuwakaribisha bila kujali imani na itikadi zao, ni agano la ukarimu wao – na kwa mji ambao unabeba hisia hizo kwa njia ya mfano. Huko Amristar, hata mambo yawe mabaya na ya kiza kiasi gani, daima roho ya wema, upendo na ukarimu huonekana kushinda.